POPULARITY
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) yanatambua kuwa kuwawezesha vijana, kulinda mazingira na kuimarisha uhakika wa kupata chakula ni miongoni mwa nguzo muhimu za kujenga jamii zenye ustahimilivu na maendeleo endelevu. Kupitia malengo kama vile la Kutokomeza umaskini, kutokomeza njaa na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi , jamii zinahimizwa kuwekeza katika suluhisho zinazowawezesha wananchi kujitegemea huku zikihifadhi mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Hatua hizo zinatekelezwa katika enoe la Kajiado Kaskazini, katika kaunti ya Kajiado, kusini mwa Kenya kama anavyosimulia Kelvin Keitany wa radio washirika, Domus Radio.Hii leo Umoja wa Mataifa umekuwa na matukio mbalimbali ya kuadhimisha siku ya Mandela, Rais wa kwanza mweusi wa taifa la Afrika Kusini kwa mchango wake wa utetezi wa haki. Miongoni mwa kulikofanyika maadhimisho hayo ni Nairobi, Kenya ambako Stella Vuzo wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa alikuwa shuhuda wetu. Licha ya idadi ya magari duniani kuongezeka kwa zaidi ya bilioni moja, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani WHO limesema vifo vinavyotokana na ajali za barabarani vimepungua kwa asilimia 21 kati ya mwaka 2011 na 2025. Hata hivyo, ajali hizo bado zilisababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 1 mwaka jana na zinaendelea kuwa chanzo kikuu cha vifo kwa watoto na vijana wenye umri wa miaka 5 hadi 29Na, Je, msikilizaji wangu, uliwahi kujiuliza kwa nini binadamu bado wanarudi kuchunguza Mwezi ulioko anga za juu , zaidi ya miaka 50 baada ya kutua huko kwa mara ya kwanza? Leo Julai 20, dunia inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya mwezi. Umoja wa Mataifa uliitenga siku hii kuenzi tukio la kihistoria la mwaka 1969, wakati wanaanga wa safari ya Apollo 11 walipoweka nyayo za kwanza za binadamu mwezini. Lakini maadhimisho haya hayaishii kwenye historia tu bali yanasisitiza pia umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika utafiti wa anga za juu na kuhakikisha uchunguzi wa mwezi unafanyika kwa amani na kwa manufaa ya watu wote duniani.".Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina, leo tunamsikia Pauline Farini Kibuya wa shirika la Congo Notre Avenir yaani Congo Mustakabali Wetu kutoka DRC akizungumza na Idhaa hii kuhusu jinsi wanavyosongesha amani kwa taifa la DRC Congo. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na jifunze Kiswahili.Katibu Mkuu António Guterres aliyeko ziarani nchini China amehutubia mdahalo kuhusu Tahadhari za Mapema kwa Wote katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi unaofanyika kwenye jukwaa la kimataifa la Akili Mnemba na Tabianchi jijini Shanghai na kutoa wito wa kuharakisha maendeleo ya mifumo ya tahadhari za mapema inayotumia akili mnemba ili kuzuia majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo amesema "tahadhari lazima zifikie kila mtu aliyeko hatarini kwa lugha wanazoelewa na mifumo ya mawasiliano wanayoweza kuiamini."Kesho Julai 18 ikiwa ni siku ya kimataifa ya Nelson Mandela, Rais wa Kwanza Mweusi wa Afrika Kusini, huko Geneva, Uswisi hii leo mashindano ya 18 ya Nelson Mandela ya Mahakama ya Kimataifa ya Kuigiza yamefikia kilele kwa timu ya Chuo Kikuu cha Midlands State kutoka Zimbabwe kuibuka mshindi ilihali Chuo Kikuu cha Strathmore kutoka Kenya kimeshika nafasi ya pili.Hii leo hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, nchi wanachama na marafiki wa mpira wa miguu au kabumbu, wamezindua kampeni ya mwaka mmoja ya Dunia Moja, Mchezo Mmoja, Lengo Moja kwa lengo la kutumia mpira wa miguu kama kichochea cha kuimarisha afya ya akili kwa vijana, tukio linalofanyika siku mbili kabla ya fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia kwa wanaume. Akizungumza mapema kabla ya tukio hilo Sahira Al Nahari, ambaye ni Kiongozi kijana mchechemuzi wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs amesema, "kwa hiyo, mpira wa miguu una mengi ya kutufundisha. Tunapokabiliwa na janga la kimataifa, hebu tuzielekeze fikra zetu kwenye viwanja vya mpira wa miguu. Tunapotazama kinachotokea viwanjani, tunajifunza nidhamu, ustahimilivu, na jinsi ya kuinuka tena baada ya kupoteza jambo muhimu sana."Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili na hii leo Dkt Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana na matumizi ya neno "CHOPOCHOPO."Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya stadi kwa vijana tunamulika jinsi gani vijana waliojiendeleza katika stadi ya akili mnemba au wengine wanaita akili unde, kwa kiingereza Artificial Intelligence au AI, wanarahisisha maisha ya jamii. Na tunamuangazia kijana Kalebu Gwalugano kutoka Tanzania, Muasisi na Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Neurotech iliyoanzishwa mwaka 2022. Kijana huyu ni Mhandisi wa AI na akiwa Dar Es Salaam, mji mkuu wa kibiashara wa taifa hilo la Afrika Mashariki, amezungumza na mwenzetu Japhael Jambo. Pia tunakuletea Muhtasariw a habari.Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Stadi za Vijana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres amesema kuwezesha vijana kufikia uwezo wao kamili kunahitaji uwekezaji mkubwa katika elimu na mafunzo jumuishi yenye ubora. Ametambua mchango wa vijana kote duniani kwamba wanaendelea kutoa mchango mkubwa kama wabunifu, viongozi na mawakala wa mabadiliko katika kujenga jamii zenye usawa, ustahimilivu na maendeleo endelevu hata hivyo mabadiliko ambayo dunia inapitia sasa yakichochewa na maendeleo ya teknolojia za kidijitali, athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika wa kiuchumi na pengo la usawa yanahitaji vijana kuwa na ujuzi mpya unaowawezesha kushindana na kunufaika na fursa zinazojitokeza.Ingawa mwaka 2025 duniani kiwango cha chanjo kwa watoto kiliongezeka kwa asilimia moja ikilinganishwa na mwaka uliotangulia, kiwango cha chanjo bado kiko asilimia moja chini ya kiwango cha mwaka 2019, kikiwa kimeendelea kubaki ndani ya kiwango finyu tangu mwaka 2009. Hayo ni kwa mujibu wa makadirio ya kila mwaka ya mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa lile la afya duniani, WHO na la kuhudumia watoto, UNICEF kuhusu viwango vya kitaifa vya chanjo.Na ripoti mpya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu OHCHR inazitaka pande zinazohusika katika vita nchini Sudan, pamoja na serikali na kampuni zinazofanya biashara ya Gum Arabic, gundi inayotokana na aina fulani ya miti ya Acacia kuhakikisha shughuli zao zinaendana na sheria za kimataifa na hazichangii kuendeleza mzozo.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka katika mkutano wa HLPF hapa makao makuu ya UN kumsikia Profesa Peter Wanderi Mwangi ambaye amewakiwakilisha Chuo Kikuu cha Mount Kenya cha nchini Kenya chenye matawi mbalimbali katika Afrika Mashariki katika mkutano wa United Nations Academic Impact (UNAI), Mpango unaosisitiza nafasi muhimu ya taasisi za elimu ya juu katika kuhimiza maendeleo endelevu na kuunga mkono utekelezaji wake. Baada ya ziara yake mjini Bunia, jimboni Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ambako ndio kitovu cha mlipuko wa sasa wa Ebola ya virusi vya Bundibugyo, Mkurugenzi Mtendaji wa WHO anayehusika na Programu ya Dharura za Afya, Dkt. Chikwe Ihekweazu, amewambia waandishi wa habari Geneva, Uswisi kwamba mlipuko wa sasa ni moto ambao kinachouchochea kiko katikati, huku ukiendelea kusambaa.Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Bahari (IMO) limesema lina wasiwasi mkubwa kufuatia mashambulizi ya jana usiku yaliyolenga meli kwenye mlango wa bahari wa Hormuz na viunga vyake na kusababisha vifo vya takribani mabaharia wawili na wengine kadhaa wamejeruhiwa. Kupitia taarifa yake iliyotolewa London, Uingereza, IMO imesema inafanya kazi kwa haraka na mamlaka husika ili kubaini mazingira halisi ya tukio hilo.Na uungwaji mkono wa umma kwa wakimbizi unaendelea kuwa imara licha ya kuwepo kwa changamoto na kutokuweko kwa uhakika wa mustakabali duniani, hii ni kwa mujibu wa utafiti wa pamoja uliofanywa na kampuni ya IPSOS na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Utafiti umebaini kuwa asilimia 66 ya washiriki katika nchi 29 wanakubaliana kwamba watu wanaokimbia vita au mateso wanapaswa kuruhusiwa kusaka hifadhi katika nchi nyingine, ikiwa ni punguzo la asilimia moja tu ikilinganishwa na mwaka 2025.Utafiti huu umefanywa ikiwa ni miaka 75 tangu kupitishwa kwa Mkatab awa Kimataifa wa kulinda wakimbizi.Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!
Taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Baharini (IMO) imeeleza kuwa Baraza la shirika hilo lililohitimisha kikao chake cha 137 linasisitiza tena umuhimu wa kulinda haki na uhuru wa usafiri katika maji kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Anold Kayanda ameifuatilia taarifa hiyo.
Karibu katika makala yetu ya leo changu chako chako changu, makala ambayo hukuletea historia ya mambo mbalimbali, utamaduni le parler francophone na Muziki, ambapo leo nakuletea historia ya lugha ya kiswahili. Na kwenye muziki nitakuletea muziki kutoka bendi ya Lelele Afrika kutoka Mombasa nchini Kenya. Mimi ni Ali Bilali, bienvenue, ama Karibu.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya lugha ya Kiswahili nampisha John Kibego wa redio washirika, Kazi Njema Redio nchini Uganda, kukueleza kuhusu harakati za kukuza lugha hiyo barani Afrika wakati huu ambapo UNESCO imeshaitangaza miaka mitano iliyopita kuwa lugha ya kimataifa.John, anamulika mpango wa ujenzi wa makao makuu ya kamisheni ya Kiswhaili ya Mungano wa Afrika. Pia tunakuletea muhtasari wa habari.Ikiwa leo ni maadhimisho ya tano ya Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Kiswahili chini ya Kaulimbiu "Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Uchumi wa Dunia" Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Togolani Mavura anafafanua ni kwa namna gani lugha ya Kiswahili inaweza kuyafanikisha hayo.Ugonjwa wa Ebola umeendelea kusambaa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na idadi ya vifo vya watu imevuka 500 limesema leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO. Mwakilishi wa WHO nchini humo, Dkt. Anne Ancia akizungumza kwa njia ya video kutoka Bunia, mji mkuu wa Jimbo la Ituri mashariki mwa DRC ambako ni kitovu cha mlipuko huu, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwamba kufikia tarehe 4 mwezi huu, serikali ya nchi hiyo ilikuwa imerekodi wagonjwa 1,561, vikiwemo vifo 506. Taarifa njema ni kuwa…“Jaribio la kitabibu lilianza tarehe 2 Julai kwa lengo la kubaini tiba madhubuti dhidi ya ugonjwa huo unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo.”Na asubuhi hii kwa saa za New York Marekani, kwa mara ya 34 tangu mwaka 1992, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekaa ili kujadili umuhimu wa kumaliza vikwazo vya kiuchumi na kibiashara vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba tangu mwaka 1960. Katika barua ya mwaliko ambayo Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock amewapelekea wajumbe wa Baraza anasema, “ninayo heshima kukujulisha kwamba nimepokea barua iliyoambatanishwa ya tarehe 16 Juni 2026 kutoka kwa Mhe. Bwana Ernesto Soberón Guzmán, Mwakilishi wa Kudumu wa Cuba katika Umoja wa Mataifa, akiomba kuitishwa kwa kikao cha Baraza Kuu ili kujadili ajenda namba 38 yenye kichwa: “Umuhimu wa kukomeshwa kwa vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Cuba.”Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Ikiwa ni siku chache baada ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Watu Wasioona na viziwi inayoadhimishwa tarehe 27 Juni kila mwaka, Rashid Malekela wa Idhaa hii anakupeleka Mashariki ya Kati akimmulika mkazi mwenye ulemavu ambaye anakumbwa na changamoto katikati ya vita.Wakati harakati za uokozi na usaidizi zikiendelea nchini Venezuela baada ya matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 1700 hadi sasa, leo hii ikiwa ni siku ya saba Emily Camargo akiwa kwenye kituo cha hifadhi kilichoandaliwa na Umoja wa Mataifa jimboni La Guaira anaelezea alivyonusurika akisema, “kila kitu kilichonizunguka kiliporomoka na kunizingira, isipokuwa nilipokuweko. Nashukuru kwa sababu jengo la pembeni yetu halikuanguka. Hakuna kilichonipata. Hapa ndio tunalala, mimi, mume wangu , wifi yangu na mbwa wangu. Binadamu yangu na mpenzi wake hatujui waliko tumewatafuta hadi hospitalini, na kwenye orodha, hakuna dalili.”Jopo Huru la Kimataifa la Kisayansi la Umoja wa Mataifa kuhusu akili mnemba, limetoa ripoti leo inayoonesha kuwa teknolojia hiyo inaendelea kusonga mbele kwa kasi kubwa zaidi kuliko uwezo wa serikali kuandaa sera na kanuni zinazoendana nayo. Miaka michache iliyopita, akili mnemba ilikuwa ikitumika zaidi kujibu maswali au kuandika maandishi rahisi. Leo, teknolojia hii inaweza kutengeneza picha na video zenye uhalisia mkubwa na hata kufanya baadhi ya kazi bila usimamizi wa karibu wa binadamu lakini mifumo ya udhibiti na sheria za usalama haijafanikiwa kuendana na mabadiliko hayo.Baada ya miongo kadhaa hatimaye hii leo Umoja wa Mataifa umeondoa kanuni ya kifedha iliyokuwa ikiulazimisha kurejesha kwa nchi wanachama fedha ambazo hazikutumika hata kama fedha hizo hazikuwa zimewasilishwa kabisa. Uamuzi huo uliofanywa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne unafuatia mapendekezo ya Kamati ya Tano, ya Baraza hilo ambayo inashughulikia masuala ya utawala na bajeti. Kanuni ilikwamisha ajira ndani ya Umoja wa Mataifa na operesheni za ulinzi wa amani. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kuwa kanuni hiyo ilikuwa inahatarisha uthabiti wa Umoja wa Mataifa na kwa uamuzi huu, Baraza limeanzisha mbinu mpya itakayohakikisha kuwa fedha ambazo hazijatumika zinarejeshwa kwa nchi wanachama pale tu zinapokuwa zimewasilishwa taslimu na kupokelewa.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili na hii leo Dkt Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana ya neno "MKUNGURU."Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina, leo tunaelekea nchini DRC, kwa Lydie Mwenge, Mwanaharakati wa kupigania haki hususan za wasichana walio na umri wa chini ya miaka 18 walioathirika na vita inayoendelea nchini humo ukiwemo ukatili wa kingono.Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea na harakati za kutoa msaada wa dharura kwa Venezuela kufuatia matetemeko mawili makubwa ya ardhi yaliyolikumba taifa hilo jana Jumatano Juni 24, na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 164 pamoja na uharibifu mkubwa katika mji mkuu, Caracas, na maeneo ya jirani. Matetemeko hayo mawili yenye ukubwa wa 7.2 na 7.5 katika kipimo cha Richter yametokea ndani ya muda wa chini ya dakika moja, yakiharibu nyumba, hospitali, barabara na miundombinu mingine muhimu.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ametoa wito wa kuimarishwa kwa ulinzi wa mabaharia duniani, akionya kuwa ongezeko la migogoro na mivutano ya kisiasa linaweka maelfu ya wafanyakazi wa baharini katika hatari wakati wakiendelea kuhakikisha biashara na usafirishaji wa bidhaa duniani vinaendelea. Katika ujumbe wake wa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mabaharia, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Juni, Katibu Mkuu amesema karibu asilimia 90 ya bidhaa na mahitaji muhimu duniani, ikiwemo chakula, dawa na nishati, husafirishwa kwa njia ya bahari.Na maandalizi ya Mkutano wa 15 wa Afrika Kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Intaneti, AfIGF utakaofanyika mwezi Novemba mwaka huu nchini Ghana yameanza ambapo maoni ya wadau yatakusanywa ili kuweka mazingira salama ya matumizi ya intaneti barani Afrika na hatimaye duniani. Vijana na watoto kutoka nchi mbalimbali wamekutana jijini Nairobi Kenya kuandaa mawazo yao na mmoja wao ni Sheryl Christine Adhiambo kutoka taasisi ya Legal Sisters ya nchini Kenya.Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!
Katika kipindi ambacho idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa duniani inaendelea kuongezeka kutokana na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na changamoto za kiuchumi, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo wa Kumi na Nne (Leo XIV), ametuma ujumbe wa mshikamano kwa kutembelea makao makuu ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, mjini Roma nchini Italia wiki hii. Ziara hiyo imeangazia umuhimu wa kuimarisha juhudi za kimataifa katika mapambano dhidi ya njaa. Flora Nducha na taarifa zaidi
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wakimbizi kesho Juni 20, viongozi wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kuimarishwa kwa mshikamano na hatua za kimataifa za kuwalinda mamilioni ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao kote duniani kutokana na vita, vurugu na mateso. Anold Kayanda amefuatilia na kutuandalia taarifa ifuatayo.
Hii leo jaridani tunaangazia wito wa UN wa kulinda mamilioni wa wakimbizi kote duniani, masuala ya kijinsia Zanzibar nchini Tanzania, na ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa UN kuhusu watoto katika maeneo ya machafuko imeonesha hali ya kutisha duniani.Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wakimbizi kesho Juni 20, viongozi wa Umoja wa Mataifa wametoa wito wa kuimarishwa kwa mshikamano na hatua za kimataifa za kuwalinda mamilioni ya watu waliolazimika kuyakimbia makazi yao kote duniani kutokana na vita, vurugu na mateso.Ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu watoto katika maeneo ya machafuko imeonesha hali ya kutisha duniani. Takribani watoto 24,174 waliuawa, kujeruhiwa, kulazimishwa kujiunga na makundi yenye silaha, kubakwa au kuathiriwa kwa namna nyingine na ukiukwaji mkubwa wa haki katika maeneo yenye mizozo mwaka 2025.Je, maisha yangekuwaje kama kila manusura wa ukatili wa kijinsia angejua mahali pa kupata msaada kwa wakati? Kisiwani Zanzibar nchini Tanzania Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women), kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya (EU) na kwa ushirikiano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, linaimarisha upatikanaji wa haki na huduma za msaada kwa manusura wa ukatili wa kijinsia, hususan katika maeneo ya pembezoni. Kupitia mradi wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Wasichana Zanzibar na Kuimarisha Uongozi wa Wanawake, manusura wanapata habari muhimu, ushauri nasaha na msaada wa kisheria wakati wowote.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Katika mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu uliomalizika wiki iliyopita baadhi ya wahudhuriaji walikuja na wakalimani wao, kutoka Tanzania Mbunge Nassriya Nassir Ali mwenye ulemavu wa kusikia au Kiziwi aliambatana na mkalimani wake Tusajigwe Ernest. Baada ya mkutano huo Leah Mushi aliketi na Tusajigwe na hapa anaanza kwa kueleza kuhusu taaluma yake. Pia tunakuletea muhtasari wa habari.Kauli za chuki zinaendelea kuhatarisha mshikamano wa jamii na amani duniani, ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akisema mara nyingi ndizo chachu ya vurugu, migogoro na uhalifu mkubwa dhidi ya ubinadamu. Katika ujumbe wake wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kauli za Chuki, leo Juni 18, Guterres amesema makundi kama wanawake, wahamiaji, wakimbizi, watu wenye ulemavu na jamii ya LGBTQIA+ mara nyingi hulengwa na ujumbe wa chuki. “Kauli za chuki ndio hatua ya kwanza katika njia ya kuwanyima watu utu wao, njia ambayo mara nyingi hupelekea vurugu, migogoro na uhalifu wa kutisha.” Pia ameonya kuwa mitandao ya kijamii imeongeza kasi ya kusambaa kwa chuki duniani.Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, MONUSCO, umetangaza kwa masikitiko hii leo kifo cha mfanyakazi wa kampuni iliyokuwa ikitoa huduma kwa ujumbe huo, aliyefariki dunia kutokana na Ebola mjini Bunia. MONUSCO imesema mfanyakazi huyo alikuwa ameacha kufanya kazi na ujumbe huo tangu Mei 22 mwaka huu na hakuwa amefika katika maeneo ya MONUSCO kwa zaidi ya siku 21 kabla ya ugonjwa huo kuthibitishwa. Ujumbe huo umetuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, marafiki na wafanyakazi wenzake na marehemu.Na Shirika la Umoja wa Mataifa la Hali ya Hewa Duniani, WMO, limesema matukio mabaya ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi yaliathiri takriban watu milioni 13 barani Afrika mwaka 2025 na kusababisha vifo zaidi ya watu 3,000. Ripoti mpya ya shirika hilo iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi inaeleza kuwa mafuriko yalikuwa janga lililoripotiwa zaidi, huku yakisababisha hasara kubwa za kiuchumi na kibinadamu. WMO pia imeonya kuwa barafu katika maeneo ya milima ya Afrika, ikiwemo Mlima Kilimanjaro, inaendelea kutoweka kwa kasi, wakati kina cha bahari katika baadhi ya maeneo ya pwani kikipanda kwa kiwango kikubwa kuliko wastani wa dunia. WMO imesisitiza kuwa Afrika bado ina pengo kubwa katika mifumo ya tahadhari za mapema, ingawa maendeleo yanaendelea kufanyika.Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!
Send us Fan MailSerikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) inatarajia kufanya Kongamano la pili la kimataifa la Kiswahili kati ya Julai 4 - 7, 2026, jijini Paris, Ufaransa.Tumezungumza na Bw. Tito Lulandala, Afisa Utamaduni Mwandamizi, kutoka Idara ya Maendeleo ya Utamaduni, na Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Maandalizi ya Kongamano la Pili la Kiswahili la Kimataifa kuhusu maendeleo ya Kiswahili, fursa zilizopo, ajenda muhimu kuelekea kongamano la pili la kimataifa la Kiswahili nchini Ufaransa, pamoja na mafanikio ya kongamano la kwanza lililofanyika Havanna, nchini Kuba, mwaka 2024.Support the showMsemaji Mkuu wa Serikali
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayoturejesha hapa Makao Makuu ya UN kusikia mahojiano maalum na ya kina baina ya Flora Nducha wa Idhaa hii na Mkuu mpya wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa na Uhalifu UNODC. Pia tunakuletea Muhtasari wa habari.Kumekuwepo na imani kwamba ugonjwa wa Ebola si halisi, hali iliyowafanya baadhi ya wananchi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kuzika wapendwa wao waliokufa kwa Ebola bila kufuata hatua za kujikinga dhidi ya maambukizi. Kutafuta suluhu ya changamoto hiyo, Shirika la Afya Duniani WHO kwa kushirikiana na Shirikisho la Kimataifa la chama cha Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, IFRC, wamesikiliza maoni ya jamii kuhusu taratibu za mazishi.Takriban nusu ya watoto wote duniani au watoto bilioni 1.1 sasa wanakabiliwa na angalau hatari tatu za mabadiliko ya tabianchi zinazolingana, zikihatarisha afya zao, elimu, na maisha yao, imesema ripoti iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF.Na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, yuko nchini Haiti kwa ziara maalum ya mshikamano ili kujionea hali halisi ya wananchi walioathiriwa na ghasia na ukosefu wa usalama. Akiwa huko, Guterres anakutana na wananchi, kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Haiti, na kutathmini juhudi za serikali, Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa za kurejesha utulivu nchini humo.Mwenyeji wako ni Feissal Kirwa, karibu!
Licha ya jitihada mbalimbali, bado watu wenye ualbino wanabaguliwa kwenye baadhi ya jamii na hata kuuawa kwa imani za kishirikina.
Licha ya jitihada mbalimbali, bado watu wenye ualbino wanabaguliwa kwenye baadhi ya jamii na hata kuuawa kwa imani za kishirikina.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu CRPD, umehitimishwa jana katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani. Watu wenye ulemavu na wadau mbalimbali wa Serikali na Mashirika yasiyo ya Serikali walikusanyika kutoka kila pembe ya dunia kujadili hatua zilizopigwa katika kipindi cha miaka 20 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu, CRPD. Mmoja wa waliohudhuria ni Bwana Kibaya Laibuta ambaye licha ya kupoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miaka 24 alipokuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi bado alifanikiwa kusonga mbele akamaliza masomo yake ya sheria na masomo mengine ya ngazi za juu na sasa miaka mingi baadaye ni Jaji katika Mahakama ya Rufaa ya Kenya. Siri yake ya mafaniko ndio hasa anaihamasisha kote duniani na anaiweka wazi katika mazungumzo yafuatayo na Anold Kayanda wa Idhaa hii ya Umoja wa Mataifa ili watu wengine wenye ulemavu wafanikiwe kama yeye. Pia tunakuletea muhtasari wa habari zikiwemo za hatua za kupambana na UKIMWI, maambukizi ya ugonjwa wa Ebola hasa kwa watoto DRC, na ujumbe katika siku ya kimataifa ya kupinga utumikishaji wa watoto.Mwenyeji wako ni Rashid Malekela.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina. Kesho kutwa Alhamisi ya Juni 11, macho na masikio yanaelekezwa Mexico, Canada na hapa Marekani kwa ajili ya fainali za kombe la dunia kwa mpira wa miguu, au soka al maarufu kabumbu. Ingawa hivyo zama za sasa za mchezo huo maarufu zaidi duniani zinakumbwa na madhara ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Ongezeko la joto kali linavuruga mechi na kuzua wasiwasi kuhusu mustakabali wa mchezo huo. Ni kwa kuzingatia hilo, Sekretarieti ya Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC inamulika suala hilo na kutoa mapendekezo ya nini kifanyike kwani hivi sasa madhara ya joto kali kwenye kabumbu ni dhahiri. Feissal Kirwa anamulika hilo kupitia video iliyoandaliwa na UNFCCC.Pia tunakuletea muhtasari wa habari na jifunze Kiswahili.Takriban watoto milioni 138 duniani kote bado wako katika ajira za watoto, wakiwemo watoto milioni 54 wanaofanya kazi hatarishi. Hayo yamo katika ripoti mpya iliyotolewa leo na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa ILO. Katika ujumbe wakwe kwenye ripoti hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Gilbert F. Houngbo, ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kubadili hali hii.“Habari njema ni kwamba hadi sasa tuna wagonjwa 19 ambao wamepona, hivyo utambuzi wa mapema na matibabu vinaokoa maisha,” Huyo ni Mkurugenzi wa Operesheni za Tahadhari na Hatua za Dharura za Afya wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani (WHO), Dkt. Abdirahman Mahamud, akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva leo kwa njia ya video kutoka Bunia katika Jimbo la Ituri, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, jimbo ambalo linachangia asilimia 94 ya wagonjwa wote wa Ebola.Mkutano wa 19 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu CRPD, umeanza leo Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York na utaendelea hadi 11 Juni. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “kuadhimisha miaka 20 ya mkataba huo na kuimarisha utekelezaji wake katika dunia inayobadilika.” Washiriki wanajadili namna ya kutokomeza ukandamizaji, ukatili na manyanyaso dhidi ya watu wenye ulemavu, kuimarisha mifumo ya huduma na msaada, pamoja na kuongeza ushiriki na uwakilishi wao katika maisha ya kisiasa na umma.Katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo Dkt Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana na matumizi ya neno "MKWARUZO."Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Bahari duniani zinakabiliwa na changamoto kubwa zinazotishia afya ya mazingira na ustawi wa binadamu, ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres na kutoa wito wa hatua za haraka na za pamoja kukabiliana na hali hiyo. Akizungumza kwa njia ya video katika ujumbe wake wa Siku ya Kimataifa ya Bahari inayoadhimishwa kila mwaka Juni 8, Bwana Guterres amesema bahari ni msingi wa maisha na maendeleo duniani, lakini zimekuwa zikikabiliwa na shinikizo linalozidi uwezo wake wa kustahimili."Bahari inaongoza tabianchi yetu, inalinda mifumo ya ikolojia na uchumi, na inalisha mabilioni ya watu duniani," anasema Guterres na kuongeza kuwa, "bahari ipo kwenye zahma kubwa na tunaishinikiza kupita uwezo wake."Guterres amerejelea Ripoti ya Tatu ya Tathmini ya Bahari Duniani iliyozinduliwa leo, ambayo imebainisha kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, uvuvi uliokithiri, kupotea kwa bionuwai na uchafuzi wa bahari.Katibu Mkuu Guterres amesisitiza akisema, "hatuwezi kuendelea kuichukulia bahari kama kitu kisicho na ukomo," akihimiza kujengwa kwa uhusiano mpya na bahari unaozingatia sayansi, unaoongozwa na sheria za kimataifa na unaojengwa juu ya wajibu wa pamoja wa mataifa, sekta mbalimbali na vizazi vyote.Ametaja mafanikio ya Mkutano wa Tatu wa Bahari wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mwaka jana pamoja na kuanza kutekelezwa kwa Makubaliano ya Baiyonuai ya Bahari katika maeneo yaliyo nje ya mamlaka ya kitaifa mwaka huu kama ushahidi kwamba ushirikiano wa kimataifa unaweza kuleta matokeo.Anasema, "hatua za pamoja za kimataifa zinawezekana na ni za lazima."Katika hitimisho la ujumbe wake wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewataka viongozi wa dunia, sekta binafsi na wananchi kuchukua hatua kwa haraka ili kulinda bahari kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.Anasema, "katika Siku hii ya Kimataifa ya Bahari, hebu tuchukue hatua kwa nia thabiti na kutatua mahitaji ya wakati huu."Hakika yanayosemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa yanaendana na aliyoyasema Mwenyekiti aliyechaguliwa wa ya Tume ya Kiserikali ya Bahari ya UNESCO (IOC) kwa Afrika na Nchi za Visiwa vinavyokaribia bara la Afrika (IOCAFRICA) Hellen Gichuhi alipozungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa.
Send us Fan MailMkutano na Waandishi wa Habari kuhusu ziara ya Kitaifa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, tarehe 7 Juni, 2026.Support the showIdara ya Habari MAELEZO
Msikilizaji Sekta ya maua nchini Kenya, ambayo kwa muda mrefu imekuwa miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi na chanzo kikuu cha mapato ya fedha za kigeni, ikiingizia nchi zaidi ya dola bilioni moja za Marekani kila mwaka, sasa inakabiliwa na changamoto zinazotia wasiwasi kuhusu mustakabali wake.
Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC iliyoko mjini The Hague, Uholanzi imesema mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda Felicien Kabuga amefariki dunia.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Tanzania kwa Chama cha Wanawake Majaji, (TAWJA) ambacho kimetambua pengo la upatikanaji wa haki hususan kwa wanawake na wasichana na tunasikia hatua zinazochukuliwa kuziba pengo hilo kutoka kwa mwenyekiti wake, Barke Sehel ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa. Pia tunakuletea mhtasari wa habari kama zifuatazo..Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametangazwa kwa mara nyingine kugundulika kwa virusi vya ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Congo DRC katika jimbo la Ituri lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Hii ni mara ya 17 kwa mlipuko wa Ebola kutokea DRC tangu kugunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976. Wagonjwa 13 vimethibitishwa na taasisi ya utafiti wa tiba ya INRB mjini Kinshasa. Dkt. Tedros amesema tayari wametuma wataalamu, vifaa tiba na ameruhusu kutolewa kwa dola laki tano kusaidia kudhibiti mlipuko huo na kuwahudumia wagonjwa.Hali ya kibinadamu nchini Somalia inazidi kuwa mbaya kuliko ilivyotarajiwa hapo awali. Akuzungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi afisa mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia George Conway amesema “Hivi sasa Takriban watu milioni sita nchini Somalia amba ni sawa na mtu mmoja kati ya sita anakabiliwa na njaa ikimaanisha kuwa anaruka muda wa kula chakula, au anaenda siku kadhaa bila chakula cha kutosha. Watoto ndio wanaolipa gharama kubwa zaidi. Karibu watoto milioni mbili wana utapiamlo mkali, ikimaanisha kuwa wana utapiamlo mbaya na dhaifu kimwili, na hivyo kuwaweka katika hatari kubwa ya kuugua au kufa.”.Na leo ni siku ya Kimataifa ya Familia, Umoja wa Mataifa unasema maadhimisho ya mwaka huu yanaangazia jinsi umaskini, ukosefu wa huduma muhimu na msaada mdogo wa malezi vinavyoathiri familia na kudhoofisha maendeleo bora ya watoto. Maadhimisho ya mwaka huu yanaweka mkazo maalum kwenye hatua jumuishi za ulinzi wa kijamii kama vile ruzuku za watoto, likizo za uzazi zenye malipo, huduma nafuu za malezi ya watoto na elimu ya awali kwa watoto wadogo.Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Hii leo jaridani tunaangazia maambukizi wa Hantavirus, juhudi za kutokomeza Adhabu za Viboko shuleni nchini Tanzania, na ujumbe wa Profesa Hamisi Masanja Malebo kuhusu haki za watu wa asili.Imethibitishwa kuwa abiria mwingine aliyekuwa kwenye meli ya kitalii iliyohusishwa na mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Hanta au Hantavirus ameambukizwa ugonjwa huo, ugonjwa ambao tayari umeua watu watatu waliokuwa ndani ya meli na kusababisha tahadhari ya kimataifa iliyoratibiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) la Umoja wa Mataifa.Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Adhabu za Viboko huadhimishwa Aprili 30 ya kila mwaka, na mwaka huu katika maadhimisho ya siku hiyo wiki iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF, nchini Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa haki za binadamu na elimu lilizindua kampeni iitwayo ‘No Collabo' iliyolenga kukomesha adhabu ya viboko kwa mtindo ambao walimu zaidi ya mmoja humchapa mwanafunzi viboko kwa wakati mmoja. Rashid Malekela amezungumza na wazazi mkoani Mwanza Kaskazini Magharibi mwa nchini hiyo kupata maoni yao.Siku tano zilizopita Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Watu wa Asili (UNPFII) limefunga pazia hapa katika makao ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani baada ya majadiliano ya takribani wiki mbili ya wadau kutoka nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu sera, mafanikio na kukabiliana na changamoto mbalimbali katika kuhudumia wananchi wao ikiwemo jamii za watu wa asili. Kwa upande wa Tanzania, mmoja wa walioshiriki ni Katibu Mtendaji wa Tume ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO ya Taifa la Tanzania, Profesa Hamisi Masanja Malebo.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Siku ya Kimataifa ya Kukomesha Adhabu za Viboko huadhimishwa Aprili 30 ya kila mwaka, na mwaka huu katika maadhimisho ya siku hiyo wiki iliyopita, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto, UNICEF, nchini Tanzania kwa kushirikiana na wadauwa haki za binadamu na elimu lilizindua kampeni iitwayo ‘No Collabo' iliyolenga kukomesha adhabu ya viboko kwa mtindo ambao walimu zaidi ya mmoja humchapa mwanafunzi viboko kwa wakati mmoja. Rashid Malekela amezungumza na wazazi mkoani Mwanza Kaskazini Magharibi mwa nchini hiyo kupata maoni yao.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Kenya kumsikia kijana ambaye baada ya kukosa ajira, alichagua kujiajiri kwa kuuza miwa na juisi yake, hatua iliyomwezesha kujipatia kipato na kupambana na umaskini. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na jifunze KiswahiliShirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO limesema abiria na wahudumu waliokumbwa na mlipuko wa hantavirus katika meli ya utalii iliyokuwa Bahari ya Atlantiki huenda waliambukizwa virusi hivyo kabla ya kupanda meli hiyo, ingawa maambukizi miongoni mwa watu ndani ya meli hayawezi kuondolewa kabisa licha ya kuwa ni nadra. Watu saba kati ya abiria na wahudumu 147 wameugua huku wengine wakifariki dunia.Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO, linaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Usafi wa Mikono hii leo 2026 chini ya kauli mbiu “Hatua Zinazookoa Maisha,” kikisisitiza haja ya kuimarisha uzuiaji wa maambukizi katika vituo vya afya. WHO inaonya kuwa maambukizi yanayotokana na huduma za afya bado ni tishio la kila siku katika hospitali na kliniki, yakichangia usugu wa dawa za viua vijasumu au antibiotiki, ongezeko la gharama, pamoja na vifo vinavyoweza kuzuilika.Leo Mei 5 ni Siku ya Kimataifa ya Wakunga, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na Afya ya Uzazi, UNFPA, likisema wakunga ni wadau muhimu katika huduma za afya ya uzazi duniani kote. Shirika hilo linasema dunia inahitaji wakunga milioni moja zaidi ili kuboresha huduma za afya na kuokoa maisha ya wanawake na watoto wachanga. Kwa mujibu wa UNFPA, wakunga wanahakikisha ujauzito na kujifungua salama, huku pia wakisaidia kupunguza mimba zisizotarajiwa, maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto na upasuaji usio wa lazima wakati wa kujifungua.”Katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali “Kwendako mema hurudi mema."Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!
Mapambano ya kimataifa dhidi ya homa ya ini ya virusi aina ya B na C yanaanza kuonesha mafanikio, imesema ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, iliyotolewa Aprili 28, 2026. Ripoti hiyo, imezinduliwa wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Homa ya Ini mjini Bangkok, Thailand, mkutano ulioingia leo siku ya pili na unakunya jamvi kesho. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.
Hii leo jaridani tunaangazia mkutano wa Kikanda wa Afya Barani Afrika wa mwaka 2026 unaokunja jamvi leeo, Mapambano ya kimataifa dhidi ya homa ya ini ya virusi aina ya B na C, na maombelezo ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda.Mkutano wa Kikanda wa Afya Barani Afrika wa mwaka 2026 “World Health Summit 2026” umehitimishwa leo mjini Nairobi nchini Kenya, ukiwaleta pamoja zaidi ya wajumbe elfu moja kutoka takribani nchi 50 kujadili namna ya kuimarisha mifumo ya afya barani Afrika na duniani.Mapambano ya kimataifa dhidi ya homa ya ini ya virusi aina ya B na C yanaanza kuonesha mafanikio, imesema ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, iliyotolewa Aprili 28, 2026. Ripoti hiyo, imezinduliwa wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Homa ya Ini mjini Bangkok, Thailand, mkutano ulioingia leo siku ya pili na unakunya jamvi kesho.Siku 100 za maombelezo ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari ya Rwanda dhidi ya Watutsi yaliyofanyika yapata miaka 32 iliyopita zikiendelea . Leo tunakupeleka mjini Kigali nchini Rwanda kwenye Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini humo kwake Eugene Uwimana afisa habari wa ofisi hiyo ili kupata simulizi ya kijana anayemuenzi baba yake aliyekuwa mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambaye aliuawa katika mauaji hayo ya kimbari. Jina la baba huyo ni Emmanuel Turatsinze.”Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Tweet URLSuala hilo la mchango wa manusura katika kuepusha mauaji kama hayo hayajirudii tena, nililimulika wakati wa mazungumzo yangu ya hivi karibuni na Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Martin Ngoga ambaye bila kumung'unya maneno alinieleza kuwa, “ wanamchango mkubwa sana kwa sababu kwanza wanapambana na hali ambayo katika hali ya kawaida ya ubinadamu ni ngumu. Chukulia mfano wetu sisi Rwanda walionusurika mauaji na waliotekeleza wanaishi pamoja kwa sababu Rwanda hakuna mgawanyiko wa kikabila wa kwamba kuna baadhi wanaishi mkoa fulani. Wanaishi pamoja katika vijiji hivyo, hivyo wanaenda shule hizo hizo wanaenda hospitali pamoja na wanaishi pamoja. Kwa mtu ambaye amepoteza familia yake nzima na anawajua wauaji walioua familia yake na anaendelea kuishi nao kijijini, ni hali ambayo kwa kweli katika akili ya kawaida unaweza usielewe lakini imetokea Rwanda.”Mwaka huu wa 2026 ni miaka 32 tangu kutokea kwa mauaji hayo ya kimbari. Hivyo Balozi Ngoga ambaye aliwahi kuwa Mwakilishi wa Rwanda kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu uliotokea Rwanda (ICTR) akafafanua kwamba, “Baadhi ambao walikuwa ni wadogo wakati huo ambao sasa ni watu wazima, wanaandika hata vitabu kueleza nini kilitokea. Lakini wamekubali kuingia katika mchakato wa maridhiano, kujenga upya taifa la Rwanda."Akaongeza kuwa, "na kama ambavyo aliwahi kusema kiongozi wetu Rais Paul Kagame wakati fulani kwamba wao walionusurika ndio wanacho cha kutoa. Wao ndio wanaombwa watoe zaidi katika kuchangia juhudi za kulijenga upya taifa kwa sababu muuaji unaenda kumuomba nini. Tunashukuru kwamba wamekubaliana na hiyo, hali ambayo katika mazingira ya kawaida ya kibinadamu ni ngumu sana. Lakini kwa miaka yote hii tunakwenda.”
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambapo juzi Jumanne na jana Jumatano wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa walipata fursa kunadi serra zao mbele ya nchi wanachama kwenye Baraza Kuu wakiwemo wawakilishi wa asasi za kiraia walioweza kuwauliza maswali. Miongoni mwa wawakilishi hao ni Irene Kitoti, Mwanzilishi na mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Genesis For Children Organization ya nchini Tanzania aliyezungumza na Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili. Pia tunakuletea muhtasari wa habari kama zifuatazo.Kutokana na mafanikio ya kihistoria kwa afya ya umma ya eneo la Karibe, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO limeipongeza nchi ya Bahamas kwa kuwa taifa la hivi karibuni zaidi katika ukanda huo wa Karibe kuthibitishwa kuwa limekomesha maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus, kupitia taarifa ya shirika hilo ameipongeza Bahamas kwa mafanikio haya makubwa, yanayoimarisha miaka ya dhamira ya kisiasa na kujitolea kwa wahudumu wa afya.Ikiwa leo imetimia miaka 15 tangu kuanza maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Teknolojia ya Habari na Mawasilino, TEHAMA au ICT, Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU), Doreen Bogdan-Martin katika ujumbe wake mahususi wa maadhimisho ya mwaka huu amesema, “kwa sasa tunaishi katika kipindi cha mabadiliko makubwa na ya kusisimua zaidi ya kiteknolojia katika historia ya binadamu lakini vilevile kwa sasa fursa zinazohusiana na mabadiliko haya ya kiteknolojia hazimfikii kila mtu kwa usawa”.Mgogoro wa usafirishaji katika Mlango Bahari wa Hormuz uliosababishwa na vita vya Mashariki ya Kati umefichua tishio jipya: upungufu wa madini ya kimkakati yanayoendesha uchumi duniani kote na sasa nchi huenda zitaanza kuhaha kuyapata. Katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Geneva Uswisi, Dario Liguti, Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Endelevu cha Tume ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ulaya, UNICE amesema, “hatua ya kwanza, mbali na ongezeko la bei bila shaka, itakuwa viwanda kupunguza matumizi yake yake ya madini ya kimkakati na hivyo kupunguza uzalishaji… iwe ni paneli za sola, sumaku, betri na kadhalika, katika siku zijazo.”Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "KUPARAMA"Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Hii leo jaridani tunaangazia juhudi za Umoja wa Mataifa za kutafuta suluhu ya vita nchini Sudan pamoja na simulizi za wakimbizi ikiwa leo ni miaka mitatu kamili tangu vita vilipoanza nchini humo, na miundombinu na ujenzi wenye mnepo nchini Tanzania.Wakati vita nchini Sudan ikiingia mwaka wa nne tangu kuvuka kwa mapigano baina ya jeshi la Sudan na kikosi vya msaada wa haraka RSF, hii leo huko Berlin nchini Ujerumani unafanyika mkutano wa Kimataifa ukilenga kurejesha mgogoro wa Sudan katika ajenda ya juu ya kidiplomasia duniani.Leo ni miaka mitatu kamili tangu vita vilipoanza nchini Sudan 15 Aprili 2023, mgogoro ambao umegeuka kuwa moja ya majanga makubwa zaidi ya kibinadamu duniani. Mamilioni ya watu wamekwama katikati ya mapigano, kuwa wakimbizi wa ndani na nje, njaa na ukosefu wa makazi, huku mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yakionya kuwa mateso yanaendelea kuongezeka kila uchao.Katika kuunga mkono lengo namba 9 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs kuhusu miundombinu na ujenzi wenye mnepo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo, UNDP nchini Tanzania, limeingia makubaliano ya kimkakati na Taasisi ya wanawake wasanifu Majenzi, TAWAH, kwa ajili ya kuboresha sekta ya ujenzi.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Wakati vita nchini Sudan ikiingia mwaka wa nne tangu kuvuka kwa mapigano baina ya jeshi la Sudan na kikosi vya msaada wa haraka RSF, hii leo huko Berlin nchini Ujerumani unafanyika mkutano wa Kimataifa ukilenga kurejesha mgogoro wa Sudan katika ajenda ya juu ya kidiplomasia duniani. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Leah Mush
Jaridani tunakuletea mada kwa kina hii leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya Tafakari kuhusu Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda. Na katika kupata tafakari hiyo Assumpta Massoi wa Idhaa hii amezungumza na Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Martin Ngoga. Balozi Ngoga anaanza kwa kuelezea mawanda ya mauaji hayo.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezisihi pande zinazo hasimiana katika mgogoro wa Mashariki ya Kati kuacha kushambulia miundombinu kwani ni kinyume cha sheria za Kimataifa. Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano wa Umoja wa Mataifa wa mjini Geneva Uswisi Alessandra Vellucci amewaambia waandishi wa habari kuwa “Umoja wa Mataifa ulishtushwa na matamshi yaliyoonekana katika chapisho la mitandao ya kijamii ambayo yalitishia mashambulizi ya Marekani dhidi ya mitambo ya kuzalisha umeme, madaraja na miundombinu mingine, iwapo Iran haitakubali makubaliano. Katibu Mkuu amezitaka pande zote kuzingatia wajibu wao kuhusu mwenendo wa mgogoro huo. Miundombinu ya kiraia, ikiwa ni pamoja na miundombinu ya nishati, haiwezi kushambuliwa, hata kama miundombinu maalum ya kiraia ingekuwa ikitumika kwa lengo la kijeshi. Umefika wakati wa pande husika kukomesha mzozo huu.”Leo ikiwa ni siku ya afya duniani, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuimarisha ushirikiano na kuunga mkono sayansi kama msingi wa kuboresha afya ya binadamu. WHO imesema sayansi inapaswa kuwa msingi wa maamuzi yote ya afya katika ngazi za kitaifa na kimataifa na kutoa wito kwa serikali, taasisi na watu binafsi kuongeza ushirikiano ili kuhakikisha sera na hatua za afya zinazingatia ushahidi wa kisayansi. Kauli mbiu ya siku hii ni “Pamoja kwa Afya, Simama na Sayansi.”Na hii leo dunia inakumbuka mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 dhidi ya watutsi nchini Rwanda, matukio ya kumbukizi yamefanyika kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa huko Nairobi, Kenya, Geneva nchini Uswisi na hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwenye ukumbi wa Baraza Kuu. Matukio yamehudhuriwa na manusura, viongozi wa Umoja wa Mataifa na Rwanda na mashirika ya kiraia ujumbe mkuu ukiwa hatua zichukuliwe kuhakikisha mauaji ya kimbari hayatokei tena.Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!
Hii leo jaridani tunaangazia migogoro yanayoendelea Mashariki ya Kati, ujumbe wa Katibu Mkuu leo dunia ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya kutozalisha taka, na kampeni ya upatiaji mifugo dawa za minyoo na udhibiti wa wadudu waenezao magonjwa Isiolo nchini Kenya.Vita vya Mashariki ya Kati vimeingia mwezi wa pili huku ghasia zikiongezeka katika maeneo kadhaa, ikiwemo Lebanon, Iran na Ghuba. Mlinzi wa amani wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon UNIFIL ameuawa baada ya kombora kulipuka katika kituo cha Umoja wa Mataifa karibu na Adchit Al Qusayr, huku mwingine akiwa mahtuti hospital.Wakati hii leo dunia ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya kutozalisha taka, Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa kila mtu kujifunza upya yamna ya kufanya manunuzi ya vitu na mapishi ambayo hayatasababisha umwagaji wa chakula ili kunusuru mifumo ya ikolojia na afya ya binadamu.Nchini Kenya katika kaunti za Isiolo, Garissa, Samburu na Mto Tana, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO limeendesha kampeni ya upatiaji mifugo dawa za minyoo na udhibiti wa wadudu waenezao magonjwa, sambamba na kupatia wananchi fedha taslimu bila masharti kama mojawapo ya kujengea jamii mnepo wakati wa ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Wakati hii leo dunia ikiadhimisha siku ya Kimataifa ya kutozalisha taka, Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa kila mtu kujifunza upya yamna ya kufanya manunuzi ya vitu na mapishi ambayo hayatasababisha umwagaji wa chakula ili kunusuru mifumo ya ikolojia na afya ya binadamu. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi.
Shirika la Nishati la Kimataifa linaonya viongozi wa dunia huenda hawathamini, kina cha mgogoro wa nishati unaokaribia, huku vita vya Marekani na Iran vikiendelea.
Umoja wa Mataifa leo umekuwa na tukio la kumbukizi ya siku ya kimataifa ya kukumbuka waathiriwa wa biashara ya utumwa kupitia bahari ya Atlanitiki ambapo nchi 123 wanachama wa Umoja huo wamepitisha azimio lililoandaliwa na mataifa 58 kutambua usafirishaji wa watu wa kiafrika na utumwa kwa misingi ya rangi ya waafrika kuwa uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu. Nchi hizo 123 ni pamoja na zile wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilhali nchi 3 zilizopinga azimio ni Marekani, Israeli na Argentina. Nchi 52 hazikuonesha msimamo wowote. Mwakilishi wa Marekani akizungumza baada ya kupiga kura ya kupinga azimio hilo amesema, "tunalaani makosa yoyote yaliyofanyika kuhusiana na utumwa kuvuka bahari ya Atlantiki, jangwa la Sahara na kwingineko, lakini tumepinga azimio kwa sababu hatuoni msingi wa kulipatia kiwango cha juu hivyo cha hadhi tukio hilo. Na zaidi ya yote kama ni fidia, fidia hiyo atalipwa nani,?" amehoji.Rais wa Ghana aliwasilisha rasimu ya azimio mbele ya Baraza KuuUN/Manuel EliasRais John Mahama wa Ghana akihutubia Baraza Kuu wakati wa siku ya Kimataifa ya Kumbukizi ya Waathirika wa Utumwa na Biashara ya Watumwa kupitia bahari ya Atlantiki.Rasimu ya azimio hilo iliwasilishwa na Rais wa Ghana John Mahama ambaye ni Balozi wa Muungano wa Afrika wa Kuendeleza Hali ya Haki na Fidia. Azimio hilo namba A/80/L.48 limepatiwa jina kutambua usafirishaji wa watu waliokuwa watumwa kutoka Afrika na utumwa kwa msingi wa rangi ya watu wa kiafrika kama mojawapo ya uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu. Azimio hilo lililoandaliwa na mataifa 58 yakiwemo mataifa ya Afrika Mashariki, lina vipengele 16 vya utekelezaji ikiwemo kutambua usafirishaji huo wa watumwa kutoka Afrika kuwa uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu, kurejeshwa kwa mali za kitamaduni kutoka Afrika na zaidi ya yote kulipwa fidia.Kauli ya Rais wa Baraza KuuTukio la kumbukizi lilianza kwa Annalena Baerbock Rais wa Baraza Kuu kuitisha kikao na kisha kuelekea kwenye mimbari kutoa hotuba yake akirejelea simulizi ya mtumwa Oladuk Ekwano kutoka Nigeria ya sasa akielezea machungu ya safari ndani ya meli iliyowabeba.UN/Manuel EliasRais wa Baraza Kuu la UN Annalena Baerbock akitoa hotuba katika tukio la siku ya Kimataifa ya Kumbukizi ya Waathirika wa Utumwa na Biashara ya Watumwa kupitia bahari ya Atlantiki.Anasema Makumi ya mamilioni ya wengine kama Egvano walinyang'anywa kutoka kwa familia zao, nchi zao na tamaduni zao, wakafanywa watumwa na kupelekwa kufanya kazi katika nchi za kigeni—kwenye mashamba ya pamba hapa Marekani, na kwenye mashamba ya miwa na kahawa katika makoloni yaliyodhibitiwa na Ulaya. Katika maeneo ambayo leo yanajulikana kama Brazili, Barbados, Jamaica, na maeneo mengine mengi. Wote wakiwa mbali na nyumbani, mbali na familia, mbali na maisha yao.Tunatambua nchi zinazoomba radhi lakini hatua zaidi zahitajikaKwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amerejelea mateso waliyopata mamilioni ya waafrika waliotekwa nyara na kusafirishwa katika hali dhalili na kugeuzwa watumwa barani Amerika. Amesema kumbukumbu pekee haitoshi.Amebainisha kuwa mfumo huo haukuwa tu ukatili wa zamani bali pia ulikuwa msingi wa miundo ya uchumi wa dunia ambayo madhara yake yanaendelea hadi leo katika mfumo wa ubaguzi wa rangi wa kimfumo na ukosefu wa usawa.UN/Manuel EliasKatibu Mkuu António Guterres akitoa hotuba katika tukio la siku ya Kimataifa ya Kumbukizi ya Waathirika wa Utumwa na Biashara ya Watumwa kupitia bahari ya Atlantiki.Hotuba hiyo imesisitiza kuwa kumbukumbu pekee haitoshi. Badala yake, nchi lazima zikabiliane na dhuluma za muda mrefu zinazoendelea kuwaathiri watu wenye asili ya Kiafrika. “Kiini cha juhudi hizo, alisema, ni kutafuta ukweli, haki, na marekebisho, ikiwa ni pamoja na mijadala yenye maana na hatua kuhusu fidia,” amesema Katibu Mkuu. Guterres anasema, “Ndiyo maana Muongo wa Pili wa Kimataifa kwa Watu wenye Asili ya Kiafrika na Muongo wa Fidia wa Muungano wa…
Nchini Tanzania kunafanyika mafunzo kwa maafisa wa misitu yenye lengo la kulinda misitu, mafunzo yanayotekelezwa kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, (FAO) na serikali ya Tanzania kwa ufadhili wa Muungano wa Ulaya (EU) kupitia mradi wa CookFund.Tweet URLMratibu wa Mradi kutoka FAO Diomedes Kalisa akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi Msaidizi wa FAO Tanzania, Charles Tulahi, amesema “mafunzo haya yanakuja wakati muafaka kwani maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Misitu yalibeba kaulimbiu, “Misitu na Uchumi.”Amesisitiza kuwa Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 48 za misitu ambayo inachangia zaidi ya asilimia 90 ya mahitaji ya nishati ya kaya kupitia nishati ya biomasi. Uvunaji haramu wa misitu ni kikwazo“Changamoto za uvunaji haramu, uzalishaji usio endelevu na udhaifu wa utekelezaji wa sheria zinalengwa kupitia mafunzo hayo yatakayojikita katika maeneo matano ya kipaumbele.” Amesema.Ametaja maeneo hayo kuwa ni usimamizi wa watoa taarifa, mbinu za ufuatiliaji, matumizi ya teknolojia, tafsiri ya sheria za misitu na marekebisho yake ya 2025, pamoja na ujuzi wa uchunguzi na utekelezaji wa sheria. Lengo namba 15 la SDG linavyomulika misituLengo la 15 la Maendeleo Endelevu (SDG15) kuhusu “Uhai juu ya ardhi,” linazingatia kulinda, kurejesha, na kuendeleza usimamizi endelevu wa misitu, kusitisha ukataji miti hovyo, na kurejesha uharibifu wa ardhi ifikapo mwaka 2030. Lengo hili linaelekeza moja kwa moja kusitisha upotevu wa bayonuai na kuimarisha mchango wa misitu katika kunasa hewa ya ukaa, hivyo kusaidia juhudi za kimataifa za kupambana na mabadiliko ya tabianchi.Manufaa ya mafunzoMkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Misitu katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Seleboni Mushi, amesema mafunzo hayo yanayosimamiwa na FAO yanalenga kujenga uwezo wa wakaguzi na wapelelezi wa TFS kutoka maeneo mbalimbali ya nchi katika kudhibiti changamoto zinazoikabili misitu ikiwemo ukataji miti haramu, uvamizi wa misitu, kilimo haramu na uchomaji moto kwenye maeneo ya misitu. “Misitu ni urithi wa taifa na ni muhimu kuilinda kwa ajili ya vizazi vijavyo,” amesema Afisa huyo na hivyo “mafunzo haya yatawapa washiriki maarifa mapya katika maeneo muhimu kama vile usimamizi wa watoa taarifa, mbinu za ufuatiliaji, matumizi ya teknolojia ya kisasa katika ulinzi wa misitu, tafsiri ya sheria na kanuni za misitu, pamoja na ujuzi wa uchunguzi na utekelezaji wa sheria.” Amesisitiza kuwa mafunzo haya ni fursa kwa washiriki kujenga mitandao imara ya kitaalamu itakayosaidia ushirikiano na ubadilishanaji wa taarifa katika kuhakikisha misitu ya Tanzania inaendelea kutoa manufaa kwa wote,” amesema Bwana Mushi.
Hii leo jaridani ni:Muhtasari;Mada kwa Kina na Jifunze lugha ya Kiswahili. Jarida leo linawasilishwa na Rashid Maleka kutoka Mwanza nchini Tanzania.Muhtasari wa Jarida:dadi ya vifo kutokana na shambulio dhidi ya hospitali moja huko Darfur, Sudan, Ijumaa iliyopita imeongezeka zaidi,Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi,UNHCR limetoa wito wa msaada wa haraka wa kimataifa ili kuhakikisha urejeaji wa wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, DRC wanaorejea kutoka Burundi unafanyika katika mazingira ya usalama na utu.Leo katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kifua Kikuu (TB) inayoadhimishwa tarehe 24 mwezi Machi kila mwaka, WHO inazihimiza nchi kuharakisha hatua za kumaliza TB na kupanua upatikanaji wa huduma za kuokoa maisha kwa kutumia ubunifu mpya ikiwemo vipimo vinavyotumia mate.Mada kwa kina: Leah Mushi amezungumza na Naibu Mrajisi wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Tanzania Chausiku Kafuti Kuya kando ya CSW70 iliyokunja jamvi wiki iliyopita hapa New York, Marekani. Jifunze lugha ya Kiswahili: Methali - “ATETEAYE MTUKU NI TANGUKO LA BURE”Karibu!
Katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Furaha ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 20 Machi, wakazi wa kata ya Luchelele, jijini Mwanza, kaskazini-magharibi mwa Tanzania, wameeleza maana ya furaha katika maisha yao ya kila siku, ambapo kwa wengi, furaha haitokani na anasa, bali inajengwa na afya njema, upendo wa familia, na uwezo wa kuitunza familia hiyo kwa mahitaji ya msingi. Wakizungumza na Rashid Malekela wa Idhaa hii, wanawake wa eneo hilo wameeleza kuwa furaha kwao ni chanzo kikuu cha amani ya moyo. Rehema James amesema kuwa furaha yake kubwa ni kuamka salama, wakati Regina Emmanuel amegusia uhusiano wa mzazi na mtoto kama nguzo ya furaha yake, "Furaha yangu kuu inatokana na mama yangu kuwa hai na mwenye afya."Faida Anthony, mmoja wa wakazi wa eneo hilo, amefafanua kuwa kwake furaha ni matokeo ya jitihada za kutafuta riziki akisema,"Furaha ni kutafuta fedha, mboga, na kuijali familia yangu."Mitandao ya kijamii na changamoto za furahaLicha ya umuhimu wa afya na familia, matumizi ya teknolojia yameanza kuathiri jinsi watu wanavyopata au kupoteza furaha katika ulimwengu wa sasa. Duch Sababu, ambaye ni Afisa Usafirishaji maarufu ‘bodaboda', amebainisha kuwa mitandao ya kijamii ina sura mbili; inaweza kuleta kicheko kupitia maudhui ya ucheshi au kuleta huzuni kulingana na kile mtu anachokiona, huku akitoa angalizo kwa watumiaji wa mitandao,"Furaha ni afya njema, lakini pia mitandao inaweza kuleta furaha kupitia vichekesho au huzuni kulingana na kile unachokiona."Wito wa Umoja wa MataifaMwaka huu, Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa furaha ya kweli kwa binadamu wote itafikiwa endapo kutakuwa na usawa, haki, na ulinzi wa mazingira kulingana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Ili kufikia malengo hayo duniani, kuna uhitaji wa kuendelea kuimarisha huduma za kijamii zinazogusa maisha ya watu wa hali ya chini moja kwa moja.Kwa vijana, wameshauriwa kutumia muda wao kwenye mitandao ya kijamii kutafuta mambo yatakayowajenga kifikra na kuwapa furaha badala ya mambo yanayoweza kuwaharibia amani yao ya moyo.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina leo baada ya takribani wiki mbili mkutano wa 70 wa CSW70 unakunja jamvi. Maudhui yalikuwa kuendeleza Haki, Sheria na Kuchagiza Hatua kwa ajili ya wanawake na wasichana, na sasa washiriki wanaeleza Idhaa hii wanachoondoka nacho.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo akizungumza na waandishi wa habari Mjini Brussels Ubelgiji kuhusu kinachoendelea Mashariki ya Kati akiwa a na Rais wa Baraza la Muungano wa Ulaya António Costa, ametoa ujumbe mahsusi kwa wahusika wakuu wa mzozo huo. Amesema “Kwanza kwa Marekani na Israel, ni wakati muafaka kumaliza vita hivi ambavyo viko hatarini kutodhibitiwa kabisa, vikisababisha mateso makubwa kwa raia, na athari zake zinaenea katika uchumi wa dunia kwa kiwango cha kutisha, zikiwa na uwezekano wa kusababisha madhara makubwa zaidi hasa kwa nchi zenye maendeleo duni”Kisha ujumbe wake wa pili ni “Kwa Iran, acheni kushambulia majirani zenu. Hawakuwa sehemu ya mgogoro huu. Baraza la Usalama limelaani mashambulizi haya na kuamuru yasitishwe, pamoja na kuagiza kufunguliwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz.”Na kuelekea Siku ya Kimataifa ya Furaha hapo Kesho Machi 20 raia Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, eneo lililoghubikwa na mizozo ya silaha wanaeleza furaha kwao inamaanisha nini.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Wanawake kote duniani walijitokeza mitaani kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wakitaka kukomeshwa kwa ukosefu wa usawa na ubaguzi.
Alya Abu Shawish, mwanamke aliyeko mstari wa mbele kuondoa hatari ya mabomu Gaza (OVERNIGHT)Hii leo pia hapa katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, imefanyika hafla ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake ambayo duniani kote iliadhimishwa jana Jumapili. Katika muktadha huo huo ninamualika Anold Kayanda atupeleke Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel kumwangazia Alya Abu Shawish, Mwanamke anayefanya kazi katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kutoa huduma ya kutegua mabomu, UNMASakisaidia kuwaweka salama wenzake katika mojawapo ya mazingira hatari zaidi duniani. Karibu Anold.(Taarifa ya Anold)Asante Flora,Hakika Gaza ni moja ya mazingira hatari duniani kwa sasa. Alya Abu Shawish anaposhuka kwenye gari kabla ya kuingia ofis iza UNMAS zilizoko Deir al-Balah katikatimwa Gaza, anavaa jaketi la kujikinga na risasi.Ndani ya ofisi amesimama mbele ya ramani ya kidijitali, akifuatilia mienendo ya timu za wafanyakazi walioko mitaani zilizosambazwa kote katika ukanda huo wa Gaza ili kufanya kazi za kuondoa mabaki ya vilipuzi vya vita katika eneo hilo.Baada ya mipango yote kukamilika ofisini, sasa Alya Abu anaendesha gari akiwa na wenzake kuelekea kazini nje ya ofisi. Anaeleza akisema,(Sauti ya Alya Abu Shawish) – Sharon“Kazi yangu kama mwanamke katika eneo hili inaonyesha kwamba wanawake wanaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuhakikisha usalama na kuleta mabadiliko yanayoonekana, hata katika mazingira hatari na yenye changamoto kubwa zaidi katika Ukanda wa Gaza.”Alya Abu Shawish anaonekana na wenzake mitaani wakifanya kazi. Watoto wanafuata, kwa vyovyote wakitambua kazi muhimu inayofanywa na UNMAS kufanya mazingira yawe salama dhidi ya vilipuzi.Hata hivyo, nyuma ya dhamira hii ya kitaaluma kuna hadithi binafsi inaloakisi hali halisi ya maelfu ya wanawake huko Gaza.(Sauti ya Alya Abu Shawish) – Sharon“Kama mwanamke na mama, nimepitia changamoto nyingi ambazo wanawake wa Kipalestina huko Gaza hukabiliana nazo wakati wa vita hofu, kuhama makazi, uhaba wa mahitaji muhimu, na hali ya kutokuwa na uhakika kila wakati. Kama wanawake wengi hapa, nimelazimika kuilinda familia yangu huku nikikabiliana na hali hizi ngumu.”Licha ya changamoto hizi, Alya Abu Shawish anasema uzoefu wake umeimarisha azma yake ya kuwasaidia wengine na kumhamasisha kufanya kazi katika uwanja ambao mara nyingi huonekana kutawaliwa na wanaume.(Sauti ya Alya Abu Shawish) – Sharon“Uzoefu huu haukunidhoofisha; uliimarisha azma yangu ya kuwasaidia wengine. Ulinitia moyo kufanya kazi katika masuala ya kuondoa mabomu na usalama na UNMAS uwanja ambao mara nyingi huonekana kuwa wa wanaume. Katika jukumu hili, ninachangia kupunguza hatari zinazosababishwa na mabaki ya vilipuzi vya vita na kusaidia jamii kuishi kwa usalama zaidi.”Wanawake wengine katika timu za UNMAS pia hushiriki katika shughuli za kuhamasisha jamii kuhusu hatari za mabaki ya vilipuzi, ambayo sasa yamekuwa moja ya changamoto kubwa zaidi za kibinadamu huko Gaza kadri uharibifu unavyoendelea kuenea. Kwa Abu Shawish, juhudi hizi hubeba ujumbe unaokwenda mbali zaidi ya kazi kwani inaonesha uimara na mnepo.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka huko Mashariki ya Kati ambako Leo ni siku ya nne ya mzozo mabomu yameripotiwa kuendelea kulipuka. Makombora yanarindima katika ukanda huo huku ndege zisizo na rubani au droni zikisababisha maafa sasa katika nchi 12. Pia tunakuletea muhtasari wa habari kama zifuatazo.Mgogoro wa Iran ukiendelea kupamba moto, Umoja wa Mataifa na mashirika yake wanaendelea kufuatilia kwa ukaribu kuhusu hali hiyo tete huku wakiendelea kuhamasisha amani kupitia diplomasia kwani tayari madhara ya moja kwa moja kwa wanadamu yameshaonekana. Mathalani leo Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, OHCHR, Ravina Shamdasani akirejelea tukio moja baya la kusikitisha ambapo inaripotiwa wasichana kadhaa waliuawa na kujeruhiwa wakati shule yao ya msingi huko Minab, kusini mwa Iran, iliposhambuliwa wakati wa saa za masomo, amesema, “watoto, wasichana wadogo katikati ya siku ya shule, mwanzoni mwa siku ya masomo, wanauawa kwa namna hii, mabegi yao ya shule yakiwa na, unajua, madoa ya damu juu yake.Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA leo limeeleza kwamba kulingana na picha mpya za satelaiti, sasa linaweza kuthibitisha baadhi ya uharibifu wa hivi karibuni kwenye majengo ya milango ya Kiwanda cha Kuchakata Mafuta cha FEP kilichojengewa chini ya ardhi huko Natanz, Iran. Ujumbe wa IAEA umefafanua kuwa hakuna athari zozote za mionzi zinazotegemewa na hakuna athari za ziada zilizobainika kwenye Kiwanda cha FEP chenyewe, ambacho tayari kilikuwa kimeharibiwa vibaya katika mzozo wa mwezi Juni.Leo ni Siku ya Kimataifa ya Wanyamapori mwaka huu kaulimbiu ya siku ikilenga “Mimea ya Dawa na Harufu nzuri inaangazia nafasi muhimu ya mimea hii katika kudumisha afya ya binadamu, urithi wa kitamaduni, na kipato cha jamii za wenyeji. Katika ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akionesha wasiwasi wake kuhusu kutoweka kwa miea asili ya dawa ametoa wito akisema,ninazihimiza nchi zote ziwe watunza bustani wa rasilimali za pamoja za dunia.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu Volker Türk ameonya kuwa shinikizo linaongezeka duniani kote dhidi ya haki za wanawake, uhuru wa kiraia na taasisi za kimataifa akitoa wito kwa serikali kujitolea upya katika ushirikiano, uwajibikaji na utawala wa sheria. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.
Kwa wanafunzi wa kimataifa wanaosomea nchini Australia, kupata huduma ya afya mara nyingi huonekana kama swala ghali sana... au la kutatanisha sana kuweza kuipitia.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Tanzania ambako UNHCR inasema ufadhili endelevu na wa uhakika unahitajka ili kuendeleza ulinzi wa wakimbizi na kusaidia urejeaji na ujumuishaji wa raia wanaorudi nchini Burundi. Pia tunakuletea jifunze Kiswahili.Ushirikiano wa kimataifa kupitia mikataba ya kimataifa ya kudhibiti dawa umesaidia watu duniani kote, imesema hii leo Bodi ya Kimataifa ya kudhibiti dawa za kulevya, INCB wakati ikizindua ripoti ya mwaka 2025 kuhusu hali yad awa za kulevya duniani.Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wa haki za binadamu wamelaani vikali ukatili unaodaiwa kufanywa na kundi la waasi la M23 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, dhidi ya watetezi wa haki za binadamu katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini mashariki mwa taifa hilo la Maziwa Makuu.Na leo ikiwa ni siku ya tatu ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) huko The Hague Uholanzi kuthibitisha iwapo kuna ushahidi wa kutosha wa kumfikisha mahakamani Rais wa zamani wa Ufilipino Rodrigo Duterte kwa madai ya uhalifu dhidi ya ubinadamu unaohusianana kile kilichoitwa “vita dhidi ya dawa za kulevya” nchini mwake, wakili upande wa utetezi, Nicholas Kaufmann amesema hakuna uhusiano uliothibitishwa kati ya hotuba zake za “kipekee, zenye kauli kali” na mauaji anayotuhumiwa kuyafanya.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali “ANUIAYE KUKUTUKANA HAKOSI MATANGO”Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!
Tuliyokuandalia katika Jarifada la Habari hii leoNi miaka miine tangu uvamizi kamili wa Urusi nchini Ukraine, Umoja wa Mataifa wataka vita vikome mara moja kuwapunguzia madhila raiaHuko Gaza Shirika la UNICEF limezindua mpango wa Gaza we want au Gaza tuitakayo ili kukusanya maoni ya watoto baada ya miaka miwili ya vitaHuko The Hague Uholanzi kikao cha majaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, (ICC) cha kuthibitisha iwapo kuna ushahidi wa kutosha wa kumfikisha mahakama aliyekuwa Rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte kwa madai ya uhalifu dhidi ya ubinadamu kinaendeleaMada yetu kwa kina inajikita Tanzania kuangazia juhudi za kuhakikisha wasichana na wanawake hawaachwi nyuma katika sayansiNa katika jifunze Kiswahili utasikia maana na neno "PEMBUA"
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina tukimsikia Barbara Batte Guevara, Mkufunzi anayefundisha lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Havana nchini Cuba. Kwa kushirikiana na Tanzania chuo hicho ambacho mwezi uliopita kimetimiza miaka 298 tangu kuanzishwa kwake, hivi karibuni kimetoa fursa kwa Wacuba kujifunza lugha ya Kiswahili.Anold Kayanda wa Idhaa hii amemtembelea Profesa Barbara Batte katika jiji la Havana nchini Cuba ili kufahamu zaidi kuhusu hatua hii na mafanikio yaliyofikiwa hadi kufikia sasa. Pia tunakuletea habari kwa ufupi kama zifuatazo.Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Kimataifa wa Akili Mnemba au AI wenye thamani ya dola bilioni 3, ili kuhakikisha teknolojia hiyo inawanufaisha watu wote duniani, badala ya kuwa mali ya mataifa machache au kampuni chache zenye nguvu. Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa kujadili Athari za AI huko New Delhi nchini India, Guterres amesema mustakabali wa AI unapaswa kujengwa kwa ushirikiano wa kimataifa”.Mashambulizi makali yanayoendelea kufanywa na Israeli dhidi ya maeneo ya Palestina ya Gaza na Ukingo wa Magharibi ambayo inakalia kimabavu yanatia hofu ya uwezekano wa utokomezaji wa kabila, imesema Ripoti mpya ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR), ya kuanzia Novemba 1 2024 hadi Desemba 31 2025. Ripoti inasema mashambulizi ya Israeli yameweka mazingira ambamo kwamo wapalestina kama kundi watashindwa kuendelea kuishi Gaza huku Ajith Sunghay, Mkuu wa Ofisi ya OHCHR Palestina akisema, “ripoti inachambua mwenendo wa mapigano ya jeshi la Israeli, linaloendelea kuua idadi kubwa ya raia, kusababisha njaa, kuwahamisha takribani wakazi wote wa Gaza, tena zaidi ya mara moja — na kuharibu miundombinu iliyosalia ya kiraia ya Gaza.”wanamgambo wa vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan walitekeleza kampeni iliyoratibiwa ya uharibifu dhidi ya jamii zisizo za kiarabu ndani ya mji wa El-Fasher na viunga vyake, kampeni yenye viashiria vya mauaji ya kimbari, imeeleza ripoti mpya iliyotolewa leo na Tume Huru ya Umoja wa Mataifa ya Kuchunguza Ukweli kuhusu Sudan. Ripoti imetaja vitendo hivyo ni pamoja na kuua wanachama wa kundi la kikabila linalolindwa; kusababisha madhara makubwa ya kimwili na kiakili; ambavyo ni vipengele muhimu vya kosa la mauaji ya kimbari chini ya sheria za kimataifa.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili tunawasikiliza baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Havana wanaojifunza lughaya Kiswahili. Tuanze na Yibran Nunez Batte.Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!