Place in Paphos District, Cyprus
POPULARITY
Categories
Katika jarida la habari za Umoja wa Mataifa hii leo utasikia kuhusu wito wa mataifa yote kuwekeza kwenye mifumo ya tahadhari za mapema ikiwa leo dunia inaadhimisha Siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu Tsunami. Utasikia pia ziara ya Rais wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa nchini Qatar ambapo amewatembelea wakimbizi wa kipalestina walioko nchini humo. Kutoka nchini Kenya utasikia juhudi za taasisi ya FODDAJ kusaidia jamii nchini Kenya kupambana na ukatili wa kijinsia.
leo ni siku ya kimataifa ya kuelimisha umma kuhusu Tsunami Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika kujiandaa dhidi ya mawimbi hayo makubwa ya bahari yanayotokana na tetemeko chini ya bahari. Anold Kayanda na maelezo zaidi.Asante Assumpta,Katika ujumbe wake, Guterres amesema maandalizi hayo yanahusisha kuweka mifumo ya kutoa maonyo ya mapema au tahadhari kwenye kila ufukwe, jamii na kokote kule.Bwana Guterres amefafanua kuwa tsunami si matokeo ya mara kwa mara lakini pindi yanapotokea madhara yake yanaweza kuwa makubwa na hata kusababisha vifo.“Husababisha vifo vya maelfu na hata mamia ya maelfu ya watu. Lakini kuna mbinu za kuweka watu salama,” anasema Guterres.Ametolea mfano janga la tsunami kwenye bahari ya Hindi mwaka 2004, janga ambalo lilisababisha dunia kuamua kuwekeza katika mifumo ya kutoa maonyo mapema.“Miongo kadhaa baadaye, uamuzi huo umelipa,” amesema Katibu Mkuu akitolea mfano tetemeko kubwa la ardhi lililokumba pwani ya Urusi mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu akisema, “lilisababisha tahadhari kwa mamilioni ya watu kuanzia pwani za Japani hadi visiwa vilivyoko bahari ya Pasifiki hadi California.”Ingawa hivyo amesema madhara ya janga hilo la tsunami yanaendelea kubadilika kutokana na mabadiliko kadhaa ikiwemo yale ya tabianchi.Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa akieleza kuwa kuheshimu baharí ni kutambua nguvu yake anasema, “kiwango cha maji ya bahari kikiongezeka, na idadi ya watu wanaoishi maeneo ya pwani ya bahari ikiongezeka, mifumo ya kutoa maonyo mapema nayo inahitaji uwekezaji zaidi na kuboreshwa,”Ni kwa mantiki hiyo amesema hilo ndio lengo la mpango wa Umoja wa Mataifa wa Mfumo wa Tahadhari kwa Wote ulioanzishwa kwa lengo la kuhakikisha kila mtu anafikiwa na mpango wa utoaji onyo mapema dhidi ya tsunami ifikapo mwaka 2027.Maadhimisho ya mwaka huu ni ya 10, ambapo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilianzisha siku hii kupitia azimio namba 70/203 la mwaka 2005.
Nchini Kenya, shirika la kiraia la FODDAJ au la Forum for Women Development, Democracy and Justice linatekeleza kivitendo lengo namba 3 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs la afya bora na ustawi ambalo pamoja na mambo mengine linataka manusura wa ukatili wa kijinsia wapatiwe huduma sio tu za afya bali pia za kijamii. Je linafanya nini, Sheilah Jepngetich amezungumza na mwakilishi wa shirika hilo.Ni Salome Gatakaa Araka, Mwakilishi wa FODDAJ ambaye katika mazungumzo nami anaanza kwa kuelezea walianzia wapi harakati zao. Akisema Policy and Advocacy anamaanisha Sera na Uchechemuzi.“FODAJ ilianza na uundaji wa ufahamu yaani policy and advocacy kumaanisha kwamba kuwe kutengwa kwa fedha za kutengeneza mahali pa waathiriwa kuishi, na pia kusisitiza ufahamu wa kutetea wale ambao wametengwa. Katika kata ya Kajiado, tumesukuma sera za GBV ili kuimarisha juhudi za kuzuia waathiriwa kuumia zaidi.”Pamoja na kukabili ukatili wa kijinsia, nikataka kufahamu iwapo wanawejengea wanawake uwezo wa kujitegemea.“FODDAJ imekuwa mstari wa mbele katika katika kupaza sauti za wanawake na wasichana, na pia kuhimiza akina mama kuweka akiba za vikundi, kushirikiana na kusaidiana ili kujikimu kiuchumi. Tumehimiza akina mama kuweka akiba kwa vikundi vya maendeleo, kushirirki mafunzo ya ujasiriamali na kushirikiana na wengine kwa pamoja. Na pia wanafundishwa mambo tofauti kama vile kutengeneza nywele , kusoma na kuandika na pia na kuhesabu.”Maneno ya Bi. Araka si matupu kwani Geraldine Ndayisenga mkazi wa Kitengela ambaye ni manusura wa ukatili na mnufaika wa miradi ya FODDAJ anafunguka.“Mimi ni mmoja wa wale waliopitia dhuluma. Nilijua kuhusu FODDAJ kupitia rafiki yangu. Nikasaidiwa, nilipata matibabu, nikapata ushauri (counselling) kwa mwezi mmoja. Baada ya hapo nikajiunga na mafunzo ya kutengeneza nywele, makucha na ushonaji. Mafunzo hayo yamenisaidia sana, sasa najisikia niko huru na nina furaha kuwa sehemu ya jamii tena. Fodaj Foundation imenishika mkono na kunionesha namna bora ya kuishi hapa Kitengela. Wamenisaidia kwa mambo mengi, na kwa kweli maisha yangu yamebadilika kwa njia chanya sana.”Nikarejea kwa Bi. Araka, kufahamu iwapo wana ushirikiano na serikali na mashirika ya kiraia. Akisema Post Traumatic anamaanisha kiwewe baada ya dhuluma.“Kwa kushirikiana na serikali na mashirika mengine ya kiraia, waathirika wanapatiwa msaada kwa ajili ya huduma za afya. Mfano wale waliobakwa au kupigwa, hupata matibabu kwa vipimo au dawa. Aidha, waathirika wa kimawazo wanapewa msaada wa kisaikolojia ili iwasaidie kuondokana na madhara ya post trauma ambayo wamepitia.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Tony Burke, anasema kwamba serikali inafanya kazi juu ya uwezekano wa kutambua ujuzi wa nje ya nchi. Anasema hii itasaidia kuokoa muda na pesa kwa wahamiaji wenye ujuzi wanaotafuta kuhamia Australia. Katika hotuba yake kwa Klabu ya Waandishi wa Habari huko Canberra, Bw. Burke pia ametangaza mabadiliko kwenye akaunti za benki zisizotumika ili kukabiliana na utakatishaji wa fedha.
Katika video hii fupi na ya kielimu, tunaingia ndani kabisa ya ulimwengu mdogo wa atomi na kuchunguza siri inayofanya muundo wake kuwa imara na thabiti. Tutatumia mifano rahisi, kama vile sumaku, kukusaidia kuelewa sheria za msingi za fizikia zinazotawala ulimwengu wetu.Jifunze sayansi kwa njia rahisi na ya kuvutia!
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "SUMIA."
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambayo Bi. Lucy Githinji, mkazi wa jimbo la New Jersey nchini Marekani amezungumza na idhaa hii baada ya matembezi ya hiari kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuhusu saratani ya titi, akisema hakika dawa zinafanya kazi.Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kibinadamu nchini Sudan, Denise Brown amesema ni kweli wamepokea ripoti za mauaji ya baadhi ya wahudumu wa kujitolea huko El Fasher jimboni Darfur wakati huu ambapo mji huo umetwaliwa na wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka, (RSF).Kimbunga Melissa kimepungua nguvu baada ya kutua nchini Jamaica kama kimbunga cha kiwango cha 5, na kuvunja rekodi ya kimbunga chenye nguvu zaidi, kabla ya kuelekea kaskazini mashariki kupita Cuba hadi Bahamas, na kusababisha mafuriko makubwa, uharibifu na kukatika kwa umeme katika maeneo mbalimbali ya Karibea na Amerika ya Kati.Nchini Cameroon, kufuatia mauaji ya raia wakati wa maandamano ya kupinga kutangazwa kwa Paul Biya kuwa mshindi wa kiti cha Urais kwenye uchaguzi uliofanyika Oktoba 12, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu imeeleza wasiwasi wake juu ya ripoti za vifo hivyo.Na katika Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "SUMIA."Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Leo jaridani tunamulika kimbunga Melissa huko Karibea, uhamishaji wagonjwa kutoka Gaza kwenda nchi za nje kupata huduma za kigeni na hali tete kwa watoto nchini Sudan. Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi.Katibu Mkuu wa Umoja wa MataifaAntonio Guterres ameonesha wasiwasi mkubwa wakati Kimbunga Melissa kikiwa miongoni mwa vimbunga vyenye nguvu zaidi kuwahi kurekodiwa katika Bahari ya Atlantiki kinaendelea kusababisha uharibifu mkubwa katika eneo la Karibea.Kupitia taarifa yake iliyotolewa leo mjini New York Marekani na msemaji wake Katibu Mkuu amesema kimbunga hicho kimeacha athari kubwa nchini Jamaica, Cuba na Bahamas huku mafuriko makubwa yakiripotiwa pia nchini Haiti na Jamhuri ya Dominika.Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani, WHO, limeongoza uhamishwaji wa kwanza wagonjwa kutoka Gaza tangu awamu mpya ya kusitishwa kwa mapigano. Katika muda wa siku mbili, wagonjwa 41 waliokuwa katika hali mbaya pamoja na familia zao 145 wamehamishwa kutoka eneo la mgogoro, huku maelfu zaidi wakiendelea kusubiri matibabu ya dharura. Flora Nducha na taarifa zaidi.Nchini Sudan hususani katika eneo la El Faher kusinimagharibi mwa nchi, hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya kila siku, huku ghasia, njaa, na vizuizi vya utoaji misaada vikiendelea kuathiri mamilioni ya watu wakiwemo watoto waliokwama katika maeneo ya vita. Anold Kayanda na taarifa zaidi.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, limeongoza uhamishwaji wa wagonjwa kutoka Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa awamu mpya ya kusitishwa kwa mapigano kwenye ukanda huo.Katika muda wa siku mbili, wagonjwa 41 waliokuwa katika hali mbaya pamoja na familia zao 145 wamehamishwa kutoka eneo la mgogoro, kuelekea Afrika Kusini, Uswisi na kwingineko, huku maelfu zaidi wakiendelea kusubiri matibabu ya dharura.Katika hospital iliyojengwa kwa mahema katika eneo la AL-MAWASI, RAFAH kwenye Ukanda wa Gaza wagonjwa wakihudumiwa kila kona watoto kwa wakubwa Miongoni mwao ni Ibrahim Abu Ashiba, mkurugenzi wa filamu ambaye maisha yake yamebadilika ghafla. Anakumbuka wakati alipojeruhiwa. Anasema, "Nilipigwa risasi mara kadhaa, mara moja kwenye kifua, mara moja kwenye bega, mara mbili mkononi. Risasi hizo mbili zilikata mishipa ya neva ya mkono wangu. Sasa siwezi kushika kamera wala kunyoosha mkono wangu kawaida. Ghafla, maisha yangu yote yalisimama."Safari ya kupona kwa Ibrahim inaanzia Afrika Kusini, ambapo amekubaliwa kwenda kupokea matibabu maalum ambapo anasema "Maisha yangu yote yalikuwa yamesimama baada ya kujeruhiwa hadi waliponipigia simu na kunijulishakwamba nitasafiri kwenda Afrika Kusini kwa matibabu. Ilionekana kama nimezaliwa upya."Mgonjwa mwingine katika hospitali hii ni, Maria Al-Shaer, alijeruhiwa vibaya katika mashambulizi yaliyokuwa yakiendelea Gaza, huku akipoteza ndugu zake. Mama yake, Raghda Ahmed Al Shaer, anaelezea mateso hayo. "Maria amepoteza baba yake na ndugu zake wote. Alijeruhiwa na kuvunjika mguu, mifupa na kupoteza nyama. Anahitaji upasuaji wa kuwekewa viungo bandia. Maisha yake yamegeuka, hawezi kutembea, na hali yake ya kisaikolojia imeathirika sana."Uhamishwaji huu umeratibiwa na Shirikisho la Chama cha Msalaba Mwekundu Palestina, kwa msaada wa WHO. Dkt. Luca Pigozzi, Mratibu wa Timu ya Dharura ya WHO, anafafanua umuhimu wake."Huu ni uhamishaji wa kwanza wa matibabu tangu kusitishwa kwa mapigano Oktoba 10. Tumejizatiti kuongeza uwezo wetu kusaidia na kuratibu uhamishaji kwa ajili ya matibabu, kwa ushirikiano wa karibu na Shirikisho la chama cha Msalaba Mwekundu la Palestina."Raghda anaeleza matumaini kwa ajili ya binti yake wanapohama kwenda Uswisi. "Wametupigia kutuarifu kwamba Maria amekubaliwa kusafiri kwenda Uswisi kwa matibabu. Tumefurahi sana kwamba atatembea tena, na hali yake ya kisaikolojia itaboreka. Atarudi kuwa Maria wa kawaida kama tuliyemjua."WHO inasisitiza kuwa wagonjwa takriban 15,000 bado wanangojea idhini ya kupata matibabu nje ya Gaza na inatoa wito kwa nchi zote kufungua milango yote za dharura kwa ajili ya uokoaji wa wagonjwa.
Katika kaunti ya Mombasa nchini Kenya, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na wa Mastercard Foundation na Serikali ya Kaunti ya Mombasa, imechukua hatua za kukabiliana na mlipuko wa MPOX kwa kutoa huduma muhimu za afya na WASH kwa wagonjwa na waliopona, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujikinga (PPEs), vituo vya kusafisha mikono na ujumbe wa mabadiliko ya tabia za kijamii. Sheilah Jepngetich na taarifa zaidi
Hii leo jaridani tunaangazia machafuko ya muda mrefu nchini Myanmar, hali ya kibinadamu nchini Sudan kufuatia ripoti za vifo vya raia na wimbi la wakimbizi wa ndani, na masuala ya afya nchini Kenya.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito kwa dunia na mataifa wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini-Mashariki mwa Asia, ASEAN kuchukua hatua za haraka kumaliza machafuko ya muda mrefu nchini Myanmar, akisisitiza kuwa mgogoro huo si tishio kwa watu wa Myanmar pekee bali pia kwa amani na usalama wa kanda nzima ya Asia ya Kusini Mashariki.Ofisi ya Uratibu wa Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA) imeelezea wasiwasi mkubwa kufuatia ripoti za vifo vya raia na wimbi la wakimbizi wa ndani, kufuatia kuendelea kwa mapigano makali katika mji wa El Fasher, huko Darfur Kaskazini nchini Sudan. Tupate tarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi.Katika kaunti ya Mombasa nchini Kenya, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) kwa kushirikiana na wa Mastercard Foundation na Serikali ya Kaunti ya Mombasa, imechukua hatua za kukabiliana na mlipuko wa MPOX kwa kutoa huduma muhimu za afya na WASH kwa wagonjwa na waliopona, ikiwa ni pamoja na vifaa vya kujikinga (PPEs), vituo vya kusafisha mikono na ujumbe wa mabadiliko ya tabia za kijamii.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Hii leo jaridani tunaangazia siku ya Umoja wa Mataifa ikiwa ni miaka 80 tangu kuanzishwa kwake 1945.Leo ni siku ya Umoja wa Mataifa ni miaka 80 tangu kuanzishwa kwake 1945, lakini pia ni kumbukizi ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilikuwa ni tukio la kihistoria na la kukumbukwa. Akiwahutubia wajumbe wa Baraza hilo kwa njia ya mtandao katika kikao cha kumbukizi hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa wito wa mageuzi ya dharura na mwamko mpya wa uwajibikaji, akiwakumbusha jukumu lao kuu la kulinda amani ya dunia.Tukiendelea na Siku ya Umoja wa Mataifa, ikitukumbusha kuanzishwa kwake tarehe 24 mwezi Oktoba mwaka 1945. Maudhui ya mwaka huu ni "Miaka 80 ya Umoja wa Mataifa: Kujenga Mustakabali Wetu kwa Pamoja - Ishara ya Matumaini kwa ushirikiano wa Kimataifa." Katika kumulika hili, Sabrina Saidi wa idhaa hii amezungumza na mwakilishi wa vijana pamoja na mmoja wa watumishi wa Umoja wa Mataifa kuhusu maadhimisho ya siku hii, huko jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.Msikilizaji, bila shaka umeyasikia mengi kuhusu Umoja wa Mataifa, lakini Umoja wa Mataifa ni nini hasa? Japo kwa ufupi, Anold Kayanda anakufahamisha akianza na historia.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Leo ni Siku ya Umoja wa Mataifa, ikitukumbusha kuanzishwa kwake tarehe 24 mwezi Oktoba mwaka 1945. Maudhui ya mwaka huu ni "Miaka 80 ya Umoja wa Mataifa: Kujenga Mustakabali Wetu kwa Pamoja - Ishara ya Matumaini kwa ushirikiano wa Kimataifa." Katika kumulika hili, Sabrina Saidi wa idhaa hii amezungumza na mwakilishi wa vijana pamoja na mmoja wa watumishi wa Umoja wa Mataifa kuhusu maadhimisho ya siku hii, huko jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania.
Karibu uungane nami Peter katika kipindi cha Fahamu wito wako, mwezeshaji Padre Innocent Bahati Mushi kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Jimbo Kuu Katoliki Arusha, akitufundisha juu ya Heri za utakatifu furahini na kushangilia. L'articolo Fahamu heri za Utakatifu katika maisha ya Mwanadamu proviene da Radio Maria.
Kuanzia furaha ya uhuru hadi maumivu ya kurejea kwa mzozo, safari ya amani ya kudumu Sudan Kusini imekuwa ndefu na bado inaendelea. Licha ya changamoto hizo, matumaini bado ni makubwa miongoni mwa jamii nchini kote kwamba uchaguzi wa amani, huru na wa haki utaleta usalama uliotafutwa kwa muda mrefu pamoja na fursa za maendeleo na ukuaji wa uchumi. Leah Mushi anatuletea taarifa ikiangazia namna Sudan Kusini inavyojiandaa na uchaguzi wake mkuu mwakani 2026.
Katika Jarida la Habari za Umoja wa Mataifa hii leo Leah Mushi anakuletea-Gaza Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula Duniani WFP lasema usitishaji wa mapigano umeleta afueni kwa wakaazi kwani sasa misaada inaendelea kuwafikia wenye uhitaji-Naibu Mratibu wa Misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Joyce Msuya amekuwa ziarani Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na kujionea hali halisi ya wakimbizi, wakimbizi wa ndani na msaada wa kibinadamu-Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa leo limesema katika tathimini yake kuwa ukataji wa misitu umepungua duniani kote ingawa bado kuna shinikizo na hatua zaidi zahitajika-Katika mada kwa kina tunakupeleka nchini Tanzania ambako Vyuo Vikuu vinachukua hatua ya kusongesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs hususan lile namba 17 la ubia kupitia umataifishaji. -Na kwenye jifunze Kiswahili unapata ufafanuzi wa methali " “NG'OMBE WA MNYONGE HAZAI"
Shirika la Umoja wa Mataifa ka Utabiri wa Hali ya Hewa Duniani WMO linaongeza kasi ya jitihada za kulinda maisha ya watu dhidi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Mkutano wake Maalum uliofunguliwa leo mjini Geneva Uswisi, unalenga kuharakisha mpango wa kimataifa wa Tahadhari za Mapema kwa Wote, sambamba na maadhimisho ya miaka 75 ya WMO. Flora Nducha amefuatilia na anafafanua zaidi (TAAFIFA YA FLORA NDUCHA)Asante Leah, kwa mujibu wa WMO idadi ya nchi zenye mifumo ya tahadhari za mapema kwa ajili ya majanga ya tabianchi imeongezeka maradufu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita lakini bado mamilioni ya watu hawana ulinzi dhidi yah atua hiyo muhimu.Ndiyo maana shirika hilo limewakutanisha mawaziri na wataalamu kutoka nchi wanachama 193 kuharakisha mpango wa Tahadhari za Mapema kwa Wote, uliozinduliwa mwaka 2022 na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres unatekelezwa kwa vitendo.Katika mkutano huo Celeste Saulo Katibu Mkuu wa WMO amesema “Miaka 75 iliyopita, Shirika la WMO lilianzishwa kutokana na ukweli kwamba hali ya hewa, maji na tabianchi havina mipaka ya kitaifa. Ushirikiano wa kimataifa katika uchunguzi na utabiri ni wa lazima, kwa sababu hakuna nchi inayoweza kufanya hivyo peke yake.”Ripoti mpya ya WMO, iliyopewa jina Tahadhari za Mapema kwa Wote Mtazamo wa Dunia, inaonesha kuwa licha ya maendeleo makubwa katika ubadilishanaji wa takwimu na utabiri wa kidijitali, bado kuna mapengo makubwa, hasa katika nchi maskini na visiwa vidogo vinavyoendelea.Celeste amesisitiza kuwa“Tahadhari za Mapema kwa Wote sasa siyo mpango tena, bali ni nembo ya mshikamano wa dunia. Pamoja, tunaokoa maisha, tunaunda sera, na kuimarisha mnepo.”Takwimu za shirika hilo zinaonesha uzito wa changamoto. Katika miaka 50 iliyopita, WMO inasema majanga yanayohusiana na hali ya hewa na maji yamesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni mbili huku asilimia 90 kati yao ni katika nchi zinazoendelea.Na ingawa mataifa 108 sasa yana mifumo ya tahadhari za majanga mchanganyiko, shirika hilo linasema viwango vya vifo bado ni mara sita zaidi katika maeneo yasiyo na mifumo hiyo.WMO inasema teknolojia mpya ikiwemo akili mnemba na matumizi ya takwimu za setilaiti kwa wakati halisi zinabadilisha uwezo wa utabiri, lakini pengo la kidijitali bado linawaacha wengi wakiwa hatarini.“Mafanikio ya Tahadhari za Mapema kwa Wote hayapimwi kwa ripoti au maazimio, anasema Celesto bali kwa maisha yanayookolewa na riziki zinazolindwa. Tunapoelekea mwaka 2027, hebu tuongeze juhudi kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa bila ulinzi.”Mkutano huo Maalum wa WMO utaendelea wiki nzima mjini Geneva, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akitarajiwa kuhutubia siku ya Jumatano.Shirika la WMO wakati likiadhimisha miaka 75 ya kile linachoita Sayansi kwa Vitendo linataka kuhakikisha sayansi hiyo inawafikia wote, kabla ya majanga kutokea.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayoangazia siku ya chakula duniani ikienda sambamba na maadhimisho ya miaka 80 ya kuanzishwa shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, na utamsikia Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania Bi. Nyabenyi Tito Tipo akieleza.Maadhimisho ya siku ya chakula duniani yamefanyika kimataifa leo huko Roma nchini Italia, yakienda sambamba na sikukuu ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na kilimo, FAO. Katika ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema, “Miaka themanini iliyopita, katika dunia iliyosambaratishwa kwa vita, nchi zilikutana kukabiliana na njaa. Miongo kadhaa tangu wakati huo, dunia imepiga hatua kubwa. Lakini bado majanga yanyoonesha kuwa hatuwezi kubweteka iwapo tunataka kuendeleza mafanikio tuliyopata. Tuna mbinu, ufahamu, rasilimali za kutokomeza njaa, na kupatia kila mtu chakula kizuri na chenye afya. Tunachohitaji ni umoja.Huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, raia wamerejea kufuatia makubaliano ya sitisho la mapigano lakini wanahaha kujenga upya makazi yao huku wakiwa wamezingirwa na vifusi. Miongoni mwao Ayman Awadallah, amesema “hakuna maji, hakuna miundombinu ya majitaka, hakuna maisha hapa, hakuna chochote.”Na kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, kilichotokea Jumatano Oktoba 15 nchini India, Umoja wa Mataifa kupitia Katibu Mkuu umetuma salamu za rambirambi na kusema hayati Odinga, alikuwa mtu muhimu katika maendeleo ya kidemokrasia nchini Kenya na pia mtetezi thabiti wa mageuzi ya kikatiba na utawala jumuishi.Na katika kujifunza Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana za neno "KIMWA"Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Katika kujifunza Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana za neno "KIMWA."
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili na hii leo Dkt. Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana ya neno "MKWECHE"!
Hii leo jaridani tunaangazia mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya amani ya Nobel, sauti za wanawake nchini Kenya ambazo zimeanza kusikika kwa uthabiti, zikililia haki, heshima, na usawa, na Puja Durga ambayo ni sherehe kubwa ya kihindu ya ushindi wa mungu wa kike.Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) imekaribisha uamuzi wa Kamati ya Tuzo ya Amani ya Nobel kumtangaza Maria Corina Machado kiongozi wa upinzani nchini Venezuela kuwa mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya amani ya Nobel, kwa kutambua kazi yake ya kuendeleza matumaini ya demokrasia ya watu wa Venezuela.Katika kila kona ya Kenya, sasa sauti za wanawake zimeanza kusikika kwa uthabiti, zikililia haki, heshima, na usawa. Kupitia msaada wa mashirika ya kimataifa kama shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo, UNDP na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na dawa za Kulevya na Uhalifu(UNODC), mabadiliko yanaanza kushika kasi.Mnamo mwaka wa 2021, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliongeza kwenye orodha ya turathi za dunia za tamaduni zisizoshikika au kugusika, Puja Durga ambayo ni sherehe kubwa ya kihindu ya ushindi wa mungu wa kike aitwaye Durga dhidi ya jini Mahishasura, ikiwa ni ishara ya ushindi wa mema dhidi ya maovu"Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Katika kila kona ya Kenya, sasa sauti za wanawake zimeanza kusikika kwa uthabiti, zikililia haki, heshima, na usawa. Kupitia msaada wa mashirika ya kimataifa kama shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo, UNDP na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na dawa za Kulevya na Uhalifu(UNODC), mabadiliko yanaanza kushika kasi. Katika jamii ambazo kwa muda mrefu mifumo ya jadi na taasisi za kisheria zimewabagua au kuwapuuza wanawake Taarifa ya SHEILAH Jepngetich inafafanua zaidi
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali "FUNDI HANA CHOMBO"
Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuna maonesho ya picha 32 zinazoonesha harakati za wanawake kwenye maeneo yenye mizozo kusongesha amani na usalama, kwa mujibu wa azimio namba 1325 lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa miaka 25 iliyopita. Maonesho ya picha hizi zilizopigwa na wanawake yamepatiwa jina Kupitia Lensi Yake na yameandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wadau ili kudhihirisha ujasiri wa wanawake katikati ya mazingira hatarishi, wakihaha kuleta amani kwenye maeneo yao. Assumpta Massoi ametembelea onesho hilo.
Hii leo jaridani tunaangazia tunzo ya Umoja wa Mataifa ya “Muonesha njia” au kwa kiingereza Trailblazer, juhudi za wapiga picha wanawake kwenye maeneo yenye mizozo katika kusongesha amani na usalama, na wafugaji Samburu nchini Kenya.Mwaka huu, Tuzo ya Umoja wa Mataifa ya “Muonesha njia” au kwa kiingereza Trailblazer imekwenda kwa Olukemi Ibikunle, afisa wa magereza kutoka Nigeria anayehudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo MONUSCO. Tunzo hii inatambua mchango wake mkubwa katika kazi za haki na magereza kwenye operesheni za kulinda amani, pamoja na ujasiri wake wa kuvunja vizingiti vya kijinsia katika maeneo yanayoongozwa na wanaume.Katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuna maonesho ya picha 32 zinazoonesha harakati za wanawake kwenye maeneo yenye mizozo kusongesha amani na usalama, kwa mujibu wa azimio namba 1325 lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa miaka 25 iliyopita. Maonesho ya picha hizi zilizopigwa na wanawake yamepatiwa jina Kupitia Lensi Yake na yameandaliwa na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na wadau ili kudhihirisha ujasiri wa wanawake katikati ya mazingira hatarishi, wakihaha kuleta amani kwenye maeneo yao.Mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Kenya wanatekeleza mradi unaowashirikisha wananchi wa Kauti ya Samburu katika kuhakika kuna upatikanaji wa chakula kwani eneo hilo linahali ya ukame ikiwa ni hatua mojawapo ya kutafsiri na kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs huko mashinani. Tuungane na Sheilah Jepngetich anayetuletea tarifa hii iliyoandaliwa na UNICEF Kenya.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo, Mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "TITIMA."
Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Mpango wa Maendeleo, (UNDP) na la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) kwa ushirikiano na viongozi wa sheria nchini Kenya hadi mashinani wamezindua mpando wa PLEAD unaolenga kuboresha mfumo wa haki katika kaunti 12 nchini humo. Lengo lao ni kuimarisha haki jumuishi kwa kutoa majawabu mbadala badala ya kifungo, kupunguza msongamano wa magereza kwa asilimia 30, na kuondoa mkwamo wa maisha. Sheilah Jepngetich anaeleza zaidi kupitia video iliyochapishwa kwenye chaneli ya Youtube ya UNDP
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili leo ukumbi ni wake mlumbi wa Kiswahili Joramu Nkumbi kutoka nchini Tanzania, anafafanua maana za maneno "USHINZI NA USHENZI"
Tuanzie hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambako kumefanyika tukio maalum la kuadhimisha siku ya wazee duniani leo Oktoba Mosi, kaulimbiu ikiwa Wazee Wanaendesha Hatua za Kijamii na Kimaisha: Matamanio Yetu, Ustawi Wetu na Haki Zetu. Anayekupeleka ukumbini ni Flora Nducha.
Kama unavyofahamu Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80 umekunja jamvi rasmi jana Jumatatu. Na tumepata fursa ya kuzungumza na washiriki mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, Veronica Nduva ambaye alizungumza na Flora Nducha kandoni mwa mjadala huo kuangazia mchango wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutekeleza ajenda ya Umoja wa Mataifa ikiwemo masuala ya Amani na usalama, maendeleo na ushirikiano wa kikanda. Ungana nao.
Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukiwa umeingia katika siku yake ya nne hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani leo Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amekuwa wa kwanza kuzungumza akitumia muda wake mwingi kushambulia wanamgambowa kipalestina, Hamas na kutetea kila uamuzi wa Israel. Anold Kayanda ameifuatilia hotuba hiyo kwa kina. Ilikuwa majira ya saa tatu na dakika chache hivi asubuhi ya leo saa za New York nchini Marekani ambapo Waziri Mkuu wa Isreal Benjamin Netanyahu amepewa fursa ya kuhutubia na ndipo ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukakosa utulivu. Wajumbe kwa makundi walinyanyuka katika viti vyao na kuondoka huku wakiwaacha maafisa wa Israel wakimpigia makofi kiongozi wao na pia nchi zinazoiunga mkono Israel zikasalia katika viti vyao ikiwemo Marekani.Baadhi ya wajumbe watoka njeKatika eneo la walipotakiwa kukaa wawakilishi wa Palestina kulikuwa wazi, huku katika eneo la Iran ikibakia picha iliyokusanya sura za baadhi ya watu wao waliouawa na mashambulizi ya Israel. Bwana Netanyahu kwa mara nyingine tena ameingia na ubao wenye picha ya ramani ya eneo la Mashariki ya Kati akiutumia kuishambulia Iran na kwa kutumia kalamu akiweka alama ya vema kuonesha namna ambavyo Israel imefanikiwa kupambana na ngome za Irani katika ukanda huo. Katika suti yake, kifuani upande wa kulia, Bwana Netanyahu pia ameweka kibandiko chenye QR Code na akawaambia watu kuwa Israel bado inakumbuka tukio walilofanyiwa na Hamas mwezi Oktoba mwaka juzi na kwamba ikiwa watu wamesahau hilo basi waelekeze simu zao kwenye QR Code hiyo kwenye nguo yake ili iwaoneshe madhara yaliyofanywa na Hamas.Majina ya mateka yakasomwaWaziri Mkuu huyo wa Israel ameyasoma majina ya mateka ambao bado wako mikononi mwa Hamas katika eneo la Ukanda wa Gaza na pia akaueleza mkutano kuwa amesambaza vipaza sauti au spika katika eneo lote la Gaza ili anapoongea leo, azungumze moja kwa moja na mateka huko walikofichwa. Na hapo akabadilisha lugha na kuongea kwa kihebrania akiwaahidi kuwa atawakomboa. Vilevile amedokeza kuwa kwa namna ya kiintelijensia Israel imefanya simu leo ziweze kusambaza hotuba katika ukanda wa Gaza na hivyo akautumia muda huo kupeleka ujumbe mkali kwa Hamas kuwa ataendelea kuwadhibiti. Bwana Netanyahu pia ameingia ukumbini na vibao viwili vyenye maswali na majibu ya kuchagua japokuwa jibu sahihi kwa mujibu wake na waliojibu kuwa ni All the Above, yaani majibu yote ni sahihi. Maswali yote yalikuwa yakiwatuhumu Iran, Hamas, Al Caeda, Hezbollah na Houthi kuwa pia wanaitakia kifo Marekani na wameua watu wengi Ulaya. Huenda hotuba hii ya Netanyahu ikaingia katika orodha ya hotuba tano ndefu zaidi baada ya ile ya Rais wa Marekani Donald Trump wa Marekani, Ya Mahmoud Abbass wa Palestina na Félix-Antoine Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambao wote hao walitumia zaidi ya dakika arobaini licha ya muda wa hotuba uliopangwa kuwa angalau dakika 15.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina maalum inayomulika mkutano wa ngazi ya juu kuhusu magonjwa yasiyo ya kuambukiza NDCs unaoendelea kandoni mwa UNGA80, na tumezungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO Kanda ya Afrika Dkt. Mohamed Yakub Janabi.Wakati viongozi wa nchi na serikali wanahutubia wakiwa ndani ya jengo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jijini New York, Kiongozi wa Palestina, Mahmoud Abbas ujumbe wake kwa UNGA80 ameutoa kwa njia ya video iliyorekodiwa kutokana na kutopata kibali cha kuingia Marekani. Katika hotuba hiyo amesisitiza kuwa, Ukanda wa Gaza utaendelea kuwa sehemu ya Taifa la Palestina na tuko tayari kuwajibika kikamilifu kwenye uongozi na usalama wa eneo hilo. Hamas hawatokuwa na jukumu lolote kwennye utawala.”.Mapema kabla ya Palestina, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud, alihutubia wajumbe akitaka nchi wanachama kujitolea upya kwa misingi ya usawa, mshikamano na ushirikiano wa kimataifa. Amesema hilo ni muhimu kwa kuwa “wakati ambapo hapo awali tulijitahidi kujiuliza ‘Nini ni sahihi' chini ya sheria ya kimataifa, leo tunashuhudia kwa wazi kuibuka kwa matumizi ya NGUVU ya kitaifa katika kusuluhisha migogoro. Hii ni njia ya giza na ya hatari sana inayotishia utawala wa sheria wa kimataifa tuliokubaliana kwa pamoja kama nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa.”Kando ya hotuba za viongozi, kunafanyika maadhimisho ya miaka 30 tangu kupitishwa kwa Programu ya Dunia kwa ajili ya vijana. Je vijana kutoka Malawi wana ujumbe gani? Mwakilishi wao kwenye mkutano huu Rachel Mganga Wanangwa anasema, “Ujumbe kutoka vijana wa Malawi ni wekezeni kwetu, tusaidieni, shirikianeni nasi, na wanashiriki kwenye meza za mazungumzo ili kuhakikisha kuwa sauti zao zinawakilishiwa.”.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Hii leo jaridani tunaangazia hotuba ya Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy katika siku ya pili ya mjadala mkuu wa UNG80, na ujumbe wa washiriki wa mkutano huu kutoka Nigeria na Tanzania.Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema taasisi za kimataifa zimekuwa dhaifu wanachoweza kufanya ni kutoa matamko makali pekee na kwamba kwa sasa duniani sheria pekee za Kimataifa haziwezi kusaidia nchi kujilinda bila ya kuwa na silaha pamoja na marafiki wenye nguvu wa kukusaidia.Katika siku ya pili ya Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA, kando ya hotuba, viongozi wa nchi 9 wanachama wa Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, ECSA watakuwa na mkutano wa kusongesha diplomasia ya kisayansi ili kuhakikisha bara la Afrika haliachwi nyuma kwenye kukabiliana na changamoto za kiafya, baada ya kujifunza kutokana na COVID-19 au UVIKO19.Tukisalia hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa Mjadala Mkuu wa UNGA80 mbali ya kusikiza hotuba za viongozi unaambatana na mamia ya matukio na mikutano ya kando. Leo, sauti kutoka pande zote za dunia zinaitaka haki ya kijamii katika moja ya mikutano ya kando na miongoni mwa sauti hizo ni ya mwanaharakati na mhamasishaji wa masuaa ya wasichana kutoka Nigeria ambaye anasema wasichana vigori hawapaswi kusahaulika.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Katika siku ya pili ya Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA, kando ya hotuba, viongozi wa nchi 9 wanachama wa Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, ECSA watakuwa na mkutano wa kusongesha diplomasia ya kisayansi ili kuhakikisha bara la Afrika haliachwi nyuma kwenye kukabiliana na changamoto za kiafya, baada ya kujifunza kutokana na COVID-19 au UVIKO19. Mkurugenzi Mkuu wa ECSA Dkt. Ntuli Kapologwe akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa hii ametaja wanachotarajia kwenye mkutano huo..
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina maalum na mada yetu inamulika maoni kuhusu miaka 80 ya Umoja wa Mataifa. Pia tunakuetea muhtasari wa habari unaofuatilia ujumbe wa viongozi katika mjadala mkuu wa UNG80.viongozi wa dunia wamekutana leo hapa kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ikiwa ni siku ya kwanza ya Mjadala Mkuu wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ukiambatana na vikao vya kando vya ngazi ya juu. Katika hotuba yake ya UNGA 80 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito kwa dunia kufanya maamuzi “ni aina gani ya dunia tunataka kujenga pamoja.”Kuanza kwa UNGA maana yake idadi kubwa ya wageni, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa UN anayeshughulikia habari na teknolojia, Bernardo Mariano, amesema wamejipanga kutoa huduma ya internet (Wi Fi) kwa watu 40,000 huku wakihakikisha hotuba za viongozi zinapeperushwa bila hitilafu za kiufundi wala kuvurugwa na mashambulizi ya mtandaoni.Na Hapo kesho Jumatano viongozi wa jumuiya ya Afya ya nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini, ESCA watakutana kumulika Diplomasia ya kisayansi na afya ili kusongesha Mkataba wa Zama Zijazo. Mkurugenzi Mkuu wa ECSA Dkt. Ntuli Kapologwe ameeleza kulikoni?.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Umoja wa Mataifa hii leo umeadhimisha miaka 80 tangu kusainiwa kwa Mkataba wake tarehe 26 Juni 1945, tukio lililotoa matumaini mapya kwa dunia iliyokuwa imechoka kutokana na vita kuu mbili za dunia, mauaji ya halaiki na ukoloni. Katika maadhimisho hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kumbukizi ya kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa ni fursa ya kukumbuka ujasiri wa waanzilishi wa taasisi hiyo na kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kukabili changamoto zinazokabili dunia hivi sasa. Tuungane na Leah Mushi aliyefuatilia maadhimisho hayo atupatie taarifa zaidi.
Kando ya maadhimisho ya siku ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, hapa makao makuu kumefanyika mashauriano ya faragha yenye lengo la kusaka majawabu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Mashauriano ya leo ni sehemu ya mashauriano 10 yatakayofanyika kuelekea mkutano wa tabianchi wa wakuu wa nchi na serikali utakaofanyika keshokutwa Jumatano hapa Umoja wa Mataifa. Assumpta Massoi amezungumza na mmoja wa watoa mada kwenye mashauriano hayo ambayo matokeo yake yatawasilishwa kwenye mkutano wa viongozi. Kwako Assumpta.(Taarifa ya Assumpta Massoi)Nats..Katika uwanda wa wageni nje ya jengo la mikutano nakutana na Emily Mohohlo, Mratibu wa shirika la kiraia la Slum Dwellers International kutoka Afrika Kusini linalojikita katika kuhakikisha maeneo ya mabanda mijini yanakuwa jumuishi, yana mnepo na maisha yao yanaboreshwa.Nikamuuliza umuhimu wa mkutano na kusema..(Sauti ya Emily Mohohlo)“Mkutano huu ni muhimu kwangu kwa sababu katika maisha halisia kuna joto kupindukia na linasababisha vifo kwa wanawake na pia kutoweka kwa mbinu zao za kujipatia kipato. Hivyo kwangu naona kama tunaweza kujumuika pamoja katika ngazi ya kijamii na kupata takwimu sahihi na kisha watafiti watusaidie. Tunahitaji wabia kwani tayari tumeshachukua hatua.”Kwa hiyo ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano?(Sauti ya Emily Mohohlo)“Njooni mshirikiane nasi, kwa sababu tuna takwimu kutoka mashinani lakini hatuna uwezo wa kifedha. Tukipata fedha kutoka kwa watafiti itakuwa vema. Tunajua wana takwimu lakini si kutoka mashinani.”Nilipomuuliza umuhimu wa Umoja wa Mataifa wakati huu unatimiza miaka 80 akafunguka..(Sauti ya Emily Mohohlo)“Ndio sasa una miaka 80, lakini bado hatuoni vya kutosha mafanikio yake mashinani. Huwezi kusaidia mtu mmoja mmoja. Waje kwenye vikundi na itakuwa vema kwa sababu kuna idadi kubwa ya watu.”Akatamatisha na ujumbe kwa Umoja wa Mataifa.(Sauti ya Emily Mohohlo)“Tumefika hapa, tafadhali tusikilizeni. Hakuna chetu bila kutushirikisha. Asante,”TAGS: Tabianchi/Afrika/Slum Dweller International/UNGA80
Hii leo jaridani tunaangazia ujumbe wa washirirki ya mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hasa maadhimisho ya miaka 80 ya umoja huo. Pia tunamulika mashauriano ya faragha yenye lengo la kusaka majawabu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi.Umoja wa Mataifa hii leo umeadhimisha miaka 80 tangu kusainiwa kwa Mkataba wake tarehe 26 Juni 1945, tukio lililotoa matumaini mapya kwa dunia iliyokuwa imechoka kutokana na vita viwili vya dunia, mauaji ya halaiki na ukoloni. Katika maadhimisho hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kumbukizi ya kuanzishwa kwa UN ni fursa ya kukumbuka ujasiri wa waanzilishi wa taasisi hiyo na kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kukabili changamoto zinazokabili dunia hivi sasa.Tukisalia na maadhimisho ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa , moja ya mchango mkubwa unaotoa kwa dunia tangu ulipoanzishwa mwaka 1945 ni kusaidia mamilioni ya watu wanaolazimika kufungasha virago kukimbia makwao na kuwa wakimbizi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita. Uganda ni moja ya nchi zinazohifadhi maelfu ya wakimbizi wengi kutoka Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wakisaidiwa chini ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na mengine. John Kibego kutoka Radio washirika Kazi-Njema FM iliyoko mjini Hoima Uganda amepata fursa ya kuzungumza na mmoja wa wakimbizi hao akielezea mchango mkubwa wa Umoja wa Mataifa kwake.Kando ya maadhimisho ya siku ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, hapa makao makuu kumefanyika mashauriano ya faragha yenye lengo la kusaka majawabu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Mashauriano ya leo ni sehemu ya mashauriano 10 yatakayofanyika kuelekea mkutano wa tabianchi wa wakuu wa nchi na serikali utakaofanyika keshokutwa Jumatano hapa Umoja wa Mataifa. Assumpta Massoi amezungumza na mmoja wa watoa mada kwenye mashauriano hayo ambayo matokeo yake yatawasilishwa kwenye mkutano wa viongozi.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Amani, hapo Jumapili tarehe 21 mwezi Septemba 2025, Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kushirikiana na baadhi ya wadau nchini humo, umeendesha warsha ya siku moja ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Hazina jijini Dar es Salaam kuhusu ya umuhimu wa kuishi kwa amani na kuchukua hatua sasa katika kuidumisha. Warsha hiyo imeongozwa na kauli mbiu “Chukua hatua Sasa, kwa ajili ya Dunia yenye Amani.” Katika warsha hiyo, baadhi ya wanafunzi wameeleza walichojifunza na namna elimu hiyo inavyoweza kuwanufaisha katika maisha yao ya kila siku. Shuhuda wetu katika mafunzo ni Sabrina Saidi anatupasha ilivyokuwa
Je, unajua jinsi ya kujigamba kuhusu gari lako?
Maelfu ya watu wanasherehekea kuwa raia wapya wa Australia, katika sherehe zilizo andaliwa na halamshauri za jiji kote nchini kwa siku ya Uraia wa Australia.
Jaridani leo jaridani tunakuletea mada kwa kina kuhusu masuala ya wanawake, tathmini ya miaka 30 ya harakati za kusongesha haki za wanawake na utamsikia maoni ya Balozi Gertrude Mongella kutoka Tanzania. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na uchambuzi wa methali.Mjadala Mkuu wa mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukianza Jumatatu ijayo, Rais wa Mkutano huo Annalena Baerbock amewaambia waandishi wa habari jijini New York, Marekani kuwa “jukumu letu ni Umoja wa Mataifa uwe thabiti kwa miaka 80 ijayo. Michakato ya kuhakikisha hilo ndio itakuwa jukumu letu mwaka huu, ikiwemo kusongesha ajenda ya marekebisho ya Umoja wa Mataifa. Kwa hiyo tukitaka Umoja wa Mataifa thabiti, basi tunahitaji ahadi kutoka serikali zote duniani.Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inayotolewa kila mwaka kabla ya kuanza kwa Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu inasema Umoja wa Mataifa umeendelea kusimama imara, ukifanya kazi ya kuendeleza amani, kuchochea maendeleo endelevu, na kupunguza mateso ya kibinadamu licha ya majaribu makubwa. Katika ripoti hiyo Antonio Guterres amesisitiza uimara wa watumishi wa Umoja wa Mataifa, ambao wamejitolea kuleta matumaini na msaada kwa wale wanaohitaji licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu.ripoti ya Hali ya Rasilimali za Maji Duniani iliyotolewa leo inasema ni takriban theluthi moja tu ya mabonde ya mito duniani yaliyokuwa na hali ya “kawaida” mwaka 2024 ilhali mengine yote yalikuwa na kiwango cha juu zaidi cha maji au chini ya kiwango cha kawaida — ikiwa ni mwaka wa sita mfululizo wa kutokuwepo kwa uwiano wa wazi. Ikitolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa, WMO, ripoti inasema mwaka 2024 uliokuwa mwaka wa joto zaidi kuwahi kurekodiwa ulianza na tukio la El Niño ambalo liliathiri vibaya mabonde makubwa ya mito na kusababisha ukame katika maeneo kadhaa ikiwemo kusini mwa Afrika.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali "MZOEA PUNDA HAPENDI FARASI"Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali "MZOEA PUNDA HAPENDI FARASI"
Wakati Israeli ikiwa imetoa amri mpya ya watu kuhama kutoka jiji la Gaza katika eneo inalokalia kimabavu la Palestina, na kuelekea eneo ililotenga na kuliita ukanda wa kibinadamu kusini mwa Ukanda wa Gaza, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO limesikitishwa na agizo hilo jipya ikisema eneo halina ukubwa wala huduma za kutosha kusaidia wale walioko tayari huko, sembuse wale watakaowasili. Huduma za afya ni tete kama anavyosimulia Flora Nducha kwa taarifa hii.
Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA, anafafanua maana za neno "MJOLI"
Leo ni siku ya kimataifa ya ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea zikijulikana pia kama nchi za kusini ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa tamko lenye msukumo mkubwa likitambua ustahimilivu, ubunifu, na ushawishi unaoongezeka wa nchi zinazoendelea katika kuleta maendeleo ya kimataifa. Assumpta Massoi anatoa maelezo zaidi.(Taarifa ya Assumpta Massoi)Kwanza kabisa ni vema kufahamu kuwa nchi hizi zinaitwa za kusini, kwa maana kwamba bado ziko nyuma kimaendeleo zikilinganishwa na zile za kaskazini, (ingawa si kijiografia) ambazo zinaonekana kuwa zina maendeleo kiuchumi.Maudhui ya siku hii ni – fursa mpya na ubunifu kupitia ushirikiano wa kusini-kusini na ushirikiano wa pembetatu, ikimaanisha ushirikiano kati ya nchi zinazoendelea, na vile vile mashirika ya kimataifa na nchi zilizoendelea.Sasa katika siku hii ya leo iliyopitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 22 mwezi Desemba mwaka 2003 kwa lengo la kusongesha ushirikiano wa kiufundi baina ya nchi zinazoendelea Guterres anasema “katika dunia inayozidi kuwa na nguvu nyingi za ushawishi, nchi zinazoendelea zinaonesha ustahimilivu wa kipekee na ubunifu wa hali ya juu. Sio tu katika kukabiliana na migogoro, bali pia katika kusukuma mbele mageuzi.”Mathalani nchi hizo zinabuni na kubadilishana majawabu bunifu katika maeneo muhimu kama vile kilimo kinachozingatia mabadiliko ya tabianchi, teknolojia rafiki kwa mazingira, fedha za kidijitali, na ubunifu katika sekta ya afya.Amesisitiza kuwa mafanikio haya yanajengwa juu ya misingi ya kuheshimu pande zote, kujifunza kwa pamoja, na lengo la pamoja—ambayo ndiyo misingi ya ushirikiano wa Kusini-Kusini na ule wa pembetatu.Hata hivyo amesisitiza kuwa ushirikiano huu si ishara tu ya mshikamano, bali pia ni nguvu kuu ya maendeleo inayohitajika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).Amepongeza juhudi za nchi za Kusini katika kuendeleza Ajenda ya 2030, licha ya changamoto zinazoendelea kama vile ukosefu wa usawa wa kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi.Vilevile, ametoa wito kwa nchi zilizoendelea kutambua na kutekeleza wajibu wao katika kusaidia juhudi za maendeleo duniani.Katibu Mkuu anasema kuwa “tunatambua pia wajibu wa nchi zilizoendelea katika kushughulikia ukosefu wa usawa unaozidi kuongezeka na kuendeleza maendeleo endelevu.”Katika hitimisho la ujumbe wake, Guterres amehimiza jumuiya ya kimataifa kukumbatia ushirikiano wa nchi za kusini kama kichocheo cha kuhuisha ushirikiano wa kimataifa, akisisitiza haja ya kuchukua hatua kwa pamoja kujenga dunia iliyo jumuishi, yenye usawa, na endelevu kwa wote.Akizungumzia siku hii, , Mkurugenzi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya ushirikiano wa nchi za kusini, UNOSSC, Dima Khatib, amesisitiza kuwa nchi za Kusini zinamiliki "uwezo mkubwa wa kuendeleza maendeleo," kwani ndiko makazi ya asilimia 80 ya watu wote duniani na ni chanzo cha ustahimilivu, ubunifu, pamoja na rasilimali watu na asili ambazo hazijatumika kikamilifu.Katika mahojiano mahsusi na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, Bi. Khatib amesema kwamba katikati ya hali ya kisiasa ya kimataifa iliyojaa mvutano ambayo dunia inashuhudia leo, ushirikiano kati ya nchi za kusini unaweza kuwa injini ya kufufua na kuimarisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa.Amepigia chepuo ushirikiano kati ya nchi za kusini na zile za kaskazini akisema, “hakuwezi kuweko na mgawanyiok wa nchi kati ya zile za kaskazini zilizoendelea na zile za kusini zinazohaha kuendelea. Badala yake “lazima tujenge madaraja. Umoja wa Mataifa una uwezo wa kubeba jukumu hili kwa kuwa ni mfumo muhimu ambao unahudumia nchi zote kwa usawa.
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu ameonesha wasiwasi mkubwa kufuatia ghasia zinazoendelea na kushika kasi nchini Nepal, huko barani Asia, ambako maandamano dhidi ya ufisadi na marufuku ya mitandao ya kijamii yamesababisha vifo vya watu wengi pamoja na majeruhi. Flora Nducha amefuatilia taarifa hiyo na anatupasha zaidi.Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, akizungumza mjini Geneva amesema“nimeshtushwa na ongezeko la ghasia nchini Nepal ambalo limesababisha vifo kadhaa na kujeruhi mamia ya waandamanaji wengi wao wakiwa vijana, pamoja na uharibifu mkubwa wa mali.”Katika siku za karibuni, maandamano yaliyoanzia katika mji mkuu Kathmandu sasa yamesambaa katika miji na vijiji vya Nepal, yakiacha barabara zikifunikwa na mabaki ya vitu vilivyoteketezwa kwa moto na kulazimisha maduka kufungwa pia kuhofia usalama.Kwa mujibu wa duru za habari maandamano hayo yanayoo nngozwa na vijana wa kati ya umri wa miaka 13 hadi 28 au Gen Z yameshakatili Maisha ya takribani watu 22, kusababisha waziri mkuu wa nchi hiyo KP Sharma Oli kujiuzulu na kuliwasha moto jengo la bunge .Türk ametoa wito kwa vikosi vya usalama kujiepusha na mapambano na waandamanajI akisema, “Naomba vikosi vya usalama waoneshe uvumilivu wa hali ya juu, na kuepusha umwagaji damu na madhara zaidi. Vurugu siyo suluhisho. Mazungumzo ndiyo njia bora na ya pekee ya kushughulikia malalamiko ya watu wa Nepal. Ni muhimu sauti za vijana zisikike.”Waandamanaji wanasema wameshikwa na hasira kutokana na ufisadi na marufuku ya serikali juu ya majukwaa ya mitandao ya kijamii, ingawa kwa sasa huduma za mitandao ya kijamii zimerejea. Türk anasema anatambua haki yao ya kusikika, lakini pia amewasihi wawe na uwajibikaji.“Nawakumbusha waandamanaji kuwa nao pia lazima washikamane na kuzingatia dhamira ya kukusanyika kwa amani na wajiepushe na ghasia.”Türk ametaka uchunguzi wa haraka, wa wazi na huru ufanyike kuhusu madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi ya vikosi vya usalama, huku pia akilaani mashambulizi dhidi ya majengo ya umma, biashara, na hata maafisa waandamizi wa serikali.Amesisitiza kuwa dunia inathamini safari ya Nepal kutoka kwenye migogoro hadi kuwa na demokrasia yenye amani na ametoa mwito kwa wadau wote kulinda mafanikio hayo. Amesema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia kupitia mazungumzo na hatua za kujenga imani ambazo zinaweza kusaidia kupunguza mvutano na kurejesha hali ya utulivu.
Huko Bunia, jimboni Ituri Mashariki Mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, Jean-Pierre Lacroix, amepongeza juhudi za pamoja za walinda amani wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MONUSCO na jeshi la serikali ya Congo, FARDC, katika juhudi za kulinda raia na kupunguza ghasia za makundi yenye silaha.Akizungumza wakati wa ziara yake iliyoanza Septemba 6, Mashariki mwa DRC katika jimbo la Ituri Lacroix amesema ushirikiano na kuaminiana kati ya mamlaka za jimbo la Ituri na vikosi vya Umoja wa Mataifa ni msingi muhimu wa kurejesha amani.Anasema “Nipo katika eneo liitwalo Fataki, katika jimbo la Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, na hapa kuna kambi ya MONUSCO yenye kikosi cha Nepal, pamoja na kambi ya wakimbizi wa ndani. Maelfu ya watu wanalindwa hapa na wenzetu wa MONUSCO, na wanapatiwa msaada wa kibinadamu pamoja na ulinzi.”Gavana wa Ituri, Jenerali Johnny Luboya, alikaribisha msaada wa MONUSCO katika operesheni za kijeshi na mazungumzo ya amani, yakiwemo dhidi ya kundi la CRP katika eneo la Djugu Ituri ambako mamia ya maelfu ya wakimbizi wa ndani sasa wananufaika na ulinzi wa pamoja wa FARDC na walinda amani wa Umoja wa Mataifa. Lacroix amesema “Katika jimbo la Ituri pekee kuna makambi kadhaa ya wakimbizi wa ndani, ambayo yanalindwa na MONUSCO, ambapo makumi ya maelfu kwa hakika mamia ya maelfu ya watu wanalindwa na wenzetu wa MONUSCO na wanapatiwa msaada.”Mkuu huyo wa operesheni za ulinzi wa amani ameohitimisha kwa kusema ziara hii ni muhimu sana kwani “Nipo hapa kuonyesha kile ambacho MONUSCO hufanya kila siku, tofauti ambayo MONUSCO inaleta katika kuwalinda raia hawa, tofauti kati ya kuwa salama au kuwa katika hatari kubwa, na nilitaka pia kutoa shukrani zangu kwa wenzetu wa MONUSCO. Aidha, nilitaka kuwasikiliza wananchi, hawa wakimbizi wa ndani, pamoja na jamii, na kuona namna ambavyo tunaweza kushirikiana nao zaidi ili kuboresha hali na kupiga hatua katika kukabiliana na ghasia ambazo bado zinaendelea katika eneo hilo.”Baada ya zira yake jimboni Itari Lacrix ameelekea katika mji Mkuu Kinshasa ambako amekutana na na kuzungumza na maafisa wa serikali.
Ikiwa leo tarehe 8 Septemba ni siku ya Kimataifa ya kujua kusoma na kuandika ambapo Umoja wa Mataifa ulianzisha siku hii ili kuwakumbusha watunga sera, walimu, wadau wa elimu, na jamii juu ya umuhimu wa ujuzi wa kusoma na kuandika katika kujenga jamii yenye elimu, haki, amani na endelevu, Sabrina Saidi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa anaiangazia kauli mbiu ya mwaka huu "Kukuza ujuzi wa kusoma na kuandika katika zama za kidijitali" akiwashirikisha baadhi ya wadau wa elimu nchini Tanzania.Amezungumza na baadhi ya wadau kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino, SAUT kilichoko jijini Mwanza, kaskazini-magharibi mwa Tanzania.Dismas Nziku ni mwalimu wa masomo ya Biashara na Ujasiriamali anazungumza kuhusu ni kwa jinsi gani ufundishaji wa zama hizi za kidijitali unavyochochea na kukuza ujuzi wa kusoma na kuandika. "Kwenye dunia ya sasa ujuzi wa kusoma na kuandika kidijitali ni msingi mkubwa kwa mwanafunzi, na miongoni mwa juzi hizi muhimu ni kama vile kujua kutumia vifaa vya kidijitali kama kompyuta, simu janja kwa ajili ya kujisomea na kutafuta maarifa, lakini pia kama mwalimu ninawafundisha wanafunzi kwa njia ya vitendo,kuandaa maswali ya utafiti kwa kutumia internet,kufanya kazi na kufanya kazi ya kikundi mitandaoni."Kuhusu umuhimu wa siku hii kwake na inachangia vipi katika kukuza uelewa wa umuhimu wa kusoma na kuandika shuleni na katika jamii Mwalimu Nziku amesema, "Siku ya Kimataifa ya kujua kusoma na kuandika ni kumbusho muhimu kwamba elimu ni haki ya msingi, na ni msingi wa maendeleo kwa kila mmoja kujua kusoma na kuandika hasa hasa kidijitali, inanipa hamasa kama mwalimu kuendelea kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kusoma na kuandika si kwa ajili ya mitihani tu, bali kwa maisha yao ya kila siku."Didas Karoli ni mwanafunzi katika chuo hicho cha SAUT akisoma shahada ya kwanza ya Mawasiliano kwa Umma, ameeleza kuhusu siku hii na jinsi maendeleo ya kidijitali yanavyochagiza katika kujifunza kwake akisema "Zana za kidijitali zimebadilisha sana upeo wangu katika suala la kujifunza,kutokana na zamani nilikuwa nategemea vitabu lakini hivi sasa natumia tu smartphone au kompyuta na kutengeneza notisi zangu mwenyewe za kujifunzia.Siku ya hii ya kujua kusoma na kuandika ni siku ambayo ni muhimu inafanya watu waweze kujua umuhimu wa kusoma na kuandika."
Katika jitihada za kuimarisha amani na usalama katika maeneo yaliyoathiriwa na machafuko ya kikabila nchini Sudan Kusini, Umoja wa Mataifa kupitia Ujumbe wake wa amani nchini humo UNMISS wameendelea kuimarisha ulinzi na kuongeza doria za magari usiku na mchana huko Greater Tambura katika jimbo la Equatoria Magharibi.Sabrina Saidi anaangazia juhudi za UNMISS katika kuhakikisha hali ya usalama inarejea na wananchi waliokimbilia katika kambi za wakimbizi kusakama usalama wanarejea makwao.TAARIFA YA SABRINA SAIDI)NAT...Video ya UNMISS inaanza kwa kumulika doria zinazofanywa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa huko katika kaunti ya Greater Tambura katika jimbo la Western Equatoria, kusini-magharibi mwa nchi ya Sudan Kusini karibu na mipaka ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC na Jamuhuri ya Afrika ya Kati.Tangu mwaka 2021, mizozo ya wenyewe kwa wenyewe, umeendelea kugharimu maisha ya watu wengi na kuwalazimu maelfu kuyakimbia makazi yao.Wananchi waliokumbwa na hofu wamekuwa wakijificha vichakani, wengine wakikimbilia nchi jirani, huku wengi wakitafuta hifadhi katika kambi mbalimbali za wakimbizi wa ndani zilizopo maeneo ya karibu.Ili kuwalinda vyema raia UNMISS wameimarisha uwepo wao katika eneo hilo na kuongeza doria za magari usiku na mchana, wakipita katika barabara mbovu zilizotapakaa tope na kuharibiwa na mvua. Walinda amani hao maarufu kama 'Blue Helmets', wamekuwa wakitembelea kambi mbalimbali za wakimbizi wa ndani na kuzungumza na jamii mbalimbali za kikabila zilizopata hifadhi huko.Tereza Martin ni mmoja wa wakimbizi wa ndani aliyepata hifadhi na hapo, anazungumza kwa hofu na simanzi...CUT: Sauti ya Tereza Martin"Hatuelewi chanzo cha mzozo huu. Tumekuwa tukiishi katika kambi hii kwa takribani miaka sita, tukiishi kwa njaa na mateso. Makazi yetu ya muda ni mabovu. Msimu wa mvua umefanya hali kuwa mbaya zaidi, sasa tunalala juu ya maji ya mvua. Hatuwezi kwenda shambani kwa hofu ya kushambuliwa. Tunaomba serikali na wadau kutuangalia kwa jicho la huruma."NAT....Margret Dominic naye ni mkimbizi wa ndani kambini hapo, anasema doria hizi zinampa amani CUT: Sauti ya Margret Dominic-"Hatuwezi kutoka nje ya kambi. Tunaweza kulala kwa sababu wanapiga doria usiku. Kama wasingekuwepo, hatujui kama tungeweza hata kupata usingizi."Emmanuel Dukundane ni Afisa wa Masuala ya Kiraia wa UNMISS, anasema wanajenga kambi mpya katika maeneo ya kimkakati.CUT: Sauti ya Emmanuel DukundaneHili lina maana kubwa sana kwa sababu tuna rasilimali nyingi, na kwa kujiweka katika kambi hiyo mpya, tutaweza kufanya doria zaidi, kufanya mazungumzo zaidi, na kuwezesha mchakato wa upatanisho na amani kwa ujumla."Ingawa UNMISS itaendelea kuisaidia serikali ya Sudan Kusini katika kuwalinda raia wa Greater Tambura, amani ya kweli na upatanisho wa kudumu vinapaswa kukubaliwa na kupatikana kupitia juhudi za jamii husika na viongozi wao wenyewe.