Makala ya Wimbi la Siasa inakupa fursa ya kufahamu masuala ya kisiasa yanayoendelea ndani na nje ya Bara la Afrika. Kwenye Makala haya utapata habari ambazo zinakugusa moja kwa moja wewe msikilizaji. Kila wakati usikose kusikiliza Makala ya Wimbi la Siasa
Rfi - Victor Melkizedeck Abuso

Joto la kisiasa limeendelea kupanda kwenye chama cha siasa cha ODM nchini Kenya kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Chama hicho kilichoanzishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita na aliyekuwa Waziri Mkuu Marehemu Raila Odinga, kimegawanyika kwa makundi mawili. Kundi moja linaongozwa na Oburu Oginga, kaka yake Raila, linamuunga mkono rais William Ruto. Kundi lingine, linangozwa na Edwin Sifuna, Katibu Mkuu anayempinga Ruto. Nini hatima ya chama hiki ?

Wawezeshaji na wasuluhishi wa mzozo wa Mashariki mwa DRC kutoka Umoja wa Afrika, wanataka usitishwaji wa vita na utekelezwaji wa mkataba wa amani wa Washington na kuheshimu mchakato wa Doha. Ni kwanini inakuwa vigumu kutekeleza mkataba huo kuheshimu maelewano ya Doha ? Tunachambua.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi amesema serikali yake ipo tayari kuongoza mazungumzo kati ya Wakongomani, ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi hiyo, hasa utovu wa usalama, mashariki mwa nchi hiyo. Hata hivyo, Chama cha "Ensemble pour la République, kinachoongozwa na mwanasiasa mashuhuri wa upinzani Moise Katumbi, kinasema mazungumzo hayo yanaweza kufanyika tu iwapo yatawashirikisha wadau wote. Rais Tshisekedi, wanaotekeleza mauaji ya raia, hawapaswi kushirikishwa kwenye mazungumzo hayo. Tunachambua.

Chama cha ODM kilichoanzishwa na aliyekuwa Waziri Mkuu nchini Kenya Hayati Raila Odinga, kinapitia mgawanyiko wa kisiasa kuhusu kumuunga mkono rais William Ruto kuwania urais kwa muhula wa pili. Viongozi wa chama hicho wamegawanyika kuhusu mpango huo kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Mvutano huu unamaanisha nini ?

Rais Yoweri Museveni, mwenye umri wa miaka 81, na ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 40, alitangazwa mshindi wa uchaguzi mkuu wa Januari 15 baada ya kupata asilimia 71.65 ya kura. Mpinzani wake wa karibu Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine mwenye umri wa miaka 43, alimaliza wa pili kwa kupata asilimia 24.72 ya kura. Bobi Wine amedai kuibiwa kura. Ushindi wa rais Museveni unamaanisha nini ?

Uchaguzi wa wabunge na urais nchini Uganda unafanyika Januari 15, 2026. Rais wa muda mrefu Yoweri Museveni ambaye ameongoza kwa miaka 40, anapambana tena na mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine. Upinzani umelalamikia kunyanyaswa, wakati huu mtandao wa Interneti ukizimwa. Je, uchaguzi huu utakuwa huru na haki ? Tunachambua kutoka Kampala.

Rais Donald Trump, Januari 3, 2026, aliagiza operesheni maalum ya wanajeshi wa Marekani nchini Venezuela, kumteka kiongozi wa nchi hiyo Nicolas Maduro. Baada ya kitendo hicho ambacho kimelaaniwa duniani, Maduro alisafirishwa jijini New York na kufunguliwa mashtaka ya kuongoza biashara haramu ya dawa za kulevya nchini Marekani. Tunachambua hatua hii ya rais Trump, inamaanisha nini ?

Matukio makubwa ya kisiasa tuliyochambua mwaka 2025 ni pamoja na kifo cha aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri nchini Kenya Raila Odinga, uchaguzi wenye vurugu uliofanyika nchini Tanzania Oktoba 29 na kutiwa saini kwa mkataba wa kumaliza vita Mashariki mwa DRC, Desemba 04, jijini Washington DC nchini Marekani.

Baada ya shinikizo kutoka kwa Marekani, waasi wa M23/AFC waliondoka kwenye mji wa Uvira, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Hata hivyo, rais Felix Tshisekedi ameelezea kitendo hicho kama kiini macho kwa jumuiya ya Kimataifa, kauli ambayo imeungwa na mkono na jeshi la FARDC wanaosema, waasi hao wamejificha katika milima inayopatikana na mji huo. Kuchambua kinachoendelea, tunaungana Mali Ali akiwa jijini Paris na François Alwende akiwa jijini Nairobi.

Hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, si shwari licha ya kutiwa saini kwa mkataba unaolenga kusitisha vita ambavyo vimekuwa vikiendelea kwa muda wa miaka 30. Waasi wa M23/AFC wameudhibiti mji wa Uvira. Marekani inaonya kuichukulia hatua Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao ambao sasa wameahidi kuondoa vikosi vyake katika mji huo, lakini kwa masharti. Tunachambua kwa kina.

Kampeni za uchaguzi nchini Uganda zimezidi kupamba moto kuelekea uchaguzi mkuu January 15 2025 ambapo Rais Yoweri Museveni aliyeingia madarakani mwaka wa 1986, anagombea tena muhula wa saba huku akishindana na wagombea wengine miongoni mwao mwanasiasa wa upinzani Robert Kyagulanyi Ssentamu almaarufu Bobi Wine. Kampeni za mwaka huu zinafanyika huku mgombea wa Upinzani Bobi wine akilalamika kushambuliwa na maafisa wa usalama. Kupata mengi zaidi ungana na mwandishi wetu Ruben Lukumbuka

Makala ya wimbi la siasa, imeangazia hatua ya viongozi wa Rwanda na DRC ambao siku ya alhamisi desemba 04 watatia saini makubaliano ya amani, mbele ya rais wa Marekani Donald Trump hii ikiwa ni mwendelezo wa mapatano ya amani mashariki mwa DRC yaliyosimamiwa na Marekani yaliyotiwa saini na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili juni 27. Profesa Pacifique Malonga ni mchambuzi wa siasa akiwa Kigali Rwanda, pia Francois Alwende ni mtaalamu wa siasa za maziwa makuu akiwa Nairobi Kenya.

Chama kikuu cha upinzani nchini Kenya cha Orange Democratic Movement-ODM kina kiongozi mpya, Seneta Oburu Oginga, kaka yake kiongozi wa zamani wa chama hicho Hayati Raila Odinga aliyefariki dunia mwezi Oktoba. Je, atafanyaje, kukiunganisha chama hicho ambacho kinaonekana kugawanyika kuhusu ushirikiano wake na uongozi wa rais William Ruto ? Tunachambua.

Nchi za Afrika Mashariki za Kenya, Uganda na Tanzania, zimeendelea kushuhudia ongezeko la visa vya wakosoaji wa serikali kutekwa na kupotezwa. Hivi karibuni, wanaharakati wawili kutoka nchini Kenya, Bob Njagi na Nicholas Oyoo walitekwa zaidi ya mwezi mmoja uliopita nchini Uganda, baada ya kuhudhuria kampeni za uchaguzi za Bobi Wine, waliachiwa baada ya shinikizo za watetezi wa haki za binadamu. Nani atakomesha utekaji ?

Machafuko yalikumba uchaguzi mkuu wa Tanzania, uliofanyika Oktoba 29, 2025 na rais Samia Suluhu Hassan kutangazwa mshindi kwa kupata asilimia 97.6 ya kura. Chama kikuu cha upinzani CHADEMA, kimesema ushindi wa Samia ni kichekesho cha demokrasia. Anapaswa kufanya nini ili kuirejesha Tanzania katika utulivu wa kisiasa ? Tunachambua.

Watanzania wanapiga kura kuwachagua wabunge, madiwani na rais, katika uchaguzi ambao rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuibuka mshindi, baada ya mpinzani wake mkuu Tundu Lissu, kuzuiwa jela na kufunguliwa mashtaka ya uhaini.

Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila, anakutana na wanasiasa wa upinzani jijini Nairobi, kuanzia Oktoba 14, wiki mbili baada ya kuhukumiwa kifo na Mahakama ya kijeshi. Wanasiasa hao wanazungumza nini ? Tunachambua.

Wachambuzi wa mambo wanaona kuwa waasi wa AFC/M 23 wanaendelea kujiimarisha zaidi kisiasa na kiuchumi, katika maeneo wanayodhibiti, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, licha ya kuwepo kwa mkataba wa Washington uliokubaliwa kati ya DRC na Rwanda kuhusu namna ya kupata mwafaka wa kudumu. Hatua hii inamaanisha nini ? Tunachambua.

Kampeni za uchaguzi mkuu nchini Uganda, uliopangwa kufanyika Januari 12, 2026, zilianza Septemba 29. Kuna wagombea wanane wa urais, akiwemo kiongozi wa muda mrefu Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 81, ambaye ameongoza nchi hiyo kwa miaka 39. Mpinzani wake mkuu ni Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, mwenye umri wa miaka 43. Nini kinachotarajiwa kwenye kampeni hizi ?

Vital Kamerhe, Septemba 22, alijiuzulu kama Spika wa Bunge la taifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya kuundwa kwa Tume ya kumchunguza dhidi ya madai ya matumizi mabaya ya madaraka, kuwahangaisha wabunge na kuwalazimisha kupitisha miswada haraka haraka.Nini hatima ya kisiasa ya Kamerhe baada ya kujiuzulu ? Ataendeleza ushirikiano wake wa karibu na rais Felix Tshisekedi ?

Nchini Sudan Kusini, serikali ya rais Salva Kiir, imetangaza kumfungulia mashtaka ya uhaini na uhalifu wa kivita, kiongozi wa upinzani Riek Machar, ambaye ameondolewa kwenye nafasi ya Makamu wa kwanza wa rais, kufuatia shambulio la wapiganaji wa White Army kwenye kambi ya jeshi katika jimbo la Upper Nile mwezi Machi mwaka 2025. Nini hatima ya Machar na Sudan Kusini ?

Mji wa Uvira, jimboni Kivu Kusini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa zaidi ya wiki moja, ikiwemo Septemba 08, umeshuhudia maandamano yaliyopangwa na mashirika ya kiraia na wapiganaji wa Wazalendo, kupinga kupinga kuteuliwa kwa Jenerali Olivier Gasita, kuwa Naibu Kamanda wa Kikosi cha jeshi la FARDC, katika eneo hilo kwa madai ya kuwa na ushirikiano na waasi wa AFC/M23 kwa sababu ya kabila lake la Banyamulenge.

Tanzania inaingia kwenye kampeni za uchaguzi Mkuu kuanzia Agosti 28, kuelekea kufanyika kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba, 29 2025. Rais Samia Suluhu Hassan, kutoka chama tawala CCM, anawania uongozi wa nchi hiyo. Mpinzani wake mkuu Tundu Lissu anaendelea kuzuiwa jela, kwa tuhma za uchochezi na uhaini.

Rais wa Marekani Donald Trump, amechukua hatua ya kuongoza harakati za kumaliza vita vya miaka mitatu vya Urusi nchini Ukraine. Trump amekutana na rais Vladimir Putin na Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine pamoja na viongozi wengine wa nchi za Ulaya Agosti 18, baada ya awali kukutana na rais Putin Agosti 15 jimboni Alaska. Je, Trump atafanikiwa kumaliza vita hivyo ?

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa M 23/AFC, Julai 19, walitia saini rasimu ya makubaliano jijini Doha nchini Qatar ya namna ya kusitisha vita Mashariki mwa DRC na kupata amani ya kudumu. Ni mambo yepi yaliyokubaliwa na changamoto zipi zinazokabili pande hizi mbili kwenye utekelezwaji ? Tunajadili.

Kiongozi wa muda mrefu nchini Uganda Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 80, ameteuliwa na chama chake cha NRM, kugombea tena urais wakati wa uchaguzi mkuu uliopagwa kufanyika mapema mwaka 2026, baada ya kuwa madarakani miaka 40. Hii inamaanisha nini katika siasa za Uganda ?

Vijana nchini Kenya maarufu kama Gen Z, wameendelea kuandamana dhidi ya serikali ya rais William Ruto. Maandamano haya yameishia kwenye maafa na majeruhi tangu mwezi Juni mwaka 2024. Tunaungana na wanafunzi wa chuo cha ufundi cha NIBS kilichopo Ruiru, kusikia kutoka kwao. Kwanini wanaandamana ?

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda, walitia saini mkataba wa amani, chini ya uangalizi wa Marekani, Juni Juni 27 2025, jijini Washington DC, unaolenga kurejesha amani ya kudumu Mashariki mwa DRC. Nchi hizo mbili zimekubaliana kushirikiana kuyaondoa makundi yenye silaha. Mkataba huu umepokelewa vipi nchini DRC ?

Israel na Iran zimekubali pendekezo la rais wa Marekani Donald Trump, kuacha kushambuliana baada ya vita vya siku 12 vilivyosababisha vifo zaidi ya 600 nchini Iran na zaidi ya 20 nchini Israeli. Israeli ilianza mashambulio hayo, kwa kulenga vituo vya nyuklia vya Iran kwa lengo la kuizuia kutengeneza silaha za maangamizi. Je, usitishwaji huu wa vita utadumu ?

Serikali ya Kenya mwezi Januari 2025, ilisaini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara na nchi ya Falme za Kiarabu kukuza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Mswada huo umezua pingamizi kubwa kutoka kwa wanaharakati, watunga será na wapinzani wa serikali na wanataka wabunge kuufanyia marekebisho. Je, kuna siasa gani kwenye mikataba ya Kimataifa inayotiwa saini kati ya serikali ya Kenya na nchi za kigeni ? Edgar Odari Mkurugenzi Mkuu wa, Econews Africa, na Torosterdt Alenga mchambuzi wa siasa za Kimataifa, wanathathmini.

Rais wa Marekani Donald Trump ameagiza raia wa nchi 12 hasa kutoka Afrika kutozuru nchi hiyo. Agizo hilo lilianza kutekelezwa Juni 9, 2025. Trump anasema amechukua hatua hii kwa sababu za kiusalama. Wakati hayo yakijiri, maandamano yamekuwa yakishuhudiwa katika mji wa Los Angeles, kupinga sera ya Trump ya kuwasaka na kuwafukuza nchini humo, wageni wanaoishi bila vibali. Tunachambua kwa kina.

Uongozi wa kijeshi nchini Sudan mwishoni mwa mwezi Mei, ulimteua mwanasiasa na mwanadiplomasia mkongwe Kamil Idris, kuwa Waziri Mkuu mpya wakati huu vita vikiendelea kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF. Tangu kuanza kwa vita Aprili 2023, watu zaidi ya 20,000 wamepoteza maisha, huku wengine Milioni 15 wakikimbia makaazi yao, wakiwemo zaidi ya Milioni nne ambao wamekimbilia katika nchi jirani kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa. Nini hatima ya Sudan ?

Maseneta nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wamemwondolea kinga ya kutoshtakiwa rais wa zamani Joseph Kabila , ambaye ripoti zinasema alirejea Goma usiku wa Mei 25.Kiongozi huyo wa zamani, ameishtumu serikali ya rais Felix Tshisekedi na kuuita ya Kidikteta. Hata hivyo, serikali ambayo inamtuhumu kiongozi huyo wa zamani kwa kushirikiana na waasi wa M23.

Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu na Mawakili mashuhuri kutoka nchini Kenya, akiwemo Martha Karua na Jaji Mkuu mstaafu Willy Mutunga, walifukuzwa nchini Tanzania, Mei 19, walikokuwa wamekwenda kama mashuhuda wa kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani Tundu Lissu. Rais Samia Suluhu Hassan ameonya kuwa nchi yake haitaruhusu wanaharakati kutoka nje, kuvunja amani ya nchi yake. Tunachambua kilichotokea nchini Tanzania.

Mswada tata, utakaoruhusu raia wa kawaida kushatakiwa kwenye Mahakama za kijeshi, umewasilishwa bungeni nchini Uganda, Mei 13, 2025. Upinzani unasema, lengo la mswada huo ni kuwalenga wanaopinga kiongozi wa muda mrefu Yoweri Museveni kuelekea uchaguzi Mkuu wa mwaka 2026. Kwanini serikali ya Uganda inataka raia wa kawaida washtakiwe kwenye Mahakama za kijeshi ?

Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, zimewasilisha mapendekezo ya rasimu ya mkataba wa amani kwa Marekani, kujaribu kutafuta mzozo wa Mashariki mwa DRC. Nchi hizo mbili zinatarajiwa kutia saini mkataba wa kudumu mwezi Juni, jijini Washington. Harakati hizi, zitazaa matunda ?

Wanasiasa wakuu wa upinzani nchini Kenya, wakiongozwa na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, Aprili 29 2025, walikutana jijini Nairobi kuanza mikakati ya kuunda muungano mpya, kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. Je, muungano huu ambao pia umemjumuisha aliyekuwa Waziri wa usalama Fred Matiang'i, unaweza kumtikisa rais William Ruto wakati wa uchaguzi huo ?

Rais wa zamani wa DRC, Joseph Kabila, Aprili 18, aliripotiwa kurejea nchini na kufikia jijini Goma, linalodhibitiwa na waasi wa M 23. Hata hivyo, taarifa hizi hazijathibitishwa rasmi. Serikali jijini Kinshasa, nayo imesitisha shughuli zote za kisiasa za chama chake cha PPRD. Kabila anashtumiwa na serikali kwa kuunga vitendo vya waasi hao.

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu, Aprili 10 alifunguliwa kesi ya uhaini, baada ya kukamatwa akiwa kwenye kampeni ya kisiasa, kushinikiza mageuzi kwenye mchakato wa uchaguzi, uliopangwa kufanyika mwezi Oktoba.

Mwezi Oktoba 2025, wananchi wa Tanzania, watashiriki kwenye uchaguzi Mkuu, kuwachagua madiwani, wabunge na rais. Hata hivyo, chama kikuu cha upinzani cha CHADEMA, kikiongozwa na Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, kinashinikiza mageuzi kwenye sheria za uchaguzi kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.Je, kitafanikiwa katika harakati zake ?

Mkuu wa Majeshi nchini Kenya, Jenerali Jenerali Charles Kahariri na Mkuu wa idara ya ujasusi Noordin Haji, wameonya dhidi ya kampeni inayoendelea kwenye mitandao ya kijamii na mikutano ya hadhara ya –Ruto Must Go- au Ruto lazima aondoke, inatishia hali ya kisiasa nchini Kenya na ni lazima, ikome.Je, jeshi la Kenya linaingilia siasa ? Tunajadili…

Wiki hii tunaangazia kinachojiri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, baada ya Angola kujiondoa kama mpatanishi wa mazugumzo ya mzozo wa Mashariki mwa nchi hiyo, rais Paul Kagame na Tshisekedi wakutana Doha na mazungumzo ya kisiasa yanayolenga kuunda serikali ya umoja wa kitaifa, yazinduliwa jijini Kinshasa.Wachambuzi wetu ni Mali Ali, akiwa Paris na Francois Alwende akiwa jijini Nairobi.

Sudan Kusini inakabiliwa na wasiwasi wa kujipata tena kwenye vita vipya, kufuatia mzozo wa hivi punde kati ya vikosi vya rais Salva Kiir na Makamu wake wa kwanza wa Riek Machar, baada ya kushambuliana kwenye jimbo la Upper Nile.Nini kinaweza kufanyika kuzuia mzozo mpya ?Wachambuzi wetu ni Dokta Brian Wanyama, kutoka Kenya na Hamdum Marcel akiwa Mwanza, Tanzania.

Wakati huu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, inapoendelea kukabiliwa na changamoto ya usalama Mashariki mwa nchi hiyo, baada ya waasi wa M23 kuingia katika miji ya Bukavu na Goma, rais Felix Tshisekedi ametangaza mpango wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa kuwashirikisha wanasiasa wa upinzani.Tunajadili iwapo hatua hii itasaidia kutatua mzozo wa mashariki mwa DRC.

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga , yupo kwenye harakati za mashauriano ya kisiasa na wafuasi wake, kabla ya kutangaza mustakabali wake wa kisiasa baada ya kukosa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika. Je, Raila ataegemea upande gani ? Tunachambua.

Wajumbe wa kisiasa kutoka kundi la RSF linaloongozwa na Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo linalopigana na wanajeshi wa Sudan, walikutana jijini Nairobi na kutia saini mkataba wa uundwaji wa serikali mbadala kwenye maeneo wanayodhibiti. Nini hatima ya mzozo wa Sudan ?

Waziri wa Mambo ya nje wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf alichaguliwa na wakuu wa mataifa ya Afrika Februari 15 2025, kuwa Mwenyekiti mpya wa Tume ya Umoja wa Afrika na kumshinda mwanasiasa mkongwe na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga. Tunachambua ushindi wake na kazi kubwa inayomsubiri

Makala ya Wimbi la Siasa wiki hii tunaangazia maazimio ya wakuu wa serikali na nchi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC waliokutana Februari jijini Dar es Salaam, kuthathmini hali ya usalama Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Miongoni mwa maazimio hayo ni usitishwaji wa vita bila masharti kati ya waasi wa M23 na wanajeshi wa DRC na kutoa wito wa mazungumzo.Wachambuzi wetu ni Chube Ngorombi akiwa Goma, na Francois Alwende akiwa jijini Nairobi.

Rais wa Marekani Donald Trump, baada ya kurejea madarakani Januari 20, ametangaza hatua ya serikali yake, kusitisha misaada hasa ya kifedha kwa nchi za kigeni, kupitia Shirika la Misaada ya Kimataifa (USAID).Hatua hii inamaanisha nini hasa kwa mataifa ya Afrika ? Tunajadili hili kwa akina na Suba Churchil, rais wa kituo cha taifa cha mashirika ya kiraia akiwa jijini Arusha Tanzania.

Wiki hii mapigano makali yameshuhudiwa jijini Goma, kati ya wanajeshi wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa M 23 wanaoripotiwa kuungwa mkono na nchi ya Rwanda. Nini suluhu ya mzozo wa Mashariki mwa DRC ?

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameteuliwa kwa kauli moja na wajumbe wa chama cha mapinduzi CCM kupeperusha bendera ya chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba. Tunachambua hatua hii.