Kurunzi ya falsafa inayoangazia bila woga masuala mazito yanayoiathiri jamii.
Matukio yanayoendelea ndani ya chama cha UDA ni dhihirisho tosha la umbali wa safari yetu kuwa na vyama vya kisiasa vyenye sera na msimamo. Vyetu ni vyama vinavyotumiwa tu kuwa daraja la kuingia mamlakani na baada ya uchaguzi, kudondoshwa kama kaa moto.
Bunge la Kitaifa linaanza kuwapiga msasa Mawaziri walioteuliwa na Rais William Ruto, katika Baraza jipya alilotangaza. Hii ni fursa adimu kwa Bunge kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba na kuonesha kuwa ni taasisi huru na inayojisimamia bila kushurutishwa na Serikali tendaji. Hii ni fursa ya Bunge kusafisha jina lake ambalo limekuwa si lolote la kujivunia.
Chama cha ODM kimeendelea kutoa msimamo kinzani kuhusu hatua ya viongozi wake wakuu kujumuishwa serikalini, na kuibua kumbukumbu ya hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi ya Wabunge wake waliotangaza msimamo wao wa kushirikiana na serikali baada ya Uchaguzi Mkuu uliopita. Je, viongozi hawa wakuu wa chama hiki watachukuliwa hatua zozote. Kama sivyo, basi tusihadaiwe zaidi.
Maandamano yaliyofanywa na wanahabari nchini hayashinikizi lolote nje ya Katiba ya nchi. Yanashinikiza tu taaluma ya uanahabari kuheshimiwa na haki za wanahabari kulindwa kama ilivyo katika sheria za nchi. Wanahabari sio wahalifu, wao ni mwito wa kuitumikia nchi na wananchi wake.
Maandamano yanayoendelea dhidi ya serikali yanamaanisha kuwa Rais William Ruto atastahili kuwasikiliza zaidi vijana wanaoandamana. Kusikiliza huku hakuwezekani katika mazingiraya kujipiga kifua na vitisho. Kusikiliza huku ni zaidi kupitia kwa matendo.
Harakati ambayo imekuwa ikiendelezwa dhidi ya serikali lazima ikuze taifa linalosikiliza. Linalosikiliza kwa lengo la kuelewa, na kukumbuka kuwa serikali ni raia na sio vinginevyo. Government by the people, for the people...
Maandamano dhidi ya serikali yameingiliwa na wahuni ambao nia yao ni kupora, kujeruhi na hata kuua na kuharibu. Jumatano wiki hii, wahuni pia wametatiza mkutano wa Azimio, wakisababisha purukushani na majeraha kwa wanahabari. Ni wakati wahuni hawa na wafadhili wao wakabiliwe vilivyo.
Kukamatwa kwa mwanahabari mtajika Macharia Gaitho katika mazingira ya kudhalilisha na kuhujumu haki za mtu, siku moja tu baada ya mwanahabari wa Kameme kufyatuliwa risasi na polisi huko Nakuru alipokuwa akiangazia maandamano dhidi ya serikali kunaonesha kuchipuka tena kwa majaribio ya kudunisha uhuru wa vyombo vya habari unaolindwa Kikatiba. Kamwe tusikubali hilo kufanyika, uhuru wa wanahabari na vyombo vya habari ni mhimili muhimu mno wa demokrasia ya Kenya.
Tukio la kufyatuliwa risasi mwanahabari wa Kituo cha Kameme Nakuru Wanjeri wa Kariuki katika maandamano dhidi ya serikali ni mfano hai wa majaribio ya serikali kuwalenga wanahabari, kwa lengo la kuwanyamazisha wasitekeleze wajibu wao ambao unalindwa na Katiba ya Kenya. Kamwe hatuko tayari kurudisha nyuma hatua kubwa zilizopigwa katika kukuza demokrasia na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari.
Tukio la kupatikana miili zaidi ya tisa eneo la Kware, Embakasi ni dhihirisho tosha la nchi ambayo taasisi zake za kiusalama hazifanyi kazi, zimefeli pakubwa. Iweje watu wauliwe na miili yao kutupwa bila NIS, DCI au Idara ya Polisi kuwa na ufahamu ya tukio hilo la kihalifu? Tunataka uwajibishwaji wa ofisi husika.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amewaandikia Mawaziri wote kuwataka kupunguza idadi ya washauri kutoka wawili hadi mmoja kwa kila Waziri ili kupunguza matumizi ya pesa za serikali. Hatua hii imeibua swali la hivi hawa washauri wamekuwa wakifanya kazi gani ikiwa kwa kipindi cha miaka miwili serikali hii imekuwa ikifanya baadhi ya maamuzi mabovu mno, kiasi cha kugeuka na kuwa shubiri kiasi hiki? Je, washauri hawa wamefeli katika majukumu yao au ushauri wao umekuwa ukipuuzwa na viongozi wanaoshauriwa?
Miaka sitini tangu kupata uhuru uongozi wa nchi ya Kenya umekuwa ukiendeshwa na wanasiasa wabinafsi wasiomjali yeyote ila maslahi yao tu. Hali inaonekana inabadilika na sasa wananchi wataanza kujiamulia wanavyotaka kuongozwa. Hilo lifanyikapo, basi ole wao hawa wanasiasa. Interesting times ahead!
Maafisa wa Kliniki wametamatisha mgomo wao ambao umedumu siku 99 baada ya mapatano kati yao na Baraza la Magavana COG. Hii ni nafuu kubwa kwa Wakenya ambao hutegemea huduma katika hospitali za umma, japo inatoa changamoto kwa serikali kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwa migomo hii ya mara kwa mara katika sekta ya afya.
Sepetuko leo inahongera serikali kwa hatua yake ya kubadili mwenendo na kuanza kuwasikiliza raia. Ni katika kuwasikiliza raia ndipo serikali itaweza kuafiki mengi, na sio katika kuwapuuza wananchi ambao ndio wenye serikali.
Viwango vya unyenyekevu miongoni mwa wanasiasa wetu, ambavyo vinashuhudiwa baada ya maandamano na harakati za vijana wa kizazi cha Gen Zs na wengine ni mfano hai wa uwezo wa watu. Yaani hadi wanasiasa wetu wenyewe wanakataa nyongeza ya mishahara waliyokuwa wameongezewa na Tume ya Utathmini wa Mishahara na Marupurupu SRC! Huu unafaa kusalia kuwa mkondo. Wanasiasa kujua kuwa kuipuuza sauti ya mwananchi ni kujiweka taabani.
Maandamano yanayoendelezwa nchini dhidi ya serikali yanalindwa na Katiba ya Kenya, bora tu yafanywe kwa amani. Inasikitisha kuwaona wahuni wakihitilafiana na maandamano haya, kuwapora Wakenya mali yao waliyoitafuta kwa jasho lao. Wacha watuhumiwa hawa wasakwe na kukabiliwa na mkono wa sheria kutokana na shughuli zao za kihalifu. Hawa sio sehemu ya waandamanaji na kamwe hawafai kuchukuliwa hivyo.
Visa vinavyoendelezwa na serikali vya kuwateka nyara vijana na wanasiasa wanaohusishwa na maandamano dhidi ya serikali yanatia shubiri uwezekano wa kufumbua fumbo hili. Zaidi ni uhuni ambao ni kinyume kabisa na sheria za nchi. Amani haipatikana kwa kiganja kilichofumbatwa.
Sehemu kubwa ya matatizo yanayokumba serikali hii ni Wakenya kukosa imani kwake kutokana na kuwapo Rais asiyependa ukweli. Rais ambaye hadi leo amekwama katika uongo wa kuwatetea maafisa wa usalama waliohusika katika ukatili dhidi ya waandamanaji. Rais anayesema hili, kisha naye anafanya jingine. Ni hadi Rais Ruto amaanishe ayasemayo, afanye anayosema na ajifundishe kusema ukweli ndipo hali hii ya sasa itaimarika.
Vijana wa Gen Zs na vijana wengine ambao wamekuwa wakiendeleza maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka wa 2024 wametukumbusha uwezo tulio nao kama wananchi wapigakura. Uwezo wa kupiga kura kuwachagua viongozi wetu, lakini zaidi kuwawajibisha wanapokuwa ofisini. Harakati hii haifai kukoma. Huu unafaa kuwa mwanzo tu wa kutetea Katiba yetu na kudai uongozi bora ambao tunastahili.
Hatua ya serikali kuwatuma wanajeshi kusaidia polisi kuwakabili waandamanaji ni ukiukaji mkubwa wa sheria za nchi. Inasikitisha kuwa Bunge la Kitaifa limetumiwa kutia muhuri uhayani huu! So unfortunate!
Tukio la vijana waliokuwa wakiandamana kuingia katika majengo ya Bunge kamwe sio la kushabikiwa. Hata hivyo, tukio hilo na mengine ya waandamanaji kuharibu mali ya umma na kibinafsi hayatoi sababu tosha kwa maafisa wa usalama kuwafyatulia risasi na kuwaua waandamanaji. Hayatoi sababu kwa Rais kuwaita Wakenya kuwa wahalifu na wahaini.
Maandamano yanayoendelezwa dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka wa 2024 ni ukumbusho kwa serikali kuhusu jinsi sauti ya vijana imekuwa ikipuuzwa. Vijana wanakumbwa na changamoto mbalimbali, kuu miongoni mwazo, ikiwa ni ukosefu wa ajira nchini. Serikali haina budi kutafakari mbinu mahsusi ya kutatua hili na changamoto nyingine zinazowakumba vijana.
Serikali sasa imegundua kuwa haiwezekani kupuuza maandamano yanayoendelezwa na kizazi cha vijana dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka wa 2024. Rais mwenyewe amekiri kuwa ipo haja ya kufanyika mazungumzo kati yake na vijana hawa. Kiukweli, hakuwa na budi. Kuanzia mwanzo haingewezekana tu kuwapuuza vijana hawa kutokana na sababu kadhaa.
Kuandamana ni haki ya wananchi wa Kenya, na inalinda na Katiba ya sasa ya nchi. Bora tu maandamano haya yafanywe kwa amani bila kuvuruga usalama. Hatua ya maafisa wa usalama kuwakabili waandamanaji wanaoandamana kwa amani ni uvunjaji wa sheria.
Maandamano yanayoendelezwa na Wakenya dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka wa 2024 ni zaidi ya Mswada wa Fedha. Ni dhihirisho la kutaabika kwa muda mrefu ambako Mkenya amekuwa akipitia mikononi mwa serikali isiyojali na inayowadharau, kwa miaka. Hii ni sababu tosha ya serikali kuwa na wasiwasi.
Maandamano ya Wakenya dhidi ya Mswada wa Fedha yahweh onyo kwa serikali. Onyo kuwa wananchi wamejifundisha kujitetea na kutetea haki yao wanapohisi kuhujumiwa. Kinyume na maandamano ya miaka ya nyuma, haya yanaongozwa na Wakenya wenyewe, na sio wanasiasa.
Mwenendo wa Wabunge wetu wakati wa kufanya maamuzi muhimu yanayomhusu Mkenya wa kawaida ni dhihirisho tosha la maamuzi duni ambayo huwa tunafanya Bungeni. Haimhitaji mpigakura kumtumia arafa Mbunge ama kuandamana ili wafanye maamuzi bora ya kutuwakilisha. Tujifundishe kitu, inatupasa kufanya maamuzi bora debeni siku za usoni.
Heko kwa Junior Starlets kwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa wanawake chipukizi chini ya miaka 17. Historia iliyoje! Junior Starlets inakuwa timu ya kwanza kabisa ya Kenya ya kandanda kufuzu kwa Kombe la Dunia. Maandalizi ya kushiriki kombe hilo yaanze sasa.
Makadirio ya Bajeti ya Mwaka wa Kifedha wa 2024/2025 yalisomwa Bungeni na Waziri wa Fedha Njuguna Ndungu. Katika makadirio hayo ya jumla ya shilingi trilioni 3.99 lipo pengo la shilingi bilioni 600. Pengo hili lazima likutie wasiwasi. Unajua kwa nini?
Suala la mafao ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta halistahili jopo, ni suala ambalo sheria za nchi zinatosha katika kulitatua. Kenyatta anauliza kipi kilifanyika kwa mgao wake wa bajeti kwa miaka miwili, kwa mfano, haihitaji jopo kujibu swali hilo.
Suala la mafao ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta halistahili jopo, ni suala ambalo sheria za nchi zinatosha katika kulitatua. Kenyatta anauliza kipi kilifanyika kwa mgao wake wa bajeti kwa miaka miwili, kwa mfano, haihitaji jopo kujibu swali hilo.
Hujuma anayopitishiwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta na ofisi yake ni aibu kubwa kwa taifa hili. Rais William Ruto anamkosea heshima Kenyatta na Wakenya wote kijumla kwa kupuuza maslahi ya Kiongozi wa nchi ambaye aliihudumia nchi hii kwa miaka kumi. Ikiwa hujuma hii inatokana na uhasama wa kisiasa wa uchaguzi mkuu uliopita, basi shame on this Government.
Ukabila bado ni sumu hatari inayokumba Kenya na Wakenya. Wacha Rais na Naibu wake waoneshe mfano bora katika kutokomeza jinamizi hili na sio kuanzisha siasa za kimaeneo ambazo kwa kiasi kikubwa zinatishia kuigawanya nchi.
Kuchaguliwa kwa mwanamke kuwa Rais wa Mexico ni dhihirisho tosha la jinsi mtazamo wa watu unaweza kubadilika na wakaukumbatia uongozi wa wanawake. Naamini ipo siku Kenya itakuja kutimizwa ndoto hii ya wanawake wengi kuchaguliwa katika nyadhfa za uongozi. Ipo siku.
Juhudi zinazoendelezwa na Naibu Rais Rigathi Gachagua kusukuma ajenda za eneo la Mlima Kenya zinahujumu azma ya tiketi ya Urais kuwa nembo ya umoja wa nchi nzima na sio eneo moja. Naibu Rais anafaa kuhudumia nchi nzima na sio kujikita tu katika eneo anakotoka.
Madai ya Rais William Ruto kuwa sehemu ya ziara yake kuenda nchini Marekani ilifadhiliwa na marafiki zake ni kinyume na Katiba ya Nchi. Waliomfadhili Rais ni kina nani na walifanya hivyo kwa nia gani?
Kuendelea kwa serikali kuongeza ushuru wanaotozwa wafanyabiashara kunatishia kuwatorosha waekezaji hadi mataifa mengine. Serikali ilenge kupanua idadi ya walipaushuru, sio kuwatoza walipaushuru waliopo ushuru zaidi ya uwezo wao.
Vikao vinavyoendelea vya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Mswada wa Fedha wa mwaka wa 2024 visiwe tu kwa nia ya kujifanya kuheshimu Katiba. Wacha maoni ya Wakenya yatiliwe maanani na kuheshimiwa.
Hatua ya kuwatuma maafisa wa Polisi Haiti ni uamuzi usiokuwa wa hekima. Ni uamuzi ambao hauwezi kuelezwa kwa njia nyingine yoyote ile, isipokuwa kuonesha ubaraka kwa taifa la Marekani na washirika wake. Na hilo litakuja na athari zake mbovu kwa nchi.
Rais William Ruto amejitetea kuhusiana na hatua yake kutumia ndege ya kibinafsi kusafiri hadi nchini Marekani, akidai kuwa kufanya hivyo kulikuwa kwa gharama ya chini kuliko kutumia ndege za Shirika la Ndege la Kenya Airways. Kujitetea huku kuionesha serikali hii kuwa isiyojali kuhusu utunzaji wa Mali ya umma na pia maafisa wakuu wa serikali hawana Imani na huduma zinazotolewa katika mashirika ya serikali kama KQ. Inasikitisha mno!
Ziara ya Balozi wa Uingereza Nchini Kenya kwa familia ya Mkenya Agnes Wanjiru aliyetuhumiwa kuuliwa na mwanajeshi wa Uingereza kwenye kambi ya Jeshi ya Uingereza iliyoko Nanyuki uwe mwanzo wa kupatikana kwa haki kwa Wanjiru na waathiriwa wengine wa hujuma mikononi mwa wanajeshi wa Uingereza waliomo nchini.
Jinsi serikali inashughulikia mgomo wa walimu wa JSS kunaonesha serikali isiyojali. Mbona tunachezea elimu ya watoto wetu? Mbona suala hili halifanywi kipaumbele?
Gumzo la mgao wa fedha za serikali na maendeleo kutolewa kwa msingi wa idadi ya watu, linatishia kurejesha nyuma hatua ambazo zimepigwa kuhakikisha ujenzi wa Kenya moja. Jamii zote zinazoishi Kenya zinastahili kujihisi kuwa nyumbani, bila kujalisha idadi yao.
Pendekezo la serikali kufutilia mbali mpango wa lishe shuleni sio la hekima. Linatishia kurejesha nyuma hatua zilizopigwa katika kuhakikisha wanafunzi kutoka maeneo kame, mitaa ya mabanda na maeneo mengine yaliyosalia nyuma kimaendeleo wanapata elimu.
Mapendekezo yaliyomo kwenye Mswada wa Fedha wa mwaka wa kifedha ujao yanaonesha wazi kuwa serikali ya Kenya Kwanza haina ufahamu wa hali halisi ya Mkenya. Haijali kuhusu vipaumbele vya Mkenya. Lakini, nani aliiweka serikali hii mamlakani kama sio Mkenya yuyu huyu. Huwa tunauliza maswali kuhusu nani atafadhili ahadi chungu nzima zinazotolewa na wanasiasa wakati wa kampeini?
Rais William Ruto amekariri kuwa analenga kupandisha hata zaidi ushuru anaotozwa Mkenya, eti ili kupunguza deni la taifa. Sepetuko inamkumbusha Rais kuwa tatizo la Kenya sio la kimapato, ila ni mianya iliyopo ya uporaji wa mali ya umma.
Mswada wa Fedha wa Mwaka wa 2024/2025 una baadhi ya mapendekezo ambayo kimsingi yatamuongezea Mkenya mzigo wa ushuru ambao tayari ni mzito. Sepetuko inakariri kuwa kamwe haiwezekani kwa nchi kujiendeleza kupitia kuwatoza wananchi wake kodi nyingi! Haiwezekani.
Shule zinapofunguliwa kwa masomo ya muhula wa pili, Sepetuko inairai serikali kuangazia masuala kadhaa kwenye sekta ya elimu. Miongoni mwa masuala hayo ni kucheleweshwa kwa fedha za serikali za kufadhili elimu, na changamoto zinazokumba elimu ya JSS.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Fiji Frank Bainimarama amefungwa jela kwa kuzuia uchunguzi wa ufisadi. Hapa Kenya, vita dhidi ya ufisadi havijazaa matunda aina hii, na kuibua swali la inawezekanaje kwa mwanasiasa wa haiba hii kufungwa jela. Sepetuko inakariri kuwa vita dhidi ya ufisadi haviwezekani ikiwa yetu ni kuwatetea na hata kuwachagua kwa nyadhfa za juu wanasiasa mafisadi.
Wabunge wana nafasi ya kuwadhihirishia Wakenya kuwa yao ni taasisi huru katika hoja ya kumbandua Waziri wa Kilimo Mithika Linturi iliyoko mbele yake. Hii ni fursa ya kuubaini ukweli na kutoa uamuzi wa haki kwa Linturi, lakini zaidi kwa Wakenya ambao huenda wakadhurika kutokana na wakulima kuuziwa mbolea ghushi.
Wakenya wanaoishi kwenye maeneo ya mito na mabwawa ya maji wameendelea kuhamishwa kutokana na mafuriko yanayoendelea nchini. Sepetuko inauliza noani waliidhinisha ujenzi wa makazi ya watu kwenye maeneo haya. Je, wapo maafisa wa serikali waliotepetea na kuzuru ujenzi huu, na ikiwa ndiyo, ni haki wawajibishwe kisheria.