POPULARITY
Jaridani leo tunakuletea mada kwa kina maalum ambayo kama nilivyokujuza hapo awali inaangazia mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu CRPD, unaofanyika hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa chini ya kauli mbiu “kuadhimisha miaka 20 ya mkataba huo na kuimarisha utekelezaji wake katika dunia inayobadilika.”Washiriki wanajadili namna ya kutokomeza ukandamizaji, ukatili na manyanyaso dhidi ya watu wenye ulemavu, kuimarisha mifumo ya huduma na msaada, pamoja na kuongeza ushiriki na uwakilishi wao katika maisha ya kisiasa na umma. Miongoni mwa wanaohudhuria mkutano huo ni Nassriya Nassir Ali mbunge wa watu wenye ulemavu kutoka nchini Tanzania, yeye anaulemavu wa kusikia au kiziwi. Leah Mushi amefanya mahojiano naye na hapa mkalimani wake wa lugha ya Alama Tusajigwe Ernest anajibu kwa sauti. Pia tunakuletea mhtasari wa habari tukimulika haki za elimu kwa watoto nchini Sudan, usalama wa mabaharia na judhibiti wa kusambaa kwa virusi vya Ebola hasa wakati huu wa michezo ya kimataifa ya kuwania kombe la dunia. Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Mataifa ya Afrika yameshuhudia mafuriko katika miaka ya hivi karibuni ,hali ambayo imesababisha wananchi wengi kulazimika kuhama makazi yao Nchini Kenya ,ukanda wa magharibi ,katika eneo la Busia,mafuriko hayo yamevuruga kalenda za wanafunzi wa shule ,watoto wengi wakishindwa kuendelea na shule au kukubaliana na msongamano kwenye shule chache ambazo ziko maeneo salama Hali hii imewasababisha changamoto za afya ya akili anavyoeleza mwaandishi wetu Petronila Ogalo.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambayo inamulika harakati za kudhibiti mlipuko wa Ebola zinaendelea huko DRC na Uganda. Maafisa wa WHO walipozungumza na waandishi wa habari huko Geneva, Uswisi walitoa ufafanuzi wa masuala kadhaa ikiwemo chanjo na nini cha kufanya ili jamii iwe kitovu cha udhibiti wa maambukizi.Hadi sasa Tani 30 za vifaa vya dharura vya kukabiliana na Ebola zimewasili Bunia, mashariki mwa DRC, ndani ya siku nne kwa msaada wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa MONUSCO. Vifaa hivyo ni pamoja na dawa, vifaa vya maabara, PPE na mahema ya kuhudumia wagonjwa. Wakati huo huo MONUSCO inaendelea kuelimisha wananchi kuhusu njia za kujikinga, huku WHO ikisema zaidi ya watu 600 wanashukiwa kuwa na Ebola na vifo 139 vinavyohusishwa na ugonjwa huo vimeripotiwa tangu mlipuko huo kuanza.Tukisalia na Ebola, Ili vifaa vya Ebola vifike kwa wakati, wako mashujaa nyuma ya pazia wanaohakikisha kila mzigo unasafiri salama. Miongoni mwao ni Milton Oloo, mwenye miaka 30 ya uzoefu wa kupakia mizigo JKIA nchini Kenya, ambaye sasa yuko mstari wa mbele kusaidia safari za ndege za Umoja wa Mataifa, UNHAS. “Tunachokifanya hapa leo ni kuhakikisha kwamba mizigo inayoelekea Congo DRC imepangwa vizuri na kupakiwa ipasavyo ili isiharibike. Pia naona fahari na Maisha ya watu yanayookolewa nafurahi”.Na jukwaa la 13 la miji dunini WUF13 linaelekea ukingoni Baku Azerbaijan likijadili changamoto ya makazi duniani, Rehema Kishoa kutoka Tanzania Mkurugenzi Msaidizi wa Uzingatiaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya ardhi anasema wao wamechukua hatua kukabili changamoto hiyo.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili, leo mchambuzi wetu ni Dkt. Josephat Gitonga, ambaye ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, kwenye kitivo cha Tafsiri na Ukalimani anafafanua maana ya methali “Kware hutetemekea majanini.”Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!
Miongoni mwa habari kuu za dunia zilizopewa uzito juma hili ni pamoja na kuapishwa kwa rais wa Uganda Yoweri Museveni kwa muhula wa saba, kufanyika na kutamatika kwa mkutano wa Afrika na Ufaransa jijini Nairobi nchini Kenya, kauli ya rais wa Rwanda Paul Kagame akikosoa vikwazo vya Marekani kuhusu nchi yake, eneo la Afrika magharibi hususan Nigeria, Ghana na Mali, lakini pia Ziara ya rais wa Marekani Donald Trump huko China. Ungana na Ruben Lukumbuka, kupata mengi zaidi
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayomulika Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani CSW70 uliofanyika mwezi Machi mwaka huu hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa ambapo tulipata fursa ya kuzungumza na washiriki wakiwemo wawakilishi wa mashirika ya wanawake. Miongoni mwao ni Severina Lemachokoti kutoka asasi ya kiraia ya Naretu Girls and Women Empowerment Programme iliyoko kaunti ya Samburu nchini Kenya, ambaye katika mahojiano na Flora Nducha ameelezea jinsi mila na desturi kwa wanawake na wasichana kutorithi chochote kwenye jamii yao zinavyoanza kuyoyoma. Pia tunamsikia kutoka Salome Gatakaa Araka wa FODDAJ ambalo ni Jukwaa la Maendeleo ya Wanawake, Demokrasia na Haki, nchini Kenya ni shirika la kiraia ambalo mwaka huu kwa mara nyingine lilishiriki mkutano huo wa CSW70. Baada ya kushriki vikao mmoja wa viongozi wa shirika hilo amezungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na ndio msingi wa mahojiano haya.Tunakuletea pia muhtasari wa habari zikiwemo za hali ya kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, na Sudan, pamoja na masuala ya afya tukimulika yanaoendelea kuhusu virusi vya Hanta au Hantavirus.Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!
Mapambano ya kimataifa dhidi ya homa ya ini ya virusi aina ya B na C yanaanza kuonesha mafanikio, imesema ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO, iliyotolewa Aprili 28, 2026. Ripoti hiyo, imezinduliwa wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Homa ya Ini mjini Bangkok, Thailand, mkutano ulioingia leo siku ya pili na unakunya jamvi kesho. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina ambapo juzi Jumanne na jana Jumatano wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa walipata fursa kunadi serra zao mbele ya nchi wanachama kwenye Baraza Kuu wakiwemo wawakilishi wa asasi za kiraia walioweza kuwauliza maswali. Miongoni mwa wawakilishi hao ni Irene Kitoti, Mwanzilishi na mkurugenzi wa asasi ya kiraia ya Genesis For Children Organization ya nchini Tanzania aliyezungumza na Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili. Pia tunakuletea muhtasari wa habari kama zifuatazo.Kutokana na mafanikio ya kihistoria kwa afya ya umma ya eneo la Karibe, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni, WHO limeipongeza nchi ya Bahamas kwa kuwa taifa la hivi karibuni zaidi katika ukanda huo wa Karibe kuthibitishwa kuwa limekomesha maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI, VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus, kupitia taarifa ya shirika hilo ameipongeza Bahamas kwa mafanikio haya makubwa, yanayoimarisha miaka ya dhamira ya kisiasa na kujitolea kwa wahudumu wa afya.Ikiwa leo imetimia miaka 15 tangu kuanza maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wasichana katika Teknolojia ya Habari na Mawasilino, TEHAMA au ICT, Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano (ITU), Doreen Bogdan-Martin katika ujumbe wake mahususi wa maadhimisho ya mwaka huu amesema, “kwa sasa tunaishi katika kipindi cha mabadiliko makubwa na ya kusisimua zaidi ya kiteknolojia katika historia ya binadamu lakini vilevile kwa sasa fursa zinazohusiana na mabadiliko haya ya kiteknolojia hazimfikii kila mtu kwa usawa”.Mgogoro wa usafirishaji katika Mlango Bahari wa Hormuz uliosababishwa na vita vya Mashariki ya Kati umefichua tishio jipya: upungufu wa madini ya kimkakati yanayoendesha uchumi duniani kote na sasa nchi huenda zitaanza kuhaha kuyapata. Katika mkutano na waandishi wa habari leo jijini Geneva Uswisi, Dario Liguti, Mkurugenzi wa Kitengo cha Nishati Endelevu cha Tume ya kiuchumi ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Ulaya, UNICE amesema, “hatua ya kwanza, mbali na ongezeko la bei bila shaka, itakuwa viwanda kupunguza matumizi yake yake ya madini ya kimkakati na hivyo kupunguza uzalishaji… iwe ni paneli za sola, sumaku, betri na kadhalika, katika siku zijazo.”Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili hii leo mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA. Anafafanua maana za neno "KUPARAMA"Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Uchaguzi Mkuu nchini Kenya ni mwezi Agosti mwaka 2027, lakini wanasiasa mbalimbali wameanza kuonesha nia ya kugombea kiti cha urais. Miongoni mwao ni Ruben Kigame, mwanasiasa, mwanaharakati, mhadhiri, mwandishi wa Habari na mwanamuziki maarufu wa nyimbo za Injili. Yeye ni mlemavu wa Macho, ameamua kujitosa uwanjani, kutafuta uongozi wa nchi ya Kenya. Nini kimemsukuma ? Wiki hii anazungumza na mwenzangu, Benson Wakoli.
Miongoni mwa matukio makubwa yaliyojiri wiki hii ni pamoja na timu ya taifa ya soka ya DRC Leopards kufuzu kushiriki fainali ya michuano ya kombe la dunia 2026, shambulio la waasi wa ADF laua 30 mashariki mwa DRC, watoto wanne wadungwa kisu hadi kufa katika shule moja nchini Uganda, wapigakura wahamasishwa kujiandikisha nchini Kenya na kupanda kwa bei ya mafuta, kuapishwa kwa rais wa Jamhuri ya afrika ya kati, vitisho vya Trump kuhusu mlango bahari wa Hormuz
Miongoni mwa yaliyojiri wiki hii ni pamoja na baraza la usalama la umoja wa mataifa lataka kufunguliwa upya kwa viwanja vya ndege kwenye miji ya Goma na Bukavu mashariki mwa DRC, kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine alisema uhuru wake sio mjadala, miili 14 ilipatikana iliyopatikana nchini Kenya kufanyiwa upasuaji kubaini chanzo cha vifo. utambuzi wa utumwa kuwa uhalifu dhidi ya haki za ubinadamu, na rais Trump, aahirisha mpango wake wa kushambulia vinu vya nishati vya Iran
Miongoni mwa matukio makubwa ni pamoja na mwendelezo wa mashambulizi ya Marelkani na Israeli huko Iran, na nchi za Ghuba, huku bei ya mafuta na gesi ikipanda, DRC na Rwanda zilikubaliana kupunguza uhasama wao, rais wa Kenya William Ruto alizindua ujenzi wa reli ya kisasa SGR katika eneo la magharibi mwa nchi yake, hali ya nchini Sudan na Senegal yavuliwa ubingwa AFCON, Morocco ilitangazwa mshindi. Ungana na mwandishi wetu Ruben Lukumbuka
Watalaam wanasema vijana wengi hufikia kwenye maduka ya kuuza dawa kupata huduma za afya baadala ya kufika hospitali kufanyiwa vipimo Unyanyapaa pia inachangia wanaume au vijana kuwa na ari ya kwenda kupata huduma za afya haswa za TB.
Katika makala haya tunajdili Juma lililopita wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kumteua rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuwa mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo, huku wakitangaza mabadiliko kadhaa muhimu waliyosema yanalenga kuifanya jumuiya kutosambaratika. Miongoni mwa mabadiliko ni pamoja na nchi wanachama kuwalipa mshahara wabunge wao na namna nchi zinazodaiwa zitalipa madeni yake. Unafikiri mabadiliko haya yatasaidia Jumuiya Kukua? Skiza maoni ya mskilizaji.
Katika makala haya tunajdili Juma lililopita wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kumteua rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuwa mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo, huku wakitangaza mabadiliko kadhaa muhimu waliyosema yanalenga kuifanya jumuiya kutosambaratika. Miongoni mwa mabadiliko ni pamoja na nchi wanachama kuwalipa mshahara wabunge wao na namna nchi zinazodaiwa zitalipa madeni yake. Unafikiri mabadiliko haya yatasaidia Jumuiya Kukua? Skiza maoni ya mskilizaji.
Miongoni mwa utakayo yasikia hii leo jaridani ni mzozo huko Mashariki ya Kati baada ya Israel na Marekani kuishambulia Iran na kisha Iran kujibu mashambulizi. Sasa nchi jirani nazo zimeathirika ikiwemo Lebanon ambapo sasa UNHCR inatoa msaada kwa wananchi. Zikiwa ni siku chache kabla ya Siku ya wanawake duniani tarehe 08 Machi, leo utasikilia simulizi ya mwanamke aliyekuwa akifanyiwa ukatili na mume wake na msaada aliopokea kutoka WLAC. Katika masuala hayo hayo ya wanawake tutasikia wanawake wa Masrabit wanavyoelimisha wenzao kukataa ukeketaji kupitia mradi wa UNFPA nchini Kenya
Agizo la kiutendaji lililosainiwa na rais wa Marekani linaagiza Marekani kujiondoa kutoka kwa jumla ya mashirika 66, karibu nusu yake ambayo yana uhusiano na Umoja wa Mataifa, Ikulu ya White House ilisema wiki iliyopita. Miongoni mwa hayo ni Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC), mkataba wa msingi wa mikataba mingine yote ya kimataifa ya hali ya hewa, uliohitimishwa mwaka wa 1992 katika Mkutano wa Rio Earth.
Agizo la kiutendaji lililosainiwa na rais wa Marekani linaagiza Marekani kujiondoa kutoka kwa jumla ya mashirika 66, karibu nusu yake ambayo yana uhusiano na Umoja wa Mataifa, Ikulu ya White House ilisema wiki iliyopita. Miongoni mwa hayo ni Mkataba wa Mfumo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa (UNFCCC), mkataba wa msingi wa mikataba mingine yote ya kimataifa ya hali ya hewa, uliohitimishwa mwaka wa 1992 katika Mkutano wa Rio Earth.
Mnapofikiria kutazama ndege, labda mnawazia wastaafu. Lakini kizazi kipya kinaanza kutumia darubini na kujihusisha na burudani hii. Kile kilichokuwa kimbilio kutoka ulimwengu wa mtandaoni sasa kinafufuka tena mtandaoni.
Miongoni mwa matukio makubwa ni pamoja na kukamatwa kwa aliyekuwa rais wa Venezuela Nicolas Maduro, kubanduliwa kwa timu ya taifa ya DRCongo kwenye michuano ya AFCON 2025, vifo vya wakimbizi wa Congo Kinshasa katika kambi huko Burundi, siasa za Tanzania, Kenya na Uganda kuelekea uchaguzi wa January 15 hali ya nchini Sudan kusini, Rais Faustin Archange Touadera kutangazwa mshindi wa Uchaguzi wa urais hivi karibuni na kauli ya Urusi kuhusu washirika wa Ukraine, Ulaya
Miaka 80 iliyopita baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, mataifa 50 yalikutana huko San Francisco hapa nchini Marekani na kupitisha Chata iliyoanzisha Umoja wa Mataifa. Miongoni mwa malengo ni kuzuia vita na kujenga uhusiano mwema baina ya mataifa. Mathalani kuepusha nchi moja kuvamia nchi nyingine na kulinda haki za binadamu. Leo hii Chata hiyo imeendelea kusiginwa na kilichoibua mjadala zaidi ni tukio la Januari 3 la Vikosi Maalum vya Marekani kuingia Venezuela na kumtwaa Rais wa nchi hiyo Nicolas Maduro pamoja na mkewe kwa madai ya kwamba wanatakiwa wajibu tuhuma nchini MArekani za uhalifu mkubwa ikiwemo usafirishaji wa dawa za kulevya. Je Chata hiyo inasema nini? Assumpta Massoi na Rashid Malekela wanapitia baadhi ya vifungu pamoja na yaliyojiri baada ya hatua ya Marekani.
Miongoni mwa matukio makubwa ya wiki hii ni pamoja na waasi wa AFC/M23 kutangaza kujiondoa kwenye mji wa kimkakati wa Uvira mkowani kivu kusini mashariki mwa DRC hatua ambayo imetiliwa mashaka, shirika la kimataifa la Amnesty lasema polisi nchini Tanzania walitumia nguvu kupita kiasi kudhibiti waandamanaji kipindi cha uchaguzi, wafuasi wa rais wa Tunisia, Kais Saied waandamana kuonesha ungwaji mkono huku mzozo wa kisiasa ukizidi, Umoja wa ulaya EU kuiipa Ukraine mkopo wa Yuro Bilioni 90
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO, limeongoza uhamishwaji wa wagonjwa kutoka Gaza eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israeli, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa awamu mpya ya kusitishwa kwa mapigano kwenye ukanda huo.Katika muda wa siku mbili, wagonjwa 41 waliokuwa katika hali mbaya pamoja na familia zao 145 wamehamishwa kutoka eneo la mgogoro, kuelekea Afrika Kusini, Uswisi na kwingineko, huku maelfu zaidi wakiendelea kusubiri matibabu ya dharura.Katika hospital iliyojengwa kwa mahema katika eneo la AL-MAWASI, RAFAH kwenye Ukanda wa Gaza wagonjwa wakihudumiwa kila kona watoto kwa wakubwa Miongoni mwao ni Ibrahim Abu Ashiba, mkurugenzi wa filamu ambaye maisha yake yamebadilika ghafla. Anakumbuka wakati alipojeruhiwa. Anasema, "Nilipigwa risasi mara kadhaa, mara moja kwenye kifua, mara moja kwenye bega, mara mbili mkononi. Risasi hizo mbili zilikata mishipa ya neva ya mkono wangu. Sasa siwezi kushika kamera wala kunyoosha mkono wangu kawaida. Ghafla, maisha yangu yote yalisimama."Safari ya kupona kwa Ibrahim inaanzia Afrika Kusini, ambapo amekubaliwa kwenda kupokea matibabu maalum ambapo anasema "Maisha yangu yote yalikuwa yamesimama baada ya kujeruhiwa hadi waliponipigia simu na kunijulishakwamba nitasafiri kwenda Afrika Kusini kwa matibabu. Ilionekana kama nimezaliwa upya."Mgonjwa mwingine katika hospitali hii ni, Maria Al-Shaer, alijeruhiwa vibaya katika mashambulizi yaliyokuwa yakiendelea Gaza, huku akipoteza ndugu zake. Mama yake, Raghda Ahmed Al Shaer, anaelezea mateso hayo. "Maria amepoteza baba yake na ndugu zake wote. Alijeruhiwa na kuvunjika mguu, mifupa na kupoteza nyama. Anahitaji upasuaji wa kuwekewa viungo bandia. Maisha yake yamegeuka, hawezi kutembea, na hali yake ya kisaikolojia imeathirika sana."Uhamishwaji huu umeratibiwa na Shirikisho la Chama cha Msalaba Mwekundu Palestina, kwa msaada wa WHO. Dkt. Luca Pigozzi, Mratibu wa Timu ya Dharura ya WHO, anafafanua umuhimu wake."Huu ni uhamishaji wa kwanza wa matibabu tangu kusitishwa kwa mapigano Oktoba 10. Tumejizatiti kuongeza uwezo wetu kusaidia na kuratibu uhamishaji kwa ajili ya matibabu, kwa ushirikiano wa karibu na Shirikisho la chama cha Msalaba Mwekundu la Palestina."Raghda anaeleza matumaini kwa ajili ya binti yake wanapohama kwenda Uswisi. "Wametupigia kutuarifu kwamba Maria amekubaliwa kusafiri kwenda Uswisi kwa matibabu. Tumefurahi sana kwamba atatembea tena, na hali yake ya kisaikolojia itaboreka. Atarudi kuwa Maria wa kawaida kama tuliyemjua."WHO inasisitiza kuwa wagonjwa takriban 15,000 bado wanangojea idhini ya kupata matibabu nje ya Gaza na inatoa wito kwa nchi zote kufungua milango yote za dharura kwa ajili ya uokoaji wa wagonjwa.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayoangazia siku ya chakula duniani ikienda sambamba na maadhimisho ya miaka 80 ya kuanzishwa shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, na utamsikia Mwakilishi wa FAO nchini Tanzania Bi. Nyabenyi Tito Tipo akieleza.Maadhimisho ya siku ya chakula duniani yamefanyika kimataifa leo huko Roma nchini Italia, yakienda sambamba na sikukuu ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na kilimo, FAO. Katika ujumbe wake alioutoa kwa njia ya video Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema, “Miaka themanini iliyopita, katika dunia iliyosambaratishwa kwa vita, nchi zilikutana kukabiliana na njaa. Miongo kadhaa tangu wakati huo, dunia imepiga hatua kubwa. Lakini bado majanga yanyoonesha kuwa hatuwezi kubweteka iwapo tunataka kuendeleza mafanikio tuliyopata. Tuna mbinu, ufahamu, rasilimali za kutokomeza njaa, na kupatia kila mtu chakula kizuri na chenye afya. Tunachohitaji ni umoja.Huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, raia wamerejea kufuatia makubaliano ya sitisho la mapigano lakini wanahaha kujenga upya makazi yao huku wakiwa wamezingirwa na vifusi. Miongoni mwao Ayman Awadallah, amesema “hakuna maji, hakuna miundombinu ya majitaka, hakuna maisha hapa, hakuna chochote.”Na kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga, kilichotokea Jumatano Oktoba 15 nchini India, Umoja wa Mataifa kupitia Katibu Mkuu umetuma salamu za rambirambi na kusema hayati Odinga, alikuwa mtu muhimu katika maendeleo ya kidemokrasia nchini Kenya na pia mtetezi thabiti wa mageuzi ya kikatiba na utawala jumuishi.Na katika kujifunza Kiswahili hii leo, mtaalam wetu Onni Sigalla, Mhariri mwandamizi wa Baraza la Kiswahili la Taifa nchini Tanzania, BAKITA anafafanua maana za neno "KIMWA"Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Hii leo ni hotuba ya Israeli kwenye mjadala mkuu wa baraza kuu, nini kilitokea? Kijana daktari mwanaharakati kutoka Ghana aishiye Uingereza akiwa UNGA80 na matumaini mapya ya kinga dhidi ya maambukizi ya VVU.Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ukiwa umeingia katika siku yake ya nne hapa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani leo Ijumaa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amekuwa wa kwanza kuzungumza akitumia muda wake mwingi kushambulia wanamgambowa kipalestina, Hamas na kutetea kila uamuzi wa Israel. Anold Kayanda ameifuatilia hotuba hiyo kwa kina. Karibu Anold utupe japo kwa muhtasari.Tukisalia hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, moja ya mikutano ya ngazi ya juu iliyofanyika kando ya mjadala mkuu wa Baraza Kuu, ni ule wa kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa program ya Umoja wa Mataifa kuhusu vijana, mkutano ukileta vijana kutoka kona mbali mbali za dunia. Miongoni mwao ni daktari wa tiba na mwanaharakati wa kijamii wa vijana kutoka Uingereza mwenye asili ya Ghana, Dkt. Khadija Owusu. Amezungumza na Flora Nducha anayetujulisha zaidi katika taarifa hiiKatika hatua kubwa ya kihistoria kwenye mapambano dhidi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) dawa mpya ya kudungwa inayoitwa Lenacapavir inatarajiwa kupatikana kwa gharama nafuu katika nchi 120 zenye kipato cha chini na kati kuanzia mwaka 2027. Dawa hiyo itauzwa kwa kiasi cha dola 40 pekee ikiwa ni gharama ya vidonge vya kila siku vya kujikinga na VVU ambavyo mhusika atatumia kwa mwaka mzima. Sabrina Saidi ana taarifa zaidi.
Katika Mkutano wa Vijana wa Umoja wa Mataifa unaofanyika kandoni mwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA80 unaoendelea hapa New York, viongozi vijana kutoka duniani kote wanataka uwakilishi mkubwa katika maamuzi ya kimataifa.Miongoni mwao ni daktari wa tiba na mwanaharakati wa kijamii wa vijana wa Uingereza na Ghana, Dkt. Khadija Owusu ambaye amezungumza na Flora Nducha wa Idhaa hii ya Kiswahili.Owusu, ambaye pia ni mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Akaya inayowakilisha wasichana wa zama hizi, anasema vijana hawapaswi kuzungumziwa tu, bali wajumuishwe moja kwa moja katika kuandaa Suluhu za changamoto zinazoihusu dunia wakiwemo na wao "Mara nyingi tunazungumza kuwa tunataka ushiriki zaidi wa vijana wakati umefika wa kuacha kuzungumza tu kuhusu kuhitaji vijana wengi, bali tuwe na vijana wengi."Niko hapa kuwakilisha maelfu ya wasichanaAnasema ushiriki wake katika mkutano huu wa ngazi ya juu wa vijana si wa kibinafsi tu, bali unaakisi sauti za wasichana na vijana wengi wanaosaidiwa na taasisi yake ya Akaya."Niko hapa kuwakilisha si mimi peke yangu, si Uingereza tu, na si Ghana tu, bali Taasisi ya Akaya, na wasichana na vijana wengi tunaowahudumia nchini kote."Owusu anaamini vijana wa Kiafrika, hususan wasichana, wanapaswa kupata nafasi kubwa zaidi katika jmaukwaa ya kimataifa kama Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kupaza sauti zao."Bado tunahitaji kuona vijana zaidi kama sisi kwenye vyumba vya mikutano, Waafrika zaidi, vijana zaidi wa Kiafrika na wasichana wa Kiafrika kwenye vyumba vya mijadala, wakishiriki majadiliano kwa sababu tunaleta mabadiliko halisi."Owusu anasema ujumbe wake kwa vijana barani Afrika ni kubeba vipaji vyao, wajiamini, na kuendeleza ndoto zao kwani kila kitu kinawezekana.
Sasa twende Gaza, hii ni hadithi ya maisha, ya watoto wa Gaza wanaokabiliana na baa la njaa, hofu, na kuporomoka kwa kila kitu kinachowaweka hai. Ni hadithi inayoelezwa kupitia macho ya wale wanaoshuhudia mateso kila siku wakiwemo madaktari, akina mama, na wahudumu wa kibinadamu wanaopiga kengele ya tahadhari. Miongoni mwa wahudumu hao ni Tess Ingram afisa mawasiliano wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF ofisi ya Kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Flora Nducha anasimulia alichokishudia(TAARIFA YA FLORA NDUCHA)Tess aliyefunga safari na kushuhudia hali halisi Gaza akizungumza na waandishi wa habari kutoka mji wa Al Mawasi amesema mwenye macho haambiwi tazama na alichokishuhudia ni cha kutisha kwani jiji hilo sasa linazidi kuzama kwenye lindi la baa la njaa, vituo vya lishe vimefungwa, familia zinalia na kuhaha na watoto wanakufa kila uchao bila msaada.(Tess Ingram- Sheillah)“Jiji la Gaza, kimbilio la mwisho kwa familia za Kaskazini, linakuwa mahali ambapo utoto hauwezi kuishi. Ni jiji la hofu, wakimbizi na mazishi.”Anasema zaidi ya nusu ya vituo vya lishe vya watoto vimefungwa na kina mama wanapofika hospitalini wakiwa wamebeba watoto wao unaoweza kuhesabu mbavu sababu ya kukonda wanaambulia patupu kwani msaada ni haba na kwengine hakuna kabisa.(Tess Ingram 2-Sheilah):“Kilichokuwa hakifikiriki si jambo lijalo ni hali ambayo iko hapa tayari. Kuanguka kwa huduma muhimu na kunawaacha watoto wasiojiweza Gaza wakihaha kusalia uhai.”Tess anasema ukiingia katika vituo vya msaada ndio utatambua wanachokipitia watoto wa Gaza kwani, mateso yanaonekana bayana(Tess Ingram 3-Sheillah)“Saa moja tu ndani ya kliniki ya lishe inatosha kuondoa shaka na shuku yoyote uliyonayo ya endapo Gaza kuna baa la njaa.”UNICEF inasisitiza wito wake kuwa raia walindwe, msaada wa chakula na dawa upelekwe kwa wahitaji bila vizuizi. Kwa sababu watoto wa Gaza bado wako hai na dunia ina uwezo wa kuamua endapo wasalie hai.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR kwa kushirikiana na Baraza la Wakimbizi la Norway NRC wanahakikisha wakimbizi wanaoishi katika kambi za wakimbizi za mkoani Kigoma Magharibi mwa Tanzania ikiwemo kambi ya nyarugusu wanapata huduma muhimu za maji na usafi kupitia ushirikiano wa viongozi wa wakimbizi. Huduma hizo zimekuwa changamoto kubwa katika kambi za wakimbizi zikichangiwa na ukata wa ufadhili. Flora Nducha na taarifa zaidi (TAARIFA YA FLORA NDUCHA)Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilipoibuka Burundi mwaka 2015, na baadaye mapigano kuighubika upya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, maelfu ya watu walikimbia na kuvuka mpaka kuingia Tanzania. Leo, wengi wao wanaishi katika kambi za wakimbizi mkoani Kigoma kama vile Mtendeli, Nduta, na Nyarugusu.Lakini maisha kambini hayajakuwa rahisi. Kwa ufadhili mdogo, familia zinapata shida kupata huduma za msingi kama maji safi, makazi, na elimu.Hapo ndipo Shirika la UNHCR, na Baraza la Wakimbizi la Norway NRC, wanapoingia. Tangu mwaka 2016, wamekuwa wakitoa huduma muhimu ikiwemo kufunga mifumo ya maji, kujenga vyoo, na kusambaza sabuni na mahitaji mengine ya usafi.Miongoni mwa wanaofanya mabadiliko kupitia msaada huo ni Ahunga Msama, mkimbizi mwenye umri wa miaka 55 kutoka DR Congo, ambaye ni afisa msimamizii wa huduma za maji, usafi, kujisafi na usafi wa mazingiira WASH katika kambi ya Nyarugusu.(AHUNGA CLIP 1)“Ninasaidia jamii yetu ya kambi ya Nyarugusu ili wawe wanapata maji safi na salama”Ahunga anasema jamii yake iliteseka sana iliteseka sana kwa magonjwa yanayosababishwa na maji machafu ndio maana aliamua kuchukua hatua kulinda afya zao. Kila siku ahakikisha watu wanapata maji safi na huduma za usafi salama.Akiwa pamoja na wakimbizi wenzake, Ahunga anapita nyumba kwa nyumba kufundisha familia jinsi ya kuzuia magonjwa kupitia usafi kwani anaamini elimu ni ufunguo(AHUNGA CLIP 2)“Tunasaidia kuelimisha jamii yetu ili wawe wasafi. Wawe na vyoo, wawe na mabafu, wawe na vichanja na wawe na mashimo ya takataka.”Watu wakielewa, wanaweza kujilinda.Anasema watu wakieelewa ni rahisi kujilinda na juhudi zake zinaokoa maisha na kuhamasisha wengine, zikionyesha kwamba hata katika mazingira magumu, wakimbizi wanaweza kuongoza mabadiliko katika jamii zao na anasema hilo ni la muhimu sana kwani(AHUNGA CLIP 3)“Tunasaidia jamii yetu ili wajilinde na magonjwa ya milipuko”Kwa msaada wa UNHCR na Baraza la Wakimbizi la Norway, maelfu ya wakimbizi katika kambi za wakimbizi za Kigoma sasa wana maji salama, usafi wa mazingira ni bora, na wana matumaini mapya ya maisha.
Jaridani leo tunakuletea mada kwa kina, wiki ya Maji ikifikia tamati leo Agosti 28 na maudhui yakiwa Maji kwa ajili ya Hatua kwa Tabianchi, tunabisha hodi kaunti ya Kajiado nchini Kenya kumsikia mtendaji kwenye mradi wa maji wa Kerarapon Water Association ambalo ni shirika la kijamii linalohusika na maji na mazingira huko kaunti ya Kajiado nchini Kenya. Mengine ni kama yafuatayo.Ukraine ambapo leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameungama na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kulaani vikali mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani droni yaliyofanywa na Urusi usiku kucha kuamkila dhidi ya miji ya Ukraine na kusababisha vifo na majeruhi kwa raia, wakiwemo watoto, na pia kuharibu majengo ya kidiplomasia jijini Kyiv. Amesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu yao yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, akitaka yakome mara moja na kurudia wito wake wa kusitisha mapigano ili kuelekea amani ya kudumu itakayoheshimu uhuru wa watu, uhuru wa kitaifa na mipaka ya Ukraine kama inavyotambuliwa kimataifa.Kuhusu Mashariki ya Kati Katibu Mkuu António Guterres akizungumza na waandishi wa Habari hii leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ameonya kuwa operesheni za kijeshi mjini Gaza zitakuwa na zahma kubwa na amesisitiza “hili lazima likome.” Amesema njaa si tishio tena bali janga la sasa, huku raia, wahudumu wa afya na waandishi wa habari wakiuawa wakati “macho ya dunia yakitazama.” Guterres ameikumbusha Israel wajibu wake wa kisheria kulinda raia na kuruhusu msaada wa kibinadamu bila vikwazo akisema “Hakuna visingizio tena. Hakuna vizuizi tena. Hakuna uongo tena,” akitoa wito wa usitishaji mapigano haraka na kuachiliwa kwa mateka wote.Kikosi cha 11 cha Tanzania TANZBATT 11 kinachohudumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO kimetoa msaada wa magodoro kwa raia walioathirika na machafuko ya karibuni katika kijiji Oicha jimboni Kivu Kaskazini. Miongoni mwao ni Bi Masika Jistine na Mzee Bahati Paluku ambao hawakusita kuonesha furaha yao.Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili na hii leo Dkt Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana ya neno "MKWIJI!.Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Mratibu Maalum wa Kuboresha Hatua za Umoja wa Mataifa dhidi ya Unyanyasaji wa kingono (SEA) Christian Saunders amefanya ziara nchini Tanzania kuona maandalizi ya vikosi vya operesheni za ulinzi wa amani katika maeneo mbalimbali duniani. Kutoka Dar es Salaam, Tanzania, Kapteni Mwijage Inyoma Afisa Habari wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Tanzania (TPTC) ametuandalia taarifa hii.Ni bendi ya jeshi la Wananchi wa Tanzania, JWTZ ikiongoza askari wengine kumkaribisha Bwana Christian Saunders hapa katika Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Tanzania (TPTC) Kunduchi, Dar es Salaam.Miongoni mwa askari hawa tayari wameandaliwa kwenda katika nchi mbalimbali katika ukanda wa Afrika Mashariki na kati na hata nje ili kuusaidia Umoja wa Mataifa kutekeleza moja ya majukumu yake kwa ulimwengu, kuleta na kuitunza amani.Bwana Saunders anasema, “wacha nianze kwa kusema asante. Kusema asante ni jambo muhimu sana, kwa sababu mko tayari kuanza jukumu la kutumwa, iwe mnaenda Lebanon au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au kwingineko. Mkiwa mbali na familia zenu, mbali na nchi yenu, katika mazingira yenye changamoto, na wakati mwingine katika hali hatarishi.”Anawapa moyo zaidi askari lakini akiwakumbusha kuwa wao ni kioo cha ulimwengu wazingatie maadili“Na tunathamini sana kujitolea kwenu. Tunathamini sana kwamba mnaenda kuwasaidia ndugu zenu katika nchi nyingine, iwe ni nchi jirani au sehemu iliyo mbali. Mnapokwenda, mnaliwakilisha dunia. Mnawakilisha watu wa dunia.”Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Ulinzi wa Amani cha Tanzania (TPTC), Brigedia Jenerali George Itang'are akamthibitishia mgeni kwamba askari hawa wameiva na hakuna kisingizio chochote cha kutozingatia maadili huko wameandako, kisha akawahoji, Nao wanajibu, “twende pamoja, turudi pamoja.”
Machafuko yanayoendelea Kaskazini Mashariki mwa Burkina Faso yamefurusha maelfu ya watu, kukatili maisha na kuwalazimisha wengi kuwa wakimbizi ndani ya nchi yao. Miongoni mwa simulizi za kugusa ni ya Fadima Bandé mama aliyelazimika kufungasha virago kunusuru maisha yake na wanawe wawili lakini akaishia kupoteza mmoja, je ilikuwaje? kupitia video ya Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF Flora Nducha anasimulia zaidi.Katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Dori Mashariki mwa Burkina Faso, sasa ni maskani ya Fadima, maisha hapa ni magumu na hana tena njia ya kujipatia kipato. Kila uchao analazimika kupambana kuhakikisha watoto wake wanapata angalau mahitaji ya msingi, anakumbuka safari ya uchugu kutoka Kijiji kwake Sohlan hadi hapaWakati tunakimbia mmoja wa binti zangu mapacha aliugua baada ya kunyeshewa na mvua kubwa na kupata mafua makali, wakati tayari alikuwa anaumwa utapiamlo. Tulimkimbiza hospitai mjini Sebba lakini akafariki dunia.”Baada ya kupata hifadhi kambini Dori Fadima akajaliwa mapacha wengine wawili ambao sasa wana umri wa miezi tisa na kwa bahati mbaya wote wana utapiamlo kutokana na changamoto ya chakula.“Hapa Dori tumebarikiwa watoto mapacha lakini wametukuta hatua makazi, hatuna chochote na tuna njaa na kibaya zaidi sikuwa hata na maziwa ya kutosha kuwanyonyesha”Watoto wa Fadima wamekuwa wakiishi kwa msaada wa kibinadamu unaotolewa na mashirika mbalimbali ikiwemo UNICEF ambayo sasa inasema hali yao inaweza kuwa mbaya zaidi kutokana na kupunguzwa kwa bajeti ya kimataifa misaada wanayoitoa na hivyo kuhatarisha maisha na mustakabali wa watoto wake. Fadima anasema“Unapotawanywa na machafuko huwezi kufanya kazi, unakuwa kama mtu asiye na ajira na hapo ndio madhila yanapokuwa makubwa zaidi, lakini bado hapa ni bora kuliko ningesalia kijijini kwetu.”Kwa mujibu wa UNICEF Burkina Faso ni moja ya migogoro ya kibinadamu iliyopuuzwa zaidi duniani. Ingawa UNICEF iko hapa kusaidia, lakini inasema msaada zaidi unahitajika haraka.
Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) lilifanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani mwezi Aprili mwaka huu wa 2025. Jukwaa hili lilifanyika kwa siku 4 likileta pamoja vijana kutoka mataifa mbalimbali duniani na wadau wa maendeleo na uchumi ili kujadili changamoto zinazowakabili vijana na kutoa mapendekezo ya kuboresha dunia kuelekea usawa na maendeleo endelevu chini ya Ajenda ya 2030 au Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).Miongoni mwa vijana walioshirikki ni Kapwani Kavenuke, kutoka Tanzania. Akizungumza na Sharon Jebichii wa Idhaa hii, Bi. Kapwani alianza kwa kuelezea alichokuwa anasongesha mbele baada ya kushiriki mkutano wa Zama Zijazo au Summit of The Future uliopitisha Mkataba wa Zama Zijazo au PACT OF THE FUTURE mwezi SEptemba mwaka jana 2024.
Burundi inaonesha kwa vitendo mshikamano na wakimbizi kwa kuwapa fursa ya kupata elimu, huduma za afya, ajira na huduma nyingine za kitaifa, na hivyo kuwasaidia kuchangia katika jamii wanamoishi. Miongoni mwa wakimbizi hao ni Amani Lukoo Elie kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akiambana na mke wake na watoto 5 wamesaka hifadhi kusini-magharibi baada ya kukimbia mapigano jimboni Kivu Kaskazini. Kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Assumpta Massoi amefuatilia kile wanachofanya sasa ili kuweza kujikimu.
Hii leo jaridani tunaangazia ajali mbayá ya meli katika pwani ya Djibouti lililokuwa linabeba wahamiaji wengi. Pia tunasalia hapa makao makuu ambapo Kikao cha 18 cha Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu COSP18. Mashinani tutakwenda nchini DRC.Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, (IOM) kwa ushirikiano wa karibu na mamlaka za Djibouti, linaongeza juhudi zake za kibinadamu kufuatia tukio la kusikitisha lililotokea pwani ya Djibouti ambapo takriban wahamiaji wanane walikufa maji na wengine 22 hawajulikani walipo.Katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Kikao cha 18 cha Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu COSP18, kinaendelea na mwaka huu, mada kuu ni kuongeza uelewa wa haki na mchango wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya kijamii. Miongoni mwa washiriki ni ya kijana kutoka Louisiana, hapa Marekani.Makala tutasalia hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York Marekani ambapo Kikao cha 18 cha Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu COSP18, kinaendelea na tutamsikiliza mmoja wa washiriki wa mkutano huu Bongani Simphiwe Makama kutoka Ufalme wa Eswatini ambaye amepata nafasi ya kuzungumza na idhaa ya Kiswahili.Na katika mashinani fursa ni yake fursa ni yake Byamungu Rukera, Mwakilishi wa watu waliokimbia makazi yao huko Sake, Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC akipazia sauti wakimbizi wenzake kwa wafanyakazi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na misaada ya dharura OCHA ambao wanawagawia chakula licha ya uhaba wa msaada huo.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Kikao cha 18 cha Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu – COSP18 – kinaendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ikiangazia juhudi za kimataifa za kuhakikisha usawa na ujumuishaji kwa watu wenye ulemavu. Miongoni mwa washiriki ni Bongani Simphiwe Makama mwakilishi wa watu wenye ulemavu kutoka Ufalme wa Eswatini, ambaye amepata nafasi ya kuzungumza na Idhaa ya Kiswahili kuhusu uzoefu wake, yale aliyojifunza, na changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu nchini kwake. Sharon Jebichii na Makala zaidi.
Katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Kikao cha 18 cha Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu COSP18, kinaendelea na mwaka huu, mada kuu ni kuongeza uelewa wa haki na mchango wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya kijamii. Miongoni mwa washiriki ni ya kijana kutoka Louisiana, hapa Marekani. Je amesema nini? Flora Nducha na taarifa zaidi
Hii leo jaridani tunaangazia mvutano unaoendelea barani Asia kati ya majirani wawili India na Pakistani, na msaada wa mguu bandia uliowezesha mtototo nchini Kenya kwenda shule. Makala tunakupeleka nchini Tanzania na mashinani tunakwenda katika ukanda wa Gaza.Huko barani Asia majirani wawili India na Pakistani wameendelea kuoneshana mvutano kati yao kwenye eneo la Jammu na Kashmiri tangu tarehe 22 mwezi uliopita wa Aprili baada ya shambulizi huko Pahalgam. Katibu Mkuu ametoa wito kwa mara nyingine tena.Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF kwa kushirikiana na wadau wameleta neema kwa watoto wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Kisumu Magharibi mwa Kenya baada ya kuwapa msaada wa vifaa ikiwemo viti mwendo na viungo bandia kupitia mradi wa ubunifu kwa ajili ya watoto wenye ulemavu, msaada uliobadili maisha yao.Makala katika wiki ya chanjo duniani, iliyotamatishwa tarehe 30 wiki iliyopita, mtaa wa Butiama, ulioko Mtoni Kijichi katika wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania ulishuhudia wazazi na walezi wakijitokeza kuwapatia watoto wao chanjo muhimu za kuwalinda dhidi ya maradhi hatari. Miongoni mwao ni Hija Halfani ambaye alimpeleka mtoto wake mwenye umri wa siku 42 kupata chanjo yake ya kwanza.”Na mashinani mashinani, kama sehemu ya juhudi za kutoa nafasi ya kujieleza kisanii na kuwaunga mkono Wapalestina kihisia (emotional support), UNRWA imeandaa maonesho ya sanaa katika Shule ya Al-Rimal, ambayo sasa ni makazi ya wakimbizi wa ndani katika ukanda wa Gaza, na watoto walipata fursa ya kuonesha kazi za sanaa zinazoakisi(reflect) madhila wanayopitia wakati wa vita kati ya Israeli na Hamas ambavyo bado vinaendelea. Malak Fayad, msichana mkimbizi kutoka Beit Hanoun ni mmoja wao akionesha sanaa yake.….Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Katika Wiki ya Chanjo duniani, iliyotamatishwa tarehe 30 wiki iliyopita, mtaa wa Butiama, ulioko Mtoni Kijichi katika wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, nchini Tanzania ulishuhudia wazazi na walezi wakijitokeza kuwapatia watoto wao chanjo muhimu za kuwalinda dhidi ya maradhi hatari. Miongoni mwao ni Hija Halfani ambaye alimpeleka mtoto wake mwenye umri wa siku 42 kupata chanjo yake ya kwanza. Je, ni mafanikio gani yamepatikana na kwa nini chanjo hizi ni muhimu? Ungana na Sharon Jebichii kwa makala hii iliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Tanzania.
Hii leo jaridani tunaangazia hali ya kibinadamu katika ukanda wa Gaza, na harakati za utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili. Makala tunasalia hapa hapa makao makuu na mashinani tunakwenda nchini Burundi, kulikoni?Hali si hali huko Ukanda wa Gaza eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli ambako wakimbizi wa ndani wanakabiliwa na hatari za kiafya ambako panya na wadudu kama vile viroboto na nzi wamesambaa kutokana na mlundikano wa taka na ukosefu wa huduma muhimu kama vile maji safi na salama.Hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, mkutano wa 24 wa Jukwaa la Kudumu la Watu wa jamii za asili (UNPFII) linaendelea kujadili utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili na kubaini mbinu bora za kushughulikia changamoto zinazowakabili. Miongoni mwa shiriki wa jukwaa hilo nimwakilishii wa Shirika la Ereto Solidarity Funds ambaye amepata fursa ya kuzungumza na Sharon Jebichii wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.Makala ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Kitabu na Haki Miliki ambapo kila mwaka tarehe kama ya leo siku hii huadhimishwa ili kutambua nguvu ya vitabu kama daraja kati ya vizazi na vizazi na tamaduni mbalimbali. Anold Kayanda wa Idhaa hii amezungumza na mwandishi maarufu wa vitabu vya elimu, Uchumi na uhamiaji, Ernest Makulilo mkazi wa Marekani katika jimbo la Missouri.Na mashinani kupitia video iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO fursa ni yake Meena Poudel kutoka nchini Nepal, Kusini mwa Asia ambaye ni Katibu wa kikundi cha wanawake watumiaji wa msitu ambacho kinabadilisha takataka za misitu kuwa mbolea rafiki kwa mazingira huku pia wakijipatia kipato."Mwenyeji wako ni Flora Nducha, karibu!
Mkutano wa 24 wa Jukwaa la Kudumu la Watu wa jamii za asili (UNPFII) hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa linaendelea kujadili utekelezaji wa Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wa asili na kubaini mbinu bora za kushughulikia changamoto zinazowakabili. Miongoni mwa shiriki wa jukwaa hilo nimwakilishii wa Shirika la Ereto Solidarity Funds ambaye amepata fursa ya kuzungumza na Sharon Jebichii wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa. Anaanza kwa kujitambulisha
Jukwaa la Vijana la Baraza la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Kiuchumi na Kijamii (ECOSOC) linafanyika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ambapo limeanza tarehe 15 Aprili na linatarajiwa kukamilika tarehe 17 Aprili 2025. Vijana kutoka nchi mbalimbali pamoja na wadau wengine wa masuala ya maendeleo na Uchumi wanakuja pamoja kujadili changamoto mbalimbali na namna bora ya kupatia ufumbuzi katika kuubadilisha ulimwengu kuwa mahali penye usawa zaidi na endelevu chini ya mwongozo wa Ajenda ya mwaka 2030 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Miongoni mwa wanaohudhuria jukwaa hilo ni Kapwani Kavenuke kutoka nchini Tanzania ambaye amefanyiwa mahojiano na Leah Mushi na hapa anaanza kwa kueleza umuhimu wa mikutano huo.
Tarehe 15 mwezi April imwaka 2023 wananchi wa Sudan hususan mji mkuu Khartoum waliamshwa na mapigano kati ya jeshi la serikali SAF na wanamgambo wa kikosi cha msaada wa haraka RSF. Hadi leo hii mapigano hayo yanazidi kushika kasi na raia wanafurushwa makwao. Miongoni mwao ni watoto ambao zahma wanayokutana nayo sio tu kufurushwa bali pia changamoto ya afya ya akili. Tayari shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limeona shida hiyo na limeanza kuchukua hatua kama anavyosimulia Assumpta Massoi kwenye makala hii.
Mkutano wa 69 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani, (CSW69) umeingia siku ya tatu hii leo Machi 12 katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijinoi New York, Marekani. Mkutano huu wa mwaka huu unafanyika katika hali ya kihistoria kwa kuzingatia kuwa ni miaka 30 tangu Mkutano wa wanawake ulipofanyika jijini Beijing - China mwaka 1995 na kuweka maazimio muhimu kuhusu masuala mazito ya kumkomboa mwanamke dhidi ya ukandamizaji kote duniani. Maelfu ya wanawake na wadau wengine wanakutana kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York. Miongoni mwao ni Nuria Mshare ambaye amewakilisha taasisi ya Haki Elimu ya nchini Tanzania.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO nchini Tanzania linaendelea kutekeleza Programu ya pamoja kwa mkoa wa Kigoma KJP iliyoanza kutekelezwa nchini humo mwaka 2017 na mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa lengo la kusaidia kutatua changamoto za kipekee za mkoa huo ikiwemo zitokanazo na kuhifadhi wakimbizi kutoka nchi jirani.Miongoni mwa miradi inayotekeleza ni ule wa kupatia wananchi mafunzo ya ufugaji bora wa mbuzi ili waweze kuinua kipato chao na vile kuimarisha lishe kwenye familia.Kupitia video ya FAO, utamsikia mnufaika wa mafunzo hayo kama anavyosimulia Assumpta Massoi kwenye makala hii.
Baada ya waasi wa M23 jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kupatia wakimbizi waliokuwa wamesaka hifadhi kambini mjini Goma, wawe wamerejea makwao ndani ya saa 72 kuanzia juzi jumatatu, mamia wameanza kutii amri hiyo licha ya hofu inayowakabili ya kule wanakotakiwa kurejea. Miongoni mwao ni Kibira Bakulu, baba wa watoto 5, aliyekimbia mapigano eneo la Saké, mwezi Februari mwaka jana, takriban kilomita 10 kutoka Goma.
Baada ya waasi wa M23 jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kupatia wakimbizi waliokuwa wamesaka hifadhi kambini mjini Goma, wawe wamerejea makwao ndani ya saa 72 kuanzia juzi jumatatu, mamia wameanza kutii amri hiyo.Miongoni mwao ni Kibira Bakulu, baba wa watoto 5, aliyekimbia mapigano eneo la Saké, mwezi Februari mwaka jana, takriban kilomita 10 kutoka Goma.Akiwa katika harakati za kubomoa kibanda chake katika kambi ya nane ya CEPAC Mugunga huko Goma, Bwana Bakulu anasema walishangaa, bila kuwa tayari, kuambiwa warudi walikotoka."Tumepatiwa saa 72 tuwe tumeondoka na kurejea Saké, kwani vita vimeisha. Sisi hatua uhakika kamili kwa sababu tuliondoka Saké kutokana na vita. Kama inabidi kusukumwa tuondoke, hatuna la kuchagua,” amesema Bwana Bakulu.Ana hofu ya kurejea Saké, akisema, “kule tulikuwa tunaishi Sake na tukirejea tutaishi vipi? Tunaomba viongozi wajitahidi watusaidie ili watuhakikishia usalama.Alipoeleza hali halisi amesema, “ hii siku ya leo hapa unaniona, watu wamepita hapa wakifanya vurugu, wananyang'anya kila kitu ulichonacho, iwe simu wanabeba. Sasa tunashindwa kufahamu amani iko katika kiwango gani?”Kwa mujibu wa Bwana Bakulu, walishaamua kuwa hawataweza kurudi na kama ni kufa basi watafia Goma, lakini sasa wamelazimishwa kurejea Saké.
Kundi la waandishi wa habari 15 wanawake kutoka nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania mwaka jana wa 2024 walitumia siku tano jijini Geneva, Uswisi kushiriki programu ya kushirikisha waandishi wa habari ili wapate uelewa wa kazi za Baraza la Umoja wa Mataifa la haki za Binadamu. Ufadhili wao ulikuwa kupitia mashirika mawili ya kiraia, Universal Rights Group (URG) na Friedrich Naumann Foundation. Wakiwa Geneva, walipata fursa ya kuzungumza mabalozi wanaowakilisha nchi zao kwenye Baraza hilo, wataalamu wa haki za binadamu, mashirika ya kiraia na waandishi wa habari ambao kituo chao cha kazi ni Baraza la Haki za Binadamu. Miongoni mwao ni Faraja Kihongole kutoka Africa Media Group Tanzania Limited. Alihojiwa na Pascal Sim, Afisa wa Mawasiliano katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu jijini Geneva kuhusu masuala kadhaa ikiwemo alichojifunza na anachoondoka nacho. Matokeo ya mahojiano hayo ndio makala ya leo inayoletwa kwako na Assumpta Massoi.
Umoja wa Mataifa unaeleza kwamba duniani kote kuna vijana bilioni 1.2 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 24. Idadi hii ni saw ana asilimia 16 ya wakazi wote wa dunia. Kama hiyo haitoshi, idadi hiyo ya vijana inatarajiwa kufikia bilioni 1.3 ifikapo mwaka 2030, yaani miaka mitano ijayo. Lakini changamoto ni kwamba bado serikali nyingi hazijaweza kutumia wingi wa idadi hii kusongesha Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs. Kwa hali hiyo baadhi ya vijana wameamua kutumia fursa na kujiongeza ili vijana wenzao waweze kufahamu wanachopaswa kufanya ili SDGs zifanikiwe ifikapo 2030. Miongoni mwao ni Paul Siniga, kijana kutoka Tanzania ambaye mwezi Oktoba mwaka huu alikuweko kwenye makao makuu ya UN jijini New York, Marekani kushiriki vikao vya ngazi ya juu. Assumpta Massoi alitaka kufahamu kwa kina ni hatua zipi alichukua hadi kufika aliko sasa.
Ujumuishwasji wa lugha mbalimbali katika dunia iliyoshikamana katika Nyanja mbalimbali ni moja ya malengu ya Umoja wa Mataifa kuanzia katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa hadi kwenye nchi wanachama unalichagiza hilo. Hamasa hiyo imezichagiza nchi nyingi kuanza kukumbatia lugha ambazo kwa asili hazizungumzwi kama alivyobaini Flora Nducha wa Idhaa hii ambaye hivi karibuni alikuwa Cuba kwenye Kongamano la Kimataifa la Kiswahili na kukutana na Profesa Juan Jacomino ambaye ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Havana na ni miongoni mwa watu wa mwanzo waliokwenda Tanzania kujifunza Kiswahili na sasa anakifundisha nchini mwake Cuba. Anafafanua kuhusu safari yake ya kujua Kiswahili katika makala hii..
Hivi karibuni mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kuzuia kuenea kwa jangwa, ulikunja jamvi huko Riyadh, Saudi Arabia ambapo Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD ulitumia fursa hiyo kuelezea harakati zake za kusaidia wakulima barani Afrika walioathiriwa vibaya na kuenea kwa jangwa. Miongoni mwa mataifa hayo ni Zimbabwe ambako IFAD imeshaanza kuchukua hatua na kuleta nuru kwa wakulima kama anavyosimulia Assumpta Massoi kwenye makala hii.
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina na tunaelekea nchini Kenya kuangazia moja ya ukiukwaji Mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya wanawake, jinamizi la ukeketaji na jitihada zinazochukuliwa na UNFPA na wadau mbalimbali. Pia tunakuletea muhtasari wa habari na mashinani inayotupeleka nchini Namibia.Baada ya serikali ya Bashar Al-Assad kupinduliwa na kuibuka kwa taarifa za baadhi ya nchi duniani kuanza kusitisha mchakato wa kushughulikia maombi ya Wasyria waliokuwa wameomba hifadhi kuokoa usalama wa maisha yao pindi hali ilipokuwa tete nchini mwao, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) linaendelea kutoa wito kwa mataifa yote kufungua milango, kuwapa hifadhi na ulinzi raia wa Syria wanaotafuta usalama. UNHCR imeahidi pia mara tu hali ya Syria itakapokuwa wazi zaidi, itatoa mwongozo kuhusu mahitaji ya ulinzi kwa Wasyria walioko hatarini.Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limekaribisha mchango wa dola za Marekani milioni 22 kutoka shirika la Korea Kusini la Ushirikiano wa Maendeleo ya Kimataifa (KOICA) ili kuimarisha mnepo kwa tabianchi na uhakika wa chakula kwa wakulima wadogo, wafugaji na makundi yaliyoko pembezoni nchini Kenya, Somalia na Sudan Kusini. Vituo vya utabiri wa hali ya hewa vinatabiri hali ya La Niña mashariki mwa Pembe ya Afrika na uwezekano wa kupunguza mvua katika kipindi hikiNa walinda amani wa kikosi cha 11 cha Tanzania -TANZBATT-11 kinachohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO jimboni Kivu Kaskazini wametunukiwa nishani ya umoja wa mataifa ikiwa ni alama ya kufanya kazi kwa utii,uhodari na uaminifu. Miongoni mwao ni Private Selina Kisemvule.Katika mashinani ikiwa ni siku ya mwisho ya maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, fursa ni yake Rais Nangolo Mbumba wa Namibia ambaye kupitia ukurasa wa X wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu, UNFPA anawahimiza wananchi na dunia nzima kwa jumla kusimama kidete ili kutokomeza unyanyasaji wa kijinsia.Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!